Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Richard Wambali akifungua Semina
ya uelimishaji kwa Waajiri kuhusu haki na wajibu wa mwajiri na
mfanyakazi jijini Dar es Salaam jana.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi Laura Kunenge akichangia mada katika semina ya
uelimishaji kwa Waajiri kuhusu haki na wajibu wa mwajiri na mfanyakazi
jijini Dar es Salaam leo (jana).
Mwanasheria Mwandamizi Mfuko wa
Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Deogratius Ngowi akitoa mada katika Semina
ya uelimishaji kwa Waajiri kuhusu haki na wajibu wa mwajiri na
mfanyakazi jijini Dar es Salaam leo (jana).
Baadhi ya washiriki wa semina ya
uelimishaji kwa waajiri wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi wa
semina hiyo ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi
(WCF) Richard Wambali (Picha Zote na Benjamin Sawe)
…………………………….
NA BENJAMIN SAWE
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi
(WCF), umeendesha semina ya siku moja kwa waajiri nchini ili kutoa
elimu juu ya shughuli za Mfuko na wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi wao
katika kujisajili na kuwalipa michango kwa niaba ya waajiriwa wao.
Akizungumza katika semina hiyo
Mjumbe wa Bodi ya Mfuko huo Richard Wambali amesema kuanzishwa kwa
mfuko huo kumekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inaelekea katika
uchumi wa viwanda hivyo kupelekea ongezeko la wafanyakazi ambapo chombo
hicho ndio mkombozi wa majanga yatokanayo na kazi.
“Ni muda muafaka kwa waajiri
kutambua wajibu wenu katika Mfuko huu na pia kutambua madhara ya
kutotekeleza wajibu wenu” Alisema Bw. Wambali.
Alisema Mfuko huo ulioanzishwa
kwa sheria ya bunge namba 20 kifungu cha 5 ya mwaka 2008, una madhumuni
ya kutoa fidia kwa Wafanyakazi kutokana na ulemavu au vifo
viinavyosababishwa na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi sambamba na
kukuza mbinu za kuzuia matukio ya ajali.
Katika hotuba yake, Bw Wambali
alieleza umuhimu wa waajiri kuwalipia michango wafanyakazi wake kama
sheria inavyotaka, ili kuwawekea akiba pindi wapatapo na majanga wakiwa
kazini.
Mfuko huo ambao umeanza kazi
rasmi Julai 1, 2015, lengo kuu ni kutekeleza nia ya Serikali kukabiliana
na changamoto za ulipaji wa fidia kwa Wafanyakazi katika mfumo wa
utoaji fidia uliokuwepo awali
Bw.Wambali alizitaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na kiwango kidogo cha malipo ya
fidia(kiwango kisichozidi shilingi 180,000) kwa ulemavu wa kudumu na
shilingi 83,000 kwa wategemezi endapo kifo kitatokea kwa Mfanyakazi
husika.
Akinukuu sheria iliyoanzisha
Mfuko huo, Bw. Wambali alisema, kifungu cha pili (2), cha sheria ya
fidia kwa wafanyakazi namba 20/2008 cha mfuko huo unawahusu Waajiri na
Wafanyakazi wote katika sekta ya Umma na Binafsi, Tanzania Bara pekee.
“Naomba ieleweke, anayepaswa
kuchangia kwa mujibu wa sheria hii ni Mwajiri na sio mfanyakazi kukatwa
mshahara wake.” Alifafanua Bw. Wambali.
Akizungumza wakati akitoa mada
Afisa Matekelezo Bw. Musa Mwambujule amesema, Mfuko umeamua kuandaa
semina hiyo ili kutoa elimu zaidi kwa waajiri kwa kutambua kuwa waajiri
ndio wadau wakuu wa Mfuko huo na semina hiyo itawasaidia kujua kazi za
Mfuko lakini pia wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi katika kutoa michango
ya kila mwezi.
Nae, Mwanasheria wa Mfuko huo
Bw. Deogratius Ngowi, alisema, Mfuko huo upo kisheria ili kutoa fidia
kwa wafanyakazi watakaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi
ni Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na umeundwa kwa
mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi Sura ya 263
iliyorejewa Desemba, Mwaka 2015.
SHARE
No comments:
Post a Comment