Tarehe 12 Juni kila mwaka ni siku ya kupinga ajira kwa
watoto duniani. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watoto milioni 168 kote
duniani wanatumikishwa kufanya kazi.
Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia watoto
UNICEF, takriban watoto 40,000 wanafanya kazi katika migodi iliyo na
madini ya Cobalt katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wakifanya kazi
saa nyingine hadi saa 24 ndani ya migodi, watoto hao hulipwa chini ya
dola mbili kwa siku na wengi wao hupokea ujira mdogo kuliko huo.Faustin Adeye anayefanya kazi na shirika la Kikatoliki la Misereor ameliambia shirika la habari la DW kuwa mazingira ya kazi migodini nchini humo ni ya kusikitisha na kuongeza kuwa watoto wengi huathirika kimwili kutokana na kufanya kazi katika migodi hiyo.
Adeye ameongeza kusema hali katika migodi kadhaa kusini mwa Congo ni mbaya mno kiasi cha kwamba saa nyingi watoto wao huzikwa wakiwa hai wakati migodi hiyo inapoporomoka.
Watoto Congo wanafanya kazi katika mazingira hatari
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema baadhi ya watoto hao ni wa umri mdogo wengine wakiwa na umri wa miaka saba na huwa hawana vitenda kazi vipasavyo kama mavazi ya kuwakinga dhidi ya madhara ya uchimbaji madini.
Madini hayo adimu ya Cobalt hutumika kutengezea betri za simu za kisasa za mkononi.
Mashirika makubwa kama Apple, Microsoft, Samsung na Sony yanategemea madini hayo ya Cobalt kutengezea bidhaa zao za kielektroniki.
Madini hayo pia yanatumika katika magari ya kieletroniki yanayotengezewa na kampuni kama Daimler na Volkswagen. Hata hivyo kampuni hizo hazikutaka kuhusishwa na biashara ya watoto kutumikishwa katika ajira.
Mnamo mwezi Desemba mwaka jana, DW ilizitaka baadhi ya kampuni hizo kuzungumzia suala hilo la watoto kuajiriwa Congo kuchimba madini.
Daimler, mojawapo ya kampuni kubwa za kutengeneza magari Ujerumani ilijibu kwa maandishi kuwa inahitaji watu wanaowauzia bidhaa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo za kimataifa.
Kampuni za simu na magari zinawajibika?
Daimler ilisema muongozo wa kampuni hiyo kuhusu mazingira ya kazi, viwango vya kijamii na kimaadili pamoja na uhifadhi wa mazingira unakwenda mbali ya vigezo vya kisheria vya kuzingatia yote hayo na kuongeza kuwa inatarajia wanaowauzia bidhaa za kutengeza magari yao kuheshimu na kuzingatia angalau vigezo vyote hivyo.
BMW, kampuni nyingine ya Ujerumani ya kutengeza magari imekubali kuwa imetumia madini ya Cobalt kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo katika utengezaji wa baadhi ya betri zao na kutangaza kuwa itaanzisha ukaguzi wa kuhakikisha wanaowauzia bidhaa hiyo hawakiuki sheria za haki za binadamu.
Kampuni ya Marekani ya Apple ilitangaza mwezi Machi kuwa inanuia kukoma kununua cobalt inayochimbwa kwa kutumia mikono kutoka Congo.
Asilimia kubwa ya madini hiyo adimu inapatikana Katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Kulingana na Amnesty International, karibu asilimia 50 ya madini hayo yanapatikana nchini humo.
Shirika la kimataifa la wafanyakazi lilianzisha siku hii ya tarehe 12 Juni kuwa ya kupinga ajira kwa watoto mnano mwaka 2002 ili kuangazia masaibu yanayowakumba watoto.
Mwaka huu, mada itakuwa ni jinsi gani mizozo na majanga inavyoathiri watoto hadi kulazimika kufanyishwa kazi. Vita na majanga yanatishia haki za binadamu.
Mara nyingi watoto ndiyo huathirika zaidi kwa kukosa elimu na hata kupoteza familia zao na hivyo kuwalazimu kufanya kazi.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment