TRA

TRA

Sunday, June 18, 2017

Duh! aibu yao, aibu yetu?

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !

Said Mwishehe

KWA Ujinga Wangu natamani Rais John Magufuli asirudi nyuma katika kupigania rasilimali za nchi yetu na hasa madini.

Natamani aendelee na jukumu hilo ambalo ameamua kulifanya kwa niaba yetu.Wapo wanaobeza eti hooo hakuna lolote ndio yale yale tu.

Ukiuliza yale yale yapi? Hawana majibu.Yaone kwanza, sijui yakoje.Ukweli lazima ubaki pale pale Rais amefanya kazi ambayo wengi hawakuamini kama anaweza kuifanya.

Nikweli kwa muda mrefu Watanzania wanatamani kuona madini yetu yanatunufaisha.

Kwa bahati mbaya kasi ya kuyalinda madini yetu haikuwa kubwa.Hivyo tulisema kwa kiwango chetu lakini hakukua na hatua zaidi.

Kwa Ujinga Wangu nilitamani kuona siku moja anatokea mmoja wa Watanzania ambaye atasema sasa imetosha na lazima madini yetu yalindwe kwa nguvu zote.

Kumbe wakati nikitamani kuwa na mtu wa kuongoza mapambano dhidi ya kulinda madini yetu, Mungu amemleta Rais John Magufuli.

Hakika anafanya kazi  inayohitaji moyo wa chuma kuifanya. Siku za karibuni wakati anapokea ripoti ya pili inayohusu mchanga wa madini maarufu kama Makinikia ameweka wazi naye ni binadamu na anayo damu.

Nafahamu mimi na wewe tuna damu.La kujiuliza tunazitumia vipi kwenye masuala yanayohusu nchi yetu?

Rais amejitoa kwa kuamua kuwa mstari wa mbele kuvunja woga wa siku wa kushindwa kusimamia rasilimali zetu.

Hongera Rais  Magufuli .Uzalendo wako umeonekana na kila mmoja wetu.Jina lako Rais kuna siku litaandikwa kwa wino wa dhahabu.

Ungeweza kukaa kimya lakini nafsi yako iliona hutatenda haki kwa Watanzania wenzako, hivyo umeamua kuchukua hatua lazima tukuunge mkono.

Kwa Ujinga Wangu huwa najiuliza hawa ambao walikuwa wanafuja madini yetu na kuyaauza kwa bei chee walikuwa wanafikiria nini?

Walidhani watanufaika milele? Ama kweli hakuna lenye mwanzo likakosa mwisho.

Waliokuwa wameweka mirija ya kula fedha za madini bila kufuata utaratibu sasa imefika mwisho wao.Hawana la kufanya tena zaidi ya kuona aibu tu.

Maana ripoti zote mbili  zilizoundwa na Rais kuchunguza makontena ya mchanga wa madini  zimethibitisha namna ambavyo nchi imeliwa. Haikuwa kazi rahisi lakini uliona bora ifanyike na liwalo na liwe.


 Rais John Magufuli (kulia) akifurahia jambo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete
 
Kwa Ujinga Wangu najiuliza aibu yao au aibu yetu?Jibu ni moja tu aibu yao maana walidhani hawatajulikana kwa namna ambavyo wameyatumia vibaya madini yetu.

Rais amesema hakuna cha rafiki wala ndugu kila aliyehusika kuitia nchi hasara naye achunguzwe.

Tunafahamu madini ambayo yapo ndani ya ardhi ya Tanzania hayakuja kwa bahati mbaya bali Mungu aliamua kuyaweka kwetu akimini yatatutoa katika umasikini.



Kwa bahati mbaya baadhi ya kampuni zinazojihusisha na madini zikatumia uwepo wa madini yetu kunufaisha wengine kabisa tofauti na Watanzania.

Kwa miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu , tumekuwa tukishuhudia kampuni za kigeni zikipigana vikumbo kwa ajili ya kuchimba madini yetu.

Kumbe walikuwa wanajua wanachokifanya.Unauliza kipi? Kwani  hujasikia? Hasara ambayo nchi yetu imeipata kwasababu ya madini yetu kuchukuliwa bila utaratibu hujaisikia kwenye ripoti za kamati zote mbili?

Kwa Ujinga Wangu, natamani Watanzania wote tuwe na dhamira kama ambayo Rais wetu anayo kwenye kupigania rasilimali zetu.

Tukimuunga mkono kwa asilimia 100 tutashinda.Rais amesema vita ya kiuchumi ni ngumu , hivyo lazima tuwe nyuma yake ili kuifanikisha.

Ukisikiliza mijadala huko mtaani kuna baadhi ya watu wao akili yao muda wote wanawaza siasa tu.Kila ambacho Rais anakifanya utasikia anatafuta kura za mwaka 2020.

Sijui wakoje?Wanakera kweli.Rais anapigania rasilimali za nchi yetu kwasababu ya uzalendo alionao kwa anaowangoza na si kwasababu anatafuta kura.

Kazi anayoifanya kila mmoja wetu anaijua, hivyo tuache kubeza anachokifanya bali tumuunge mkono ili atimize kile anachokipigania kwa ajili yetu.

Kwa Ujinga Wangu natamani waliohusika wachukuliwe hatua kama zile za nchi ileeeee ya kule mbali.Natania tu , nachotaka kusema ni vema sheria ikachukua mkondo wake.Haki itendeke.Naiona Tanzania yenye neema kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa maoni
0713833822

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger