TRA

TRA

Sunday, June 18, 2017

Matumizi sahihi ya rasilimali zetu

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !





Julian Msacky

SERIKALI ya Awamu ya Tano imefumbua Watanzania macho. Imeonesha namna tunavyoibiwa rasilimali zao kila kukicha.

Mfano nzuri tumeuona kwenye sekta yetu ya madini ambako ufujaji mkubwa wa mapato unafanyika kwa kiwango kikubwa.

Kama tulivyosikia ama kuambiwa na Rais Magufuli ni kwamba kiwango tunachopata ni kidogo ukilinganisha na kinachopotea.

Hii ina maana kuwa Tanzania si maskini, lakini ni wa kujitakia ndiyo maana Rais anasema “Watanzania tumelogwa na nani?”

Katika safu hii ya leo ninapenda kuzungumzia matumizi sahihi ya rasilimali za nchi katika kuharakisha maendeleo yetu.

  Rais John Magufuli

Ninazungumzia hili baada ya kubaini kuwa rasilimali zetu nyingi hazitumiki ipasavyo ndiyo maana tunashindwa kupiga hatua inavyotakiwa.

Kwa msingi huo ninashauri ama kupendekeza mfumo unaofaa wa kutumia rasilimali zilizopo kukuza sekta mbalimbali nchini.

Ninadhani umefika wakati sasa tuweke utaratibu wa kutumia rasilimali mathani madini ya dhahabu pekee kuhudumia sekta ya elimu.

Hii ikiwa na maana kuwa mapato yanayotokana na madini kama nchi tunaweza kuamua ni kwa ajili ya kuhudumia shule za msingi tu.

Kwa maana kuwa watoto wasome bure, wapatiwe vitabu muhimu na vitendea kazi bora kwa walimu na mazingira bora ya kufundishia.

Hatuna sababu ya kuumiza vichwa namna gani watoto wetu wasome wakati tunao utajiri wa kutosha kufanya mambo hayo vizuri.

Hatuna sababu ya walimu kutolipwa vizuri au kukosa nyumba bora za kuishi wakati mali zetu zinasombwa kama hazina wenyewe.

Tangu tumeanza kuchimba madini hadi sasa ninaamini hatuna mfuko maalumu wa mapato hayo na badala yake tunazitumia tunavyojua.

Mimi naamini tukiweka mfumo wa kila rasilimali kuhudumia eneo fulani itasaidia kuliko ilivyo sasa kwani tunapoteza vingi. 

Hebu tujiulize kama Libya chini ya Muammar Gaddafi alitumia mafuta kuifanya nchi hiyo na watu wake kuishi vizuri, sisi tunashindwa nini.

Gaddafi alisomesha wanafunzi hadi vyuo vikuu kwa mapato ya mafuta, akawajengea nyumba, akawapatia umeme, maji na vingine vingi.

Alifanya hivyo kwa kutumia rasilimali ya mafuta. Alitumia pia rasilimali hiyo kwa usahihi kusaidia mataifa mengi tu ya Afrika.

Hicho ndicho kilichowaudhi mabepari na kumuua. Hicho ndicho pia kilichosababisha Saddam Hussein wa Iraq auawe.

Kwa hiyo utamaduni wa kutumia mapato yatokanayo na rasilimali zetu kiholela utakoma endapo kila rasilimali itahudumia upande wake.

Tunaweza kufanya hivyo kwa majaribio chini ya usimamizi imara na kuangalia je, dhahabu inamudu kuendesha sekta ya elimu?

Hili linawezekana kwa sababu Rais Magufuli alipoingia madarakani amefanya mabadiliko makubwa na mafanikio yanaonekana.

Kwa mfano, alisimamia suala la upungufu wa madawati shuleni na leo hii nadhani hakuna shule yenye tatizo hilo kwa kiwango kikubwa. 

Alianzisha kampeni ya usafi na hadi sasa inaendelea ingawa baadhi ya mikoa, ikiwemo Dar es Salaam hali bado si nzuri.

Hii maana yake ni nini. Maana ni kuwa tuna tatizo la uongozi kuanzia idara moja hadi nyingine ndiyo maana tunakwama.

Kwa hiyo Rais amezibua mirija ambayo iliziba ndiyo maana tunaona mambo yanakwenda. Hii ni changamoto nyingine.

Ni kwa hiyo njia tunatakiwa tuanze kuweka mifumo ambayo itasaidia kuboresha huduma zetu za kijamii kwa kutumia rasilimali asilia.

Kama utajiri wa kutosha tunao ni kwani tusijiwekee utaratibu wa kila rasilimali iliyopo nchini ishughulike kutatua jambo fulani.

Utajiri uliopo hatuna sababu ya wananchi kukosa huduma bora za afya. Uwezo wa serikali kuwapitia huduma nzuri upo.

Kwa utajiri tuliona nao tuna uwezo wa kutoa tiba bure kwa Watanzania. Mathalan tukitenga mapato yatokana na misitu tutashindwa nini.

Mlima Kilimanjaro umetuingizia mapato mangapi tangu tupewe bure na Mwenyezi Mungu? Hayatoshi kuhudumia sekta ya afya?.

Wakati tuna chanzo hiki, hebu tujiuze ni kwa nini tuangalia wananchi wakifa, wakiwemo wajawazito kwa kukosa huduma bora.

Hivi kweli tulistahili kukosa zahanati, vituo na hospitali za kutosha nchini kwetu au ni kwa sababu tu ya kusimamia rasilimali zetu vibaya.

Tulistahili kweli kuwa na shule zisizo na vyoo katikati ya utajiri uliopo nchini au ni matumizi holela ya utajiri tuliopewa na Mungu?

Inabidi tuseme imetosha. Kama wazungu wanatumia mali hizi hizi kufanya mataifa yao yaonekane kama peponi, tunashindwa nini.

Leo hii ukienda Marekani inang’aa. Ukienda Uingereza inang’aa. Ukienda Canada vivyo hivyo. Hivi tatizo letu ni nini?

Ni lazima tubadilike. Ni lazima viongozi nao wabadilike na kutuonesha kuwa Tanzania inaweza kuwa kama Marekani. Naam.

Haiwezekani mali zetu zineemeshe mataifa hayo halafu tukimbilie kwao kwenda kutibiwa kwa sababu eti wana hospitali nzuri.

Tunazo mali za kuweka hospitali hizo. Ni wapi tuanzie ndiyo mjadala tunaofungua hapa. Ninaamini tukiamua inawezekana.









Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger