
Na Daudi Manongi, MAELEZO, DODOMA.
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu
wa Rais(MUUNGANO NA MAZINGIRA) imelenga kupanda miti zaidi ya milioni
280 kila mwaka katika maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali
ya jangwa na ukame.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais(MUUNGANO NA MAZINGIRA) Mhe.January Makamba alipokuwa
akiongea na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya kupambana
na kuenea kwa hali ya jangwa na Ukame Duniani inayofanyika tar 17 Juni
kila mwaka.
“Ukataji wa miti kiholela na
uharibifu wa misitu unaosababishwa na utegemezi mkubwa wa binadamu wa
kupata mahitaji kutokana na mazao ya misitu pamoja na huduma zingine
muhimu,kunazidisha ukubwa wa tatizo hili”,Aliongeza Mhe.Makamba.
Aidha Waziri Makamba amesema kuwa kutokana na athari hizi Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na taizo hili.
Serikali imeandaa mkakati wa Taifa
wa kupanda na kutunza miti wa mwaka 2016-2021 ambao unalenga kupunguza
kasi ya uharibifu wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na
kuhakikisha kwamba kila mwananchi anahusika katika utaratibu huu.
Maelekezo hayo ni pamoja na
programu za upandaji miti,kuandaa mpango bora wa matumizi ya
ardhi,kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa,ufugaji bora na wa
kisasa na kusisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi
wa kuni na mkaa pamoja na kuhifadhi maji katika kipindi cha mvua.
Ametoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu.
“Kauli mbiu ya mwaka huu ni Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa manufaa ya baadaye
hivyo wananchi wote washiriki kikamilifu katika kuitekeleza ili
kuhakikisha ardhi yetu inatunzwa kwa ajili ya kizazi kijacho”,Aliongeza
Makamba
Mwaka 1994 Baraza la Umoja wa
Mataifa liliazimia na kuitangaza tarehe 17 mwezi juni ya kila mwaka kuwa
ya maadhimisho ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na
ukame.
SHARE
No comments:
Post a Comment