
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya ,
Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis
Kigwangalla wakati Tamasha la Uelimishaji na Upimaji Afya na Kinga dhidi
ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na vijana kwenye uwanja wa
michezo wa shule ya msingi Kinyerezi. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akihutubia kwenye Tamasha la Uelimishaji na Upimaji
Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na vijana
kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi Kinyerezi
NA MWANDISHI MAALUM
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kote
nchi kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto kijinsia ili
waweze kukamatwa na kuchukua hatua za kisheria kama hatua ya kukomesha
vitendo hivyo ambayo vimeanza kushamiri katika baadhi ya jamii nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo katika
hotuba yake ya kuhitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ambayo ilitoa huduma bure za vipimo na matibabu kwa watoto na
vijana zaidi ya 1500 kampeni ambayo iliambatana na maadhimisho ya siku
ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi mkoani
Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema kuwa
watenda maovu hao lazima vifichuliwe na wananchi, walezi pamoja na
wazazi kwa kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya udhalilishaji wa
watoto wapo miongoni mwa jamii.
Katika kukabiliana na hali hiyo,
Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya dola kutofumbua macho vitendo hivyo
bali pindi wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji wa watoto
wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki
watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya.
Makamu wa Rais pia ametoa wito
maalum kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini waache
kuwaficha watu wanaotendea vitendo hivyo vibaya bali wawapatie taarifa
walimu wao na polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.
Amesema kwa kufanya hivyo watoto
watakuwa salama katika mazingira ya nyumbani na wakiwa mashuleni kwani
watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo watawajibishwa kulingana na matendo
maovu waliyokuwa wanawafanyia watoto hao.
“Mtoto anaweza kufaidika na fursa sawa iwapo tu atalindwa kwa kuwezeshwa kuwa afya bora”, Amesisitiza Makamu wa Rais.
Kuhusu kukabiliana na magonjwa
yasiyo ya kuambukiza, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema
magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameendelea kuua watu kwa kasi katika nchi
zinazoendelea Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.
Amesema ipo haja ya kuimarisha
juhudi za kukabiliana na tatizo hilo kwa ushirikiano wa wadau wote kwani
janga hilo linagharimu taifa na wananchi wake wakiwemo watu wazima,
watoto na vijana.
“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza
yasipodhibitiwa yatapunguza uzalishaji mali,ufanisi mahali pa kazi na
hata shughuli za ulinzi na usalama nchini mwetu na hivyo pato la taifa
litapungua na taifa kuwa watu maskini kutokana na magonjwa hayo”, Alifafanua Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema kuwa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza
Serikali imeweza kupanua maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa
saratani nchini kwa kujenga jengo jipya katika Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road na kuongeza majengo mapya ya huduma za saratani kwenye
Hospitali za Rufaa ya kanda ya Bugando mkoani Mwanza.
Amesema Serikali pia imejenga
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo ni taasisi ya mfano ya kutibu
maradhi ya moyo ambapo kutokana na kujengwa kwa taasisi hiyo Serikali
imefanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambayo yangetumika kuwagharamia
wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Hamisi Kingwangala
amemhakikishia Makamu wa Raia kuwa Wizara hiyo itaendelea kuweka
mipango na mikakati imara ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza nchini.
Dkt Kingwangala ameomba wadau
mbalimbali zikiwemo taasisi za kidini na wadau wengine kushirikiana na
Wizara ya Afya katika kuongeza kasi ya kukabiliana na magonjwa hayo ili
yasiendelee kuteketeza maisha ya watu nchini.
SHARE
No comments:
Post a Comment