Mshauri wa Kiufundi wa MIVARF, Bw. Ravi Malik
(kushoto) akimkabidhi zawadi kutoka NABAD Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (kulia).
NA
MWANDISHI WETU
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa
kushirikiana na Benki ya Taifa ya Kilimo na Maendeleo Vijijini India
(NABAD) na Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma
za Kifedha Vijijini (MIVARF) zimeanza kutoa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za
Ukopeshaji katika Kilimo.
Mafunzo hayo ya siku sita (6) yanalenga kuwajengea
uwezo watoa huduma hasa kutoka mabenki na taasisi za kifedha nchini kuweza
kutoa huduma kwa wakulima kwa wakati na kuzingatia tija wakulima nchini ili
kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya
Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye
ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa TADB
alisema kuwa katika kuunga mkono kwa vitendo juhudi za serikali kuinua ukuaji
wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, TADB imeamua kuwajengea uwezo
wadau kutoka mabenki na taasisi za kifedha nchini kwa kushirikiana na
NABAD na MIVARF ili kuweza kutoa huduma kwa uhakika ili kuwakomboa wakulima
nchini.
“Mafunzo haya yanalenga kuunga mkono juhudi za
Serikali ili kuharakisha mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo,
ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini
na pia kutoa kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya
viwanda vya nchi,” alisema.
Bw. Assenga aliongeza kuwa TADB imedhamiria na
kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta
Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia kuyajengea
uwezo mabenki na taasisi za kifedha ili kuchagiza upatikanaji na utoaji wa
fedha ili kusaidia maendeleo ya kilimo nchini.
Kwa upande wao wakufunzi wa mafunzo hayo kutoka NABAD,
walisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma watoaji wa
mikopo kwa upande wa kilimo kufahamu kwa undani vigezo vya kuzingatia wakati wa
utoaji wa mikopo hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya
Kilimo ya Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (kulia) akihimiza jambo kwa
washiriki wa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo. Mafunzo
hayo ya siku sita yanafanyika katika Hoteli ya Beach Comber, Dar es Salaam.
Meneja Msaidizi wa Mafunzo kutoka NABAD, Dkt. R.S.
Reddy akizungumza kuhusu mafunzo hayo. Mafunzo hayo ya siku sita yanaendeshwa
kwa pamoja kati ya TADB, NABAD na MIVARF.
Meneja Msaidizi wa Mafunzo kutoka NABAD, Bw. M.R.
Gopal akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za
Ukopeshaji katika Kilimo. Mafunzo hayo ya siku sita yanaendeshwa kwa pamoja
kati ya TADB, NABAD na MIVARF.
Washiriki wa Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji
katika Kilimo wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa mafunzo hayo. Mafunzo hayo
yanafanyika katika Hoteli ya Beach Comber, jijini Dar es Salaam.
SHARE
No comments:
Post a Comment