Julian Msacky
SERIKALI ya Awamu ya Tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa
nchi ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati.
Ndiyo maana viongozi wa serikali na sekta binafsi wanahimiza watu
wajikite katika sekta hiyo ili kuikwamua nchi kiuchumi.
Tunavyofahamu ni kwamba ili kufikia huko lazima sekta ya
kilimo iwezeshwe kwa kila mbinu ili iweze kufanya kazi kwa tija.
Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TABD), Francis Assenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam hivi karibuni. Kushoto ni Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa benki hiyo, Albert Ngusaru.
Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TABD), Francis Assenga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam hivi karibuni. Kushoto ni Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa benki hiyo, Albert Ngusaru.
Kusema kweli bila kuwekeza katika sekta ya kilimo chini ya
kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ni vigumu kuwa nchi ya kiviwanda.
Hii ni kwa sababu kuna uhusiano wa karibu kati ya viwanda na
kilimo ili Taifa liweze kuwa na uchumi imara kwa nchi na watu wake.
Ni katika kuwekeza maeneo hayo tutaweza kupunguza umaskini
nchini na kupanua wigo wa ajira kwa Watanzania wengi.
Kwa hiyo viongozi wetu wanapohubiri suala la viwanda ni
lazima wahakikishe pia kwamba sekta ya kilimo imewezeshwa vilivyo.
Ili wakulima walime kwa tija wanahitaji kuwezeshwa na
kupatiwa nyenzo zinazotakiwa ili kutuondoa hapa tulipokwama.
Ni lazima tukiri pia kwamba enzi za uongozi wa Mwalimu Julius
Nyerere kilimo kilithaminika mno kwa sababu uongozi ulikithamini.
Watu wengi walibaki vijijini wakifanya shughuli za kilimo na
hakika wimbi la vijana kukimbilia mijini lilikuwa dogo mno.
Lakini siku hizi vijana wamefurika mijini kwa sababu vijiji
si sehemu rafiki kwao. Wanaona usalama
wa maisha yao upo mijini.
Swali ni je, serikali imejipanga inavyotakiwa kuhakikisha
kilimo chetu kinaboreshwa kama enzi za Mwalimu Nyerere?
Je, wataalamu wa kilimo wapo vijijini wakielekeza wakulima
nini walime na katika ardhi gani ili tuzalishe kwa ufanisi?
Tumejipangaje kuwapatia wakulima mikopo rahisi na ruzuku ili
wafufue mazao waliotelekeza kwa vile hakiwalipi?
Hebu tuone. Hivi karibuni Wizara ya Fedha na Mipango
iliipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) sh. bilioni 209.5.
Tumeambiwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiongezea mtaji ili
kukidhi malengo ya kutoa mikopo kwa wakulima wa kati na wadogo.
Ndivyo alivyotuambia Naibu Katibu Mkuu wa Waziri hiyo, Dk
Khatibu Kazungu akisema wameongeza mtaji TADB ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa
Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/2021 ili kuboresha sekta ya
kilimo.
Kaimu Mkurugenzi wa benki hiyo, Francis Assenga anasema fedha
hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na hadi sasa wamefikia wakulima 3700
tangu ilipoanzishwa.
Nikiri tu hapa kuwa kuanzishwa kwa benki hii ni jambo jema.
Ni hatua muhimu ya kuhakikisha tunawezesha wakulima kimtaji.
Katika hili niseme mambo kadhaa ambayo pengine yakizingatiwa
itasaidia nchi kufanya vitu vya kwa mpangilio na tija zaidi.
Mosi, benki ikitumiwa vizuri na kutoa elimu kwa walengwa
tutaona mabadiliko ya haraka katika sekta yetu ya kilimo.
Hii ikiwa na maana kuwa wakulima waoneshwe fursa hiyo hasa
vijijini. Benki hii isitumie muda wake mwingi maeneo ya mijini.
Maofisa wake waendee vijijini, waelimishe wakulima taratibu
za kukopo na waelimishwe aina ya mazao yenye tija kwao.
Benki hii inatakiwa iwe mwarobaini wa kuinua kilimo nchini
hasa mazao ya biashara kwani kwa sehemu kubwa ni kama vile yamekufa.
Ni wapi leo hii utaona wakulima wakichangamkia kilimo cha
kahawa, pamba, chai, katani au korosho kama ilivyo zamani?
Ingefurahisha kama benki hiyo ingetumika zaidi kuwekeza
kwenya mazao hayo na kuhakikisha tunazalisha kwa ufanisi.
Kilichoua mazao hayo ni gharama kubwa za uendeshaji na
wakulima kunyonywa bei wakati wanapouza na kuona haina maana tena kulima.
Sasa benki hiyo iamshe upya ari ya wakulima kulima mazao
hayo. Tukifanya hivyo kwa hakika Watanzania wengi watakimbilia huko.
Wataacha tabia ya kuzunguka mjini na viatu viwili wakitafuta
wateja kwa sababu wimbi la wamachinga “tumelitaka sisi wenyewe”.
Kwa maana hiyo wa kuliondoa ni sisi wenyewe. Njia nzuri ni
mosi, kuwekeza vizuri kwenye sekta ya kilimo ili kithaminiwe.
Hivyo Benki ya Kilimo ina nafasi kubwa kututoa hapa
tulipokwama kwa miongo kadhaa sasa hususan kwenye sekta ya kilimo.
Tunaamini maofisa wa benki hiyo watajipanga vizuri na
kuhakikisha inaleta mabadiliko chanya kwa wakulima wetu.
Sekta hiyo imezirai kwa muda mrefu na wakulima wamekata tamaa
kwa muda mrefu, hivyo benki hiyo iwaondoe Watanzania hapo.
Kama kweli tunaamini kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu
tuoneshe hivyo kwa vitendo maana ardhi ipo pamoja na rasilimali watu.
Tunasubiri kuona maajabu ya benki ya kilimo kwa wakulima
wetu, lakini nisisitize kuwa tukishindwa tena wakati huu hatutaweza tena.
Hii ni kwa sababu wakulima wetu wameteseka kwa muda mrefu
hivyo wanahitaji faraja na faraja yenyewe ni kuwezeshwa.
Waendeshe kilimo cha kisasa, kilimo cha umwagiliaji kama
wanavyofanya wenzetu wa Misri badala ya kutegemea mvua tangu Uhuru.
Wiki
ijayo tutaangalia namna ya kutumia rasilimali zetu kutokana na mahitaji ya
nchi.
0718981221
SHARE








No comments:
Post a Comment