Na Hamza Temba
SERIKALI imesema imebaini mchezo mchafu unaofanywa na
wafanyabiashara haramu wakiwemo majangili wa kutumia mbinu za kutakatisha fedha
haramu kwa kununua makundi makubwa ya mifugo, kuyachunga kwenye maeneo ya
hifadhi nchini na baadaye kuyauza kwa faida kubwa kwenye minada.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Prof. Maghembe alimueleza balozi huyo kuwa Serikali tayari imebaini ujanja huo na sasa inajipanga namna ya kushughulika na wahalifu hao ili kukomesha kabisa matendo hayo ambayo yameifikisha nchi kwenye migogoro mikubwa ya ardhi huku yakiharibu maeneo ya hifadhi pamoja na vyanzo vya maji.
“Sasa hivi tumegundua janja ya genge la watakatisha fedha haramu ambapo wananunua mifugo kwa wingi kisha wanawapa watu wawachungie kwenye maeneo yetu ya hifadhi baada ya miezi kama sita hivi wanakuja kuichukua na kuiuza kwenye minada kwa faida kubwa, tutashuulika nao ipasavyo”, alisema Maghembe.
Aliongeza kuwa “Wanapoingiza mifugo hiyo ndani ya hifadhi, huingia na majangili pamoja na wachoma mkaa, tumebaini pia kuwa karibu nusu ya mkaa unaovunwa Tanzania huuzwa nje ya nchi hususan nchi jirani, hatutakubali vitendo hivyo viendelee, ni lazima misitu yetu iliyobakia ilindwe na kuhakikisha kuwa inaendelea kuwepo”.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke majarida mbalimbali yanayoelezea vivutio vya Tanzania ofisini kwake mjini Dodoma mwishoni mwa wiki. Alimueleza kuwa Serikali imebaini na itakomesha ujanja unaofanywa na wafanyabiashara haramu wa kutakatisha fedha kwa kununua makundi makubwa ya mifugo na kuyachunga kwenye maeneo ya hifadhi nchini na baadaye kuyauza kwa faida kwenye minada. (Picha na Hamza Temba - WMU)
Akizungumzia athari za kimazingira zitokanazo na uharibifu wa misitu, Prof. Maghembe alisema kwa sasa maeneo mengi nchini yaliyokuwa yakipata mvua kwa miezi mitano mfululizo sasa yamekuwa yakipata mvua chini ya kiwango na kufikia miezi mitatu hadi miwili hali inayotishia nchi kuwa jangwa.
Kwa upande wake balozi Cooke, alimuhakikishia Waziri Maghembe kuwa atakua balozi mzuri wa vivutio vya Tanzania nchini Uingereza pamoja na kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya uhifadhi. Aliahidi pia kushawishi wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya uhifadhi na utalii.
SHARE








No comments:
Post a Comment