Watu 12
wamethibitishwa kufariki na wengine 18 wamo katika hali mahututi
hospitalini baada ya moto kuteketeza jumba la ghorofa 24 la makazi
magharibi mwa London.
Jengo hilo bado linawaka moto na watu wengi hawajulikani walipo.
Kulitokea nini?
Taarifa za kwanza za kuzuka kwa moto jumba hilo la Grenfell Tower, kaskazini mwa Kensington ziliripotiwa saa, 00:54 BST (saa tisa kasoro dakika tisa Afrika Mashariki).
Inaaminika moto huo ulianza ghorofa ya nne na kuenea kwa kasi.
Malori 40 ya kuzima moto yalitumiwa kukabiliana na moto huo. Kulikuwa na wazima moto 200.
Ni watu wangapi walioathiriwa?
Watu 12 wamefariki kwa mujibu wa polisi, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.
Kuna watu 78 ambao wamepokea matibabu hospitalini. Hospitali sita - St Mary's, Chelsea and Westminster, Royal Free, St Thomas', Charing Cross Hospital na King's College Hospital - zilipokea majeruhi.
Kamishna wa wazima moto wa London Dany Cotton anasema wazima moto kadha walipata majeraha madogo.
Walioshuhudia wanasema huenda kuna watu waliokwama kwenye jengo hilo, lililokuwa na nyumba 120 za makazi.
Diwani wa Notting Dale Judith Blakeman, anayeishi hapo karibu, anasema kumekuwa na watu kati ya 400 na 600 ambao wamekuwa wakiishi katika jumba hilo.
Meya wa London Sadiq Khan amesema wazimamoto walifanikiwa kufikia ghroofa ya 12 pekee.
Polisi wa jiji wametoa nambari ya dharura kwa watu wanaotafuta habari kuhusu jamaa na marafiki - 0800 0961 233.
Nini kilisababisha moto?
Chanzo cha moto huo hakijabainika.
Matt Wrack, katibu mkuu wa Chama cha Wazimamoto, amesema "uchunguzi kamili utafanywa haraka iwezekanavyo".
Jumba hilo linapatikana wapi?
Grenfell Tower linapatikana barabara ya Latimer, magharibi mwa London.
Ni sehemu ya mtaa wa makazi wa Lancaster West Estate, ulio na jumla ya nyumba 1,000, katika eneo la Kensington na Chelsea.
Jumba hilo linapatikana karibu na kituo cha kibiashara cha Westfield, eneo la White City na barabara ya A40 - inayotumiwa sana na watu kuingia na kutoka magharibi mwa London.
Tunafahamu nini kuhusu Grenfell Tower?
Grenfell Tower ilijengwa mwaka 1974 na baraza la mtaa wa Kensington na Chelsea.
Jumba hilo lilifanyiwa ukarabati uliogharimu £10m, ambao ulifanywa na kampuni ya Rydon Construction.
Ukarabati huo ulimalizika mwaka uliopita.
Kulifanyiwa mabadiliko makubwa orofa nne za kwanza, ambapo nyumba tisa ziliongezwa na vituo vya huduma za kutumiwa na jamii kwa pamoja vinaongezwa.
Jumba hilo pia lilipambwa nje, madirisha mapya yakawekwa na mfumo wa kupasha joto vyumba ukawekwa.
Ramani ya jengo hilo inaonyesha jinsi ukarabati ulivyofanyia mabadiliko jumba hilo, na ngazi moja.
CHANZO: BBC
SHARE
No comments:
Post a Comment