Na Jonas Kamaleki-MAELEZO
Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi imepima viwanja 4333 hadi mwishoni mwa Mei, 2017 na
hatua za umilikishaji zimeanza katika utekeleza wa kurasimisha maeneo
yaliyojengwa kiholela jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo (jana) na
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Mipango Miji na Vijiji wa Wizara ya
Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bertha Mlonda katika maohojiano
maalum na mwandishi wahabari hii.
Kwa mujibu wa Mlonda, jumla ya
viwanja 6,000 vinatarajiwa kupimwa na kumilikishwa katika jiji la Dare
es Salaam katika zoezi zima la urasimishaji wa makazi holela.
“Pamoja na urasimishaji katika
Jiji la Dar es Salaam halmashauri nyingine 6 zimepangwa kutekeleza
mradi huo. Halmashauri hizo ni; Manispaa za Musoma, Kigoma-Ujiji,
Tabora, Singida, Sumbawanga na Lindi”, amesema Mlonda.
Aidha, Mlonda amesema kuwa
mradi unatekelezwa katika Kata za Kimara na Saranga Manispaa ya Ubungo
ambazo zina ukubwa wa hekta 3,960.8. Kata ya Kimara, inajumuisha mitaa
sita (6) ambayo ni Kilungule “A”, Kilungule “B”, Mavurunza, Baruti,
Kimara Baruti na Golani. Kata ya Saranga ina jumla ya mitaa saba (7) ambayo ni Kimara B, King’ong’o, Matangini, Michungwani, Saranga, Spotover na Upendo.
Ameongeza kuwa kwa pamoja kata
hizo zina wastani wa viwanja 34,000. Mradi umeanzia kutekelezwa katika
Kata ya Kimara kwenye Mitaa ya Kilungule ‘A’, Kilungule ‘B’ na sasa
Mavurunza. Lengo la Mradi ni kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha
viwanja 6,000.
Mkurugenzi Msaidizi huyo amesema
kuwa baada ya kukamilisha michoro ya Mipangomiji na Ramani za Upimaji na
kupata upana wa barabara, kazi iliyofuata ni kufungua barabara.
Barabara hizo zilifunguliwa kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo.
Uchongaji wa barabara umefuata vipimo vilivyoainishwa katika Michoro ya
Mipangomiji na Ramani za Upimaji.
Barabara zenye urefu wa kilomita 9.128 zimechongwa katika Mitaa ya Kilugule ‘A’, Kilungule ‘B’ na Mavurunza, amesema Mlonda.
Katika urasimishaji huo,
Mlonda aliainisha mafanikio ya mradi kama ifuatavyo: Kuwa na Michoro ya
Mipangomiji na Ramani za Upimaji katika eneo la Kimara, kuboresha
mazingira katika makazi, kuongeza huduma za jamii na miundombinu katika
maeneo ambayo awali yalikuwa hayafiki kwa gari sasa yanafikika na
kuongeza usalama wa miliki ya ardhi kwa wananchi na kuongeza fursa ya
kutumia ardhi kama mtaji na kupunguza umasikini.
Ameyataja mafanikio mengine
kuwa kanzi data inajenga uwezo wa halmashauri kusimamia na kutoa huduma
za ardhi kwa ufanisi, kuwa na maeneo yaliyopangwa, kupimwa na
kumilikishwa,kupunguza au kuondoa kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi na
kuongeza wigo wa mapato ya serikali kwa kupitia tozo mbalimbali za ya
kodi ya ardhi.
Urasimishaji huu unatekelezwa
kwa mkopo wa Benki ya Dunia ambapo viwanja 3000 vinatarajiwa kupimwa
katika kila Halmashauri. Utekelezaji utatumia uzoefu uliopatikana wakati
wa utekelezaji wa mradi katika Jiji la Dar es Salaam na Mwanza. Zoezi
hili linalenga kuboresha hali ya mazingira katika maeneo yasiyopangwa na
kuzuia ukuaji holela wa miji.
SHARE
No comments:
Post a Comment