Nchini Rwanda, wagombea wa nafasi ya urais leo hii
wanaanza kampeni rasmi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa taifa hilo
unaotarajiwa kufanyika Agosti 4.
Katika barabara za viunga vya mji wa Kigali, mji mkuu wa Rwanda,
ambako kunaonekana majengo mapya kwenye miinuko ya mji huo, watu
wachache mpaka wakati huu wanaelezwa kuweza kusikia habari za wagombea
wa nafasi ya urais kwa upande wa upinzani Frank Habineza na Philippe
Mpayimana.Ndio pekee waliothibitishwa kuwa wagombea na kuruhusiwa kuanza kuchangisha fedha wiki moja kabla ya leo hii siku ya kuanza kwa kampeni, yakiwa maandalizi ya mchakato wa uchaguzi wa tarehe nne mwezi wa nane, katika taifa hilo lililo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kiasi kidogo cha fedha walichonacho na kuwa na wiki tatu za kutafuta uungwaji mkono, wagombea hao wawili wanakabiliwa na kazi ngumu ya kumkabili rais mwenye nguvu zote Paul Kagame, ambae pia anatarajiwa kushinda kwa urahisi kabisa katika awamu hii ya muhula wa tatu madarakani.
Sauti ya raia wa Rwanda
Bwana mmoja anaefanya shughuli za ubebaji mizigo mitaani, One Love Nkundimana mwenye umri wa miaka 28, anasema wao kama umma wa raia wemekuwa wakiishi kwa muda mrefu na rais wao Paul Kagame. Ndio pekee wanaotambua kile alichowafanyia, kwa hivyo hawajali kuhusu wagombea wengine wowote.
Rais Kagame na chama chake tawala "Rwandan Patriotic Front" wamekuwa wakiongoza Rwanda kwa mkono wa chuma tangu walipoipindua serikali ya utawala wenye msimamo mkali wa Kihutu, jambo uliosababisha mauwaji ya Kimbari ya mwaka 1994 ambapo watu laki nane waliuwawa wengi wao ni kutoka katika kabila la Watutsi.
Wakati akisifiwa kwa kuleta utawala wa sheria, ujenzi wa miundombinu na utulivu katika taifa hilo lililokuwa limevurugwa na vita, makundi ya haki za binaadamu yanasema Kagame anaongoza kwa mfumo wa hofu wa ukandamizaji dhidi ya upinzani, uhuru wa kutoa maoni, na vyombo vya habari. Mgombea wa chama kinachopigania demokrasia cha kijani, Frank Habineza amenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa AFP akisema "Tunajua watu wamechoshwa na kuongozwa na serikali moja kwa miaka 23 lakini hawawezi kusema, kwa kuwa kuna mazingira ya hofu."
Anasema mikutano ya kisiasa nchini humo imekuwa ikivunjwa,wanaowaunga mkono kufungwa au kulazimishwa kukimbilia uhamishoni, na hata kuondoka kwake, kwenda Sweden kulitokana na naibu wake kuuwawa kinyama muda mfupi kabla ya uchaguzi uliopita wa 2010. Lakini aliweza kufanikiwa kusajili chama chake 2013, baada ya kurejea nchini humo akitokea Sweden.
Mgombea mwingine wa upinzani Mpayimana mwenye umri wa miaka 47, ambae pia ni pekee kati ya wagombea wanne binafsi walioruhusiwa na tume ya uchaguzi kushiriki kuwania kiti hicho anasema ana wasiwasi kwa kuwa hawakupewa hata muda wa kutosha katika kuchapisha na hata kupandika mabango ya kampeni. Mgombea huyo mwandishi habari wa zamani aliyeishi uhamishoni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ufaransa kwa miaka 18 alirejea nchini humo Februari kwa ajili ya kuwania nafasi ya Urais.
Rais Paul Kagame alishinda uchaguzi wa 2003 na 2010 kwa zaidi asilimia 90 ya kura.
SHARE
No comments:
Post a Comment