
Naibu Spika Dk. Tulia Akson akiangalia taarifa mbalimbali za kabila la wagogo
……………………………………………………………………………
NA MAKUBURI ALLY
JULAI 21-23 Wilayani Chamwino
mkoani Dodoma maeneo karibu na Ikulu kunatarajia kuwa na burudani ya
aina yake kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo yanayokizunguka, ambapo
linatarajia kufanyika Tamasha la 9 la muziki wa asili ya Cigogo
‘Chamwino Music Festival’.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa
Tamasha hilo, Dk. Kedmon Mapana mipangilio ya maandalizi kuelekea
tamasha hilo yamekamilika kwa kiasi kikubwa yakiwemo makundi na kamati
nzima ya maandalizi imekamilisha asilimia kubwa ya matakwa ya tamasha
hilo.
Dk. Mapana anasema mipangilio
imekamilika katika maeneo kama ukusanyaji wa fedha zitakazofanikisha
tamasha hilo, maandalizi kwa washiriki na wageni waalikwa katika tamasha
hilo.
Dk. Mapana anasema kwa upande wa
bajeti ya tamasha hilo ambayo ilikuwa ni shilingi milioni 32 lakini
zimepatikana milioni 18 kwa sababu kwamba wafadhili wakubwa ni watu
binafsi wanaoamini urithi wetu ni muhimu sisi kama binaadam sababu utu
wetu umejengeka katika mila na desturi.
“Ukitaka kupata utambuzi kwa
wanachofikiria Wagogo jinsi wanavyokula, mahusiano yao ya kijamii na kwa
ujumla kwa yote yanabebwa katika nyimbo na ngoma zao, hivyo tumeonelea
tuyaweke wazi, ndipo tukaasisi tamasha hilo,” alisema Dk. Mapana.
Anasema kwamba ufadhili wa
tamasha hilo wameupata kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Chamwino
Connect lenye makazi yake nchini Marekani huku wafadhili wengine ni
serikali ya kijiji cha Chamwino ambacho kinatoa maeneo ya kufanyia
tamasha hilo huku wafadhili wengine ni wasanii wenyewe ambao hujitolea
kwa kiasi kikubwa ili kukuza utamaduni wao.
Dk. Mapana anasema maandalizi
mengine ni kwa wasanii ambao wanashiriki tamasha hilo, yamekamilika kwa
kiasi kikubwa kwani awali makundi yaliyopatikana yalikuwa 70 na
wamefanikiwa kubaki na makundi 50 yaliyothibitisha kushiriki.
Anasema katika makundi hayo
wanawafuatilia mienendo yao katika sanaa kwani wanataka kile cha asili
katika muziki na sanaa husika na mambo mapya ambayo wanaweza kuyaonesha
katika tamasha hilo.
Anasema kauli mbiu ya tamasha la
mwaka huu ambayo imekuja katika muda muafaka kwa sababu serikali ya
awamu ya tano imejipanga kupambana na Rushwa ambayo ni Piga rushwa
kupitia Sanaa kwani ujumbe huo utafika kwa watu zaidi ya 10,000 kupitia
tamasha hilo, ingawa wahusika wanatakiwa kuwa na dhamira ya utekelezaji .
Aidha Dk. Mapana anaweka bayana
makundi shiriki ya tamasha hilo yanatoka katika Wilaya za Kongwa, Dodoma
mjini na Chamwino na makundi mengine yanatoka nje ya mkoa huo.
Makundi hayo ni pamoja na Mbeta
(Morogoro), Happy African Art (Iringa), Kipauli (Njombe), Samba Group na
Tulia Traditional Dance Festival (Tukuyu- Mbeya), Mandoo na Shada
(Bagamoyo) na Muungano (Singida).
“Kwanini tumeshirikisha na
makundi mengine katika tamasha letu ni kujifunza pia tamaduni za mikoa
mingine ili kuimarisha mila na desturi,” alisema Dk. Mapana.
Dk. Mapana anakumbusha kwamba
matamasha yaliyopita walishirikisha makundi kutoka maeneo mbali ya
Tanzania ambako tamasha la mwaka juzi lilishiriki kundi la Taarab kutoka
Zanzibar ambalo baada ya tamasha walitengeneza wimbo wenye vionjo
mchanganyiko wa bara na Zanzibar.
Anasema katika maandalizi ya
tamasha hilo kamati 70 ya maandalizi ya Chamwino Arts Centre
imefanikisha kutunga wimbo wa halaiki ambao unahamasisha Umoja na amani
kwa Tanzania ambao utaimbwa katika tamasha hilo.
Anasema kwa upande wa Malazi
wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukodi nyumba zaidi ya 50 zilizowazi
kijijini hapo na kuwataka wasanii kuwasili kijijini wakiwa hawana shaka
na malazi.
Anaweka bayana wageni
wanaotarajia kuwepo kwenye tamasha hilo ni pamoja na wageni wanne kutoka
Nzega Arts Centre ya Tabora ambao wanafika katika tamasha hilo kwa
ajili ya kujifunza zaidi maandalizi ya tamasha lao la Sukuma- Nyamwezi.
Wageni wengine ni wanafunzi 12 wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaokwenda kujifunza kuandaa matamasha ya
muziki wa asili, wageni 12 kutoka vyuo vikuu nchini Marekani; 11 kutoka
Chuo Kikuu cha Seattle Pacific na mmoja kutoka New Wark.
Mgeni mwingine ni kutoka Uganda
kwenye taasisi isiyo ya kiserikali ya Soul Expression ambayo pia
inahitaji kuunganisha nguvu ya pamoja na Kituo cha Sanaa cha Chamwino.
Huku mgeni mwingine mshiriki
anatoka Visiwa vya Mayotte, Anima Abdallah ambaye aliwahi kuimba pamoja
na wanamuziki nguli barani Afrika, Pepe Kalle, Papa Wemba na Koffi
Olomide ambaye pia anajipanga kwa dhamira ya kuunganisha tamaduni za
Mayotte na kituo cha sanaa cha Chamwino.
Dk. Mapana ambaye ni Mkuu wa
Sanaa wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam, anamuweka bayana mgeni rasmi
katika tamasha hilo ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo,
Dk. Harrison Mwakyembe.
Anaeleza faida za matamasha ya
muziki wa asili na kueleza kwamba yanasaidia wasanii na jamii kuendelea
kuutunza utamaduni wao ambako pia wanataka Tanzania kuwa na utamaduni
unaoishi.
“Tunayajali makundi ya sanaa
tunayofanya nayo kazi kwani matamasha yaliyopita tulikuwa tunayafuatilia
kwa karibu makundi hayo kwa zaidi ya miezi mitano ili kuendeleza
mikakati ya kudumisha na kuendeleza utamaduni wetu,” alisema Dk. Mapana.
Faida nyingine inayopatikana
wameshapeleka makundi tisa katika matamasha ya nje ya Tanzania kwa lengo
la kupanua wigo wa ufikishaji wa sanaa yetu nje ya nchi.
Makundi matano yalishawahi
kushiriki matamasha nchini Poland ambayo ni Nyerere Muheme Group,
Yerusalem, Ndagwa na Yeriko (Yote ya Chamwino) na Milungu Group (Kijiji
cha Kawawa) huku kundi moja la Ufunuo Majereko limeshawahi kushiriki
tamasha nchini Ujerumani, Ndagwa liliwahi pia kushiriki tamasha nchini
Ufaransa.
“Katika hayo makundi, washiriki
wote elimu yao ni ya darasa la saba ambao hivi sasa mawazo na akili zao
na upeo pia vimebadilika kupitia ziara za nje ya nchi ambako wanajifunza
mambo mbalimbali,” alisema Dk. Mapana.
Faida nyingine wanayoipata ni
kwamba wamejenga umoja mkubwa kwa wakazi wa Dodoma na maeneo mengine na
pia wameongeza upendo na amani ambako pia anaeleza kwamba wao hawafanyi
mashindano.
Anaeleza faida nyingine ni
kufanikisha elimu ya kutosha kwa kila aliyehudhuria kupata maono mapya
kupitia sanaa zinazofanyika kijijini Chamwino huku faida nyingine ni
kuendeleza kurithisha elimu ya muziki wa asili, utamaduni, mila na
desturi kwa sababu linashirikisha watoto, vijana na watu wazima.
Dk. Mapana anaweka bayana faida
nyingine ya tamasha hilo ni kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake
kwani idadi kubwa ya watalii wanaongezeka kujionea sanaa ya Tanzania
ikiwa ni nchi ya Amani na utulivu ndio maana wanakuja kujonea tamaduni
zetu ambazo zinaonesha mwelekeo mzuri wa maendeleo.
Dk. Mapana anamalizia kuweka
bayana faida nyingine ambayo inachangia ukuaji wa uchumi wa kijiji cha
Chamwino kwa sababu katika tamasha hilo wenyeji wanauza chakula,
vinywaji na wapishi pia wanapata fedha sambamba na biashara ndogondogo.
“Milioni 18 zilizopatikana
kupitia tamasha hilo zinazama pale kijijini hivyo ni sehemu yetu ya
uchagiaji wa maendeleo,” alisema Dk. Mapana
SHARE








No comments:
Post a Comment