Paschal Dotto, MAELEZO
Tume ya Vyuo vikuu (TCU)
imevifutia udahili vyuo 19 na kufuta kozi 75 katika vyuo 22 kwa kukiuka
Sheria taratibu na kanuni za utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hii Jijini Dar es Salaam Jana Afisa habari wa Tume hiyo Bw. Edward
Mkaku amesema uamuzi wa kuvifutia udahili baadhi ya vyuo ni kutekeleza
agizo la serikali lililoitaka Tume hiyo kuvisimamia kwa karibu vyuo ili
viweze kutoa elimu bora.
Makaku amesema kuwa kwa vyuo
ambavyo wanafunzi wanaendelea na masomo mabadiliko haya hayatawahusu
wanatakiwa kuendelea na masomo kama kawaida, ila vyuo hivyo
haiviruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa mwaka huu wa masomo.
Alizitaja baadhi ya sababu
zilizopelekea baadhi ya vyuo kufutiwa udahili wa Shahada, Shahada za
Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu kuwa ni kukosa vitendeakazi na
wataalam katika kufundisha elimu ya juu.
Aidha Mkaku amesema kuwa TCU
imeandaa maonesho yatakayoanza Julai 26, 2017 katika viwanja vya Mnazi
Mmoja Jijini Dar es Salaam,maalum kwaajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi
wanaohitaji kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini, pia kuelezea
shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume hiyo.
Bw.Mkaku pia amesema baadhi ya
vyuo vinavyotoa taaluma za afya kama Kilimanjaro Chritiani medical
College (KCMC) cha mkoani Kilimanjaro, Kampala International University
(KIU) cha Jijini Dar es Salaam pamoja na Hubert Kairuki Memorial
University (HKMU) pia cha Jijini Dar es Salaam ambavyo vilikuwa vikitoa
kozi za udaktari, ufamasia pamoja na shahada ya uzamili katika Udaktari
wa magonjwa ya kinamama iliyokuwa ikitolewa na Chuo cha Hubert Kairuki
imebainika kuwa hawakuwa na vifaa na wataalam wa kutosha kufundisha
kozi hizo.
Alivitaja vyuo vilivyofungiwa
kutokana na kutokuwa na wataalam wa kutosha kuendesha kozi zake kuwa ni,
St. Joseph, St. John, Tumaini University pamoja na vyuo vingine kadhaa
ambavyo havina walimu pamoja na vifaa kwa mujibu wa maelekezo ya Tume
hiyo.
Mkaku amebainisha kuwa katika
vyuo 22 hapa nchni kuna zaidi ya kozi 75 ambazo hazitakiwi kudahili
wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2017/2018 na kuwashauri watahiniwa
wanaotarajia kujiunga na mwaka huu wa masomo kuingia katika tovuti rasmi
za vyuo ili kujua kozi ambazo zinatakiwa na kozi ambazo zimezuiliwa.
“Tulifanya uhakiki wa vyuo hapa
nchni Septemba na Oktoba 2016 na kubaini baadhi ya vyuo kutokukidhi
mahitaji ya watahiniwa katika baadhi ya kozi kwa hiyo ni muhimu kutoa
taarifa mapema kwa umma juu ya mchakato huu” Alisema.
Katika kuondoa changamoto kwa
watahiniwa wa miaka ijayo, Mkaku amesema kuwa maonesho ya vyuo yatakuwa
yanafanyika kikanda ili kutoa elimu kwa umma katika masuala mazima ya
elimu ya juu.
TCU ilikabidhi rasmi jukumu la udahili kwa vyuo husika
Julai 20,2017 ili waendeshe wenyewe na wao watabaki kuwa wasimamizi wa
Sheria na sera za vyuo vya elimu ya juu.
TCU wametoa onyo kwa vyuo
vitakavyoendelea kudahili wanafunzi katika kozi zilizofutwa kuwa ni
kinyume cha Sheria na wakibainika watashitakiwa kwa mujibu wa Sheria za
nchi na zile za vyuo vikuu.
SHARE
No comments:
Post a Comment