Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limewatoa hofu watumishi wa
Serikali waliokutwa na vyeti feki na kuwataka kupuuza taarifa kuwa
hawatolipwa malimbikizo ya madai yao.
Limewahakikishia
watumishi hao, wanaoidai Serikali malimbikizo mbalimbali kuwa mchakato
wa ulipaji wa malimbikizo yao ya mishahara na madai mengine utaanza hivi
karibuni.
Kauli
hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano
waliyoafikiana na Serikali.
“Kumekuwapo
na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa watumishi
waliokutwa na vyeti feki hawatolipwa madai yao, jambo hilo si kweli,
nawahakikishia watumishi hawa TUCTA tumekutana na waziri mwenye dhamana
na katibu mkuu wake ambao nao wamesema taarifa hizi hazina ukweli.
“Tumeambiwa uhakiki utakapokamilika, ndipo watatangaza uamuzi wa madai yao,” alisema.
Kuhusu
malimbikizo ya mishahara na madai mengine ya watumishi wa Serikali,
wakiwamo walimu, Nyamhokya alisema wamehakikishiwa wataanza kulipwa hivi
karibuni.
“Ingawa
hatukupewa muda kamili yataanza kulipwa lini, niwatoe hofu watumishi
kuwa madai yao yote yataanza kulipwa hivi karibuni… kauli ambayo imetoka
kwa waziri mwenyewe, baada ya kukutana naye ana kwa ana ofisini kwake
hivi karibuni,” alisema.
Licha
ya kupongeza juhudi za Rais Dk. John Magufuli katika kuisafisha
Serikali, Nyamhokya aliiomba Serikali kutekeleza ahadi za rais
alizozitoa wakati akihutubia sherehe za Mei Mosi, mwaka huu.
“Aliahidi
kurejesha madaraja kwa wafanyakazi katika mwaka huu wa fedha, kuongeza
mishahara pamoja na kulipa madeni ya watumishi wote,” alisema.
Hadi kufikia Novemba, mwaka jana, Serikali imelipa Sh bilioni 29 kwa watumishi mbalimbali wa umma wakiwamo walimu.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa hotuba aliyotolewa bungeni Aprili 18, mwaka huu na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora), Angellah Kairuki, ni madai 18,823 ya malimbikizo ya
watumishi yenye thamani ya Sh bilioni 32.8 ambayo yamehakikiwa na
kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mshahara kwa malipo.
SHARE
No comments:
Post a Comment