Serikali ya Marekani imeziamrisha familia za
wanadiplomasia wa ubalozi wake wa Venezuela kurudi nyumbani na kutoa
idhidi ya kuwaruhusu wafanyakazi wa ubalozi huo kuondoka kwa hiari, huku
machafuko yakizidi kuwa mabaya.
Serikali ya Marekani hapo jana imeziamrisha familia za wafanyakazi wa
ubalozi wake wa Venezuela kuondoka nchini humo, na wafanyakazi wa
serikali kuondoka kwa hiari wakati wowote wanaoutaka, huku mgogoro wa
kisiasa ukizidi kuwa mbaya, ikiwa ni siku chache kabla ya kufanyika
uchaguzi wenye utata ambao wakosoaji wanasema utakuwa ndiyo mwanzo wa
kutoweka kwa demokrasia katika taifa lenye utajiri wa mafuta.Vifo vitano vimeripotiwa kufuatia vurugu za maandamano ya Alhamis, na kuifanya idadi jumla ya vifo katika miezi minne ya machafuko kufikia watu zaidi ya 100.
Wengi waliopoteza maisha katika maandamno hayo ya kuipinga serikali yaliyoanza mwezi Aprili ni vijana waliouwawa kwa kupigwa risasi. Idadi hiyo pia inajumuisha waporaji, polisi wanaodaiwa kushambuliwa na waandamanaji na raia wa kawaida waliouwawa katika ajali zilizotokana na vizuwizi vilivyowekwa barabarani wakati wa maandamano hayo.
Mazungumzo ya amani na upinzani
Hapo jana akiwa anahutubia umati wa wafuasi wake, Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amewataka raia wake kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Jumapili ijayo uliogubikwa na utata, wa kuteua wajumbe wa baraza ambalo litapewa kibarua cha kuiandika tena katiba ya Venezuela.
Maduro pia alirudia tena pendekezo lake kwa upinzani la kukaa kitako pamoja kwa mazungumzo akidai kwamba ndio njia pekee ya kutatua mgogoro wa kisiasa uliolikumba taifa hilo.
"Ninapendekeza kwa upinzani wa Venezuela kuwa waachane na njia yao ya uasi, katika masaa machache yajayo, kabla ya uchaguzi wa kuteua Baraza la Taifa la Kuandika Katiba, tuanzishe mazungumzo, makubaliano ya kitaifa na maridhiano ya nchi yetu," amesema Maduro.
Upinzani umeitisha maandamanoo ya umma Ijumaa katika mji mkuu wa Caracas, jambo litakaloweza kuongeza kasi ya mvutano. Serikali kwa upande wake imepiga marufuku kufanyika maandamano yoyote kuanzia Ijumaa hadi Jumanne, baada ya kumalizika uchaguzi, hatua inayoweza kuongeza machafuko nchini humo.
Upinzani pia unawataka raia wa Venezuela kususia kura hiyo ya Jumapili, wakisema kwamba sheria za uchaguzi zina udanganyifu na zitahakikisha kuwa Maduro atapata wingi wa kura na kwamba katiba mpya itachukuwa nafasi ya demokrasia kupitia mfumo wa uongozi wa chama kimoja.
Vifo vilivyongezeka vya waandamanaji sasa vimekuwa chanzo kingine cha hasira miongoni mwa vijana wa Venezuela ambao huandamana mchana na kukusanyika nyakati za usiku na kupambana na maafisa wa polisi pamoja na walinzi wa taifa nchini kote.
Mapema wiki hii Marekani ilitangaza kuwawekea vikwazo viongozi 13 wa ngazi za juu wa Venezuela, wa sasa na wa zamani, kwa madai ya kuhusika na makosa ya rushwa, kudhoofisha demokrasia ya nchi na kushiriki katika vitendo vya ukandamizaji.
SHARE
No comments:
Post a Comment