BENNY MWAIPAJA, WFM,
DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amefanya ziara
ya kushitukiza katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam na kuamuru kituo cha Mafuta cha GBP kifungwe hadi hapo
kitakapo funga mashine maalumu za kutolea risiti baada ya kubainika hakitumii
ipasanyo mashine za kieletroniki za kukusanyia kodi (EFD)
Dkt. Mpango amechukua hatua hiyo baada ya kujionea kituo hicho
kikiwa na pampu nne za mafuta lakini kuna mashine moja pekee ya mkononi ya
kutolea risiti jambo linasababisha wateja wao wengi kutopewa risiti na hivyo
kuikosesha Serikali mapato yake na ni kinyume cha sheria za nchi.
“Sasa nawachukulia hatua ili liwe fundisho kwa wengine wote
wanaouza mafuta nchini bila kufuata taratibu, na nitaanza na wewe, biashara
yako isimame mpaka mashine zifungwe kwenye kituo chote na utekeleze mara moja”
alisistiza Dkt. Mpango
Katika ukaguzi wa Kituo cha Mafuta cha Puma, Dkt. Mpango amesifu
utaratibu mzuri uliowekwa na kituo hicho kwa kufunga mashine maalumu za kutolea
risiti zilizounganishwa na kila pampu za mafuta kitu ambacho ndicho Serikali
inavitaka vituo vyote vya mafuta vitumie mfumo huo
“Kituo hiki kimezingatia sheria sheria kwa kufunga mashine kwa
kuzingatia maelekezo ya Serikali na hapa tunauhakika wa kupata fedha za
kuwatumikia wananchi, kinyume kabisa na kituo cha mafuta nilichokifungia, hapa
ndio ningeomba Watanzania wanunue mafuta” aliongeza Dkt. Mpango.
Ameiagiza Mamlaka ya mapato Tanzania-TRA kufanya ukaguzi nchi
nzima ili kubaini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaokiuka maagizo ya Serikali
yaliyowataka wafunge mashine hizo maalumu tangu mwaka uliopita.
Waziri wa Fedha na Mipango amewageukia wenye vyombo vya moto
wanaonunua mafuta kwenye vituo vya mafuta kote nchini kudai risiti wanapopata
huduma ya kuwekewa mafuta kwenye vituo hivyo ili kuokoa fedha za Serikali
zinazoishia mikononi mwa wajanja wachache wanaokwepa kodi kwa makusudi na
kuikosesha Serikali mapato yake.
Baadhi ya wananchi wamepongeza uamuzi wa Serikali kupitia Waziri
wa Fedha na Mipango wa kufanya ziara za kushitukiza kwenye vituo vya mafuta na
kutaka hatua hiyo iwe endelevu kwa maafisa wengine wa Serikali ili kukomesha
vitendo vya wenye vituo vya mafuta kukwepa kodi ya Serikali
Katika siku yake ya kwanza ya ziara za namna hiyo, Julai 10
mwaka huu, Dkt. Mpango alikifungia kituo cha Mafuta cha Mawenzi kilichoko
Kigamboni, Jijini Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa kituo hicho kimefunga
mashine maalumu za kutolea risiti za kielektroniki lakini hazitumiki na kuamuru
kituo hicho kifungwe hadi kitakapo rekebisha kasoro hiyo na kuvionya vituo vya
mafuta vya OilCom kufunga mashine za aina hiyo mara moja.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, akizungumza na mmoja wa wasimamizi wa kituo cha mafuta jijini
Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kushtukiza kukagua vituo vya
mafuta jijini vinavyokiuka taratibu za mauzo kwa kutokutoa risiti za
EFDs.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)
(mwenye miwani) akizungumza na wananchi pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha
Mafuta cha Puma, kuhusu umuhimu wa kutoa na kudai risiti baada ya kukagua kituo
hicho na kuridhika namna mashine za kieletroniki za kutolea risiti
zinavyofanyakazi ipasavyo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akiwa
katika mitaa ya maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,
Jijini Dar es Salaam, akizungumza na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kuhusu
umuhimu wa kudai risiti wanaponunua mafuta kwenye vituo vya mafuta na
kuitaarifu Serikali wanapobaini wamiliki wa vituo hivyo hawatoi risiti za EFD.
Waziri Mpango akishuhudia jinsi wananchi wanavyohudumiwa kwenye kituo cha mafuta jijini Dar es Salaam leo Julai 11, 2017.
Kulia ni Ally Gidai Mkazi wa Vingunguti akimueleza Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) kero wanayoipata
katika vituo vya mafuta ambavyo havitoi risiti kwa kutumia Mashine za
kielektroniki za EFDs. Hii ni baada ya Waziri huyo kueleza umuhimu wa kudai
risiti katika vituo vya mafuta.
SHARE
No comments:
Post a Comment