NA K-VIAS BLOG/KIGOMA
KWA wakazi wa Manispaa ya Mji wa
Kigoma-Ujiji, watakubaliana na mimi kuwa kero ya upatikanaji maji safi
na salama ya kunywa imekuwa ni miongoni mwa kero tatu kubwa na za muda
mrefu mkoani humo.
Kero nyingine ambayo sasa imekuwa ni
historia ilikuwa ya upatikanaji wa umeme, wakati ile ya miundombinu ya
barabara na reli kila mtu anajua ilivyosumbua kwa miaka mingi.
Yumkini kero ya umeme na miundombinu hususan ya barabara sasa inaanza kuondoka, ikabaki kero ya upatikanaji maji.
Jambo lililosikitisha wengi ni kwamba,
Manispaa ya Mji wa Kigoma-Ujiji, imebarikiwa kuwa na ziwa lenye maji
baridi, ziwa Tanganyika, hivyo swala la uwepo wa maji mkoani humo sio
tatizo tatizo kubwa ilikuwa ni miundombinu ya kuhifadhi na kusambaza
maji hayo ili kuwafikia wananchi.
Nakumbuka, aliwahi kutokea mbunge mmoja
kutoka Chama Tawala CCM, ambaye sasa sijui yuko wapi, naye ni Mhe.
Hamilimenshi Kahena Mayonga, mheshimiwa huyu, yeye akifika bungeni,
alikuwa hana hoja nyingine bali ni kulilia mambo hayo matatu kila
wakati, lakini hadi anamaliza muda wake na kutupwa nje ya siasa za
uwakilishi kutoka mkoani humo, hakuna hata kero moja iliyoshughulikiwa
hata walipokuja akina Mhe. Kabourou na wengine wengi mambo yalibaki kuwa
yale yale hadi ikafikia wakazi wa mji wa Kigoma kutamani kuwa mkoa wao
uhame kutoka mipaka ya Tanzania na kuwa kwenye mipaka ya nchi jirani
jambo ambalo kwa maoni yangu isingekuwa suluhisho kwani huko kwa wenzetu
pengine kuna shida nyingi kuliko zile ambazo wakazi wa mkoa wa Kigoma
walizipitia.
Alipokuja Mhe. Zitto Kabwe, ambaye ni
Mbunge wa Kigoma Mjini, mwanzo akiwa kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
walau mabadiliko fulani katka kuatatua kero hizi yalianza kuonekana,
mwanzo palifungwa mashine mpya ya kufua umeme, na hivyo changamoto ya
upatikanaji wa umeme kwenye Manispaa hiyo ikatatuliwa, baadaye, wakati
wa utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete, kero ya
pili ya miundombinu ya barabara nayo ikaanza kutatuliwa kwa barabara ya
Kasulu, ambayo ndiyo barabara kuu inayotoka mkoani Kigoma kwenda mikoa
ya Mashariki na kwingineko nchini nayo ikaanza kuwekwa lami.
Wakati huo Waziri aliyekuwa anashughulikia Ujenzi, alikuwa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Hata hivyo kuna kipande cha barabara
kilisalia kuwa vumbi, na furaha ya wakazi wa Kigoma-Ujiji imerejea tena
hapo majuzi baada ya Mhe. Rais kuzindua ujenzi wa kipande hicho cha
barabara kilichosalia ili sasa wananchi waweze kusafiri kwenye barabara
ya lami mwanzo mwisho kama wenzao wa mikoa mingine.
Lakini jambo mbalo litakuwa kumbukumbu
ya kudumu kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma kwa Rais wao Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli ni hili la sasa la kuzindua mradi wa maji ambao sasa utakuwa
umetatua kabisa kero ya upatikanaji wa maji safi na salama tena ya bomba
kwa wakazi wa Manispaa hiyo inayosifika kwa kuwa na ardhi nzuri ya
kilimo lakini kuwa na wananchi wenye kupenda kufanya kazi. Hongera sana
Dkt. Magufuli na hongera Mbunge Zitto Kabwe, wananchi wa Kigoma nina
hakika hawatawasahau.
SHARE
No comments:
Post a Comment