Na Tiganya Vincent-RS-Tabora
Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC) limeikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Tabora
nyumba 32 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 ambazo zitalipwa kwa
kipindi cha miaka saba.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya pande zote kukaa chini na kusainiana Mkataba wa
kuuziana nyumba hizo bei kwa ajili makazi ya Watumishi wa Halmashauri
hiyo ambao walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwa sababu ya
ukosefu wa nyumba za watumishi katika eneo la ofisi yao.
Nyumba
hizo zilikabidhiwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. Angeline Mabula (Mb),kwa niaba ya NHC katika eneo la
Isikizya Wilayani Uyui.
Akizungumza
kabla ya kukabidhi nyumba hizo alisema ni vema Halmashauri ya Wilaya ya
Tabora ikaheshimu makubaliano ya kuuziana nyumba hizo ya kulipa kila
mwezi shilingi milioni 260 kama walivyokubaliana ili fedha
zitakazopatikana ziweze kusaidia katika ujenzi wa nyumba katika meneo mengine.
Katika
hatua nyingine Mhe. Mabula alizitaka Halmashauri zote za Wilaya hapa
nchini zihakikishe zinapima na kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuzuia
migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika maeneo
mbalimbali.
Alisema
hatua hiyo itasaidia katika uondoaji wa migogoro ambayo imekuwa
ikisababisha mapigano na itawezesha miji na vijiji kupangika vizuri.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri alisema kuwa baada ya
Halmashauri hiyo kununua nyumba hizo hakutakuwepo kwa kisingizio cha
mfanyakazi kuishi Tabora mjini badala yake wanatakiwa kuwepo wakati wote
eneo la Isikizya.
Alisema
hatua hiyo itasaidia kuipungizia mzigo Halmashauri ya Wilaya ya Tabora
wa gharama zikiwemo za matumizi ya mafuta ya magari ambayo yalikuwa
yakitumika kuwasifirisha watendaji kutoka Tabora Mjini hadi eneo ilipo
Ofisi ya Halmashauri hiyo.
Mkuu
huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa hivi sasa hataki kuona Mfanyakazi anaishi
nje ya eneo hilo kwa kisingizio cha kukosa nyumba ya kuishi.
Kwa
upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora Hadija
Makuwani alilishukuru Shirika la Nyumba kwa kuwauzia nyumba hizo ambazo
wanapaswa kulipa deni hilo kwa kipindi cha miaka saba kwa kiwango cha
shilingi milioni 260 kila mwaka.
Aliongeza
kuwa wataheshimu mkataba waliofikia na Shirika la Nyumba wa kulipa kila
mwezi ili ndani ya kipindi walichokubaliana wamalize deni.
SHARE
No comments:
Post a Comment