Na: Veronica Kazimoto
ZOEZI la kuorodhesha kaya kwa
ajili ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka
2017/18 linaendelea nchi nzima ikiwa ni maandalizi ya utafiti huo unaotarajia
kufanyika hivi karibuni.
Akizungumzia zoezi hilo, Meneja
wa Takwimu za Jamii na Watu, Sylvia Meku wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema mpaka
sasa mikoa kumi na tatu (13) imekamilisha zoezi hilo ambapo ni sawa na silimia
50.
“Zoezi la kuorodhesha kaya kwa
ajili ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka
2017/18 linaendelea vizuri na mpaka sasa wadadisi wamekamilisha kuorodhesha
kaya katika mikoa 13,” amesema Sylvia Meku.
Ameitaja mikoa iliyokamilisha
zoezi la uorodheshaji wa kaya kuwa ni pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Manyara,
Iringa, Njombe na Morogoro. Mikoa mingine ni Mwanza, Tabora, Katavi, Mbeya,
Mara, Kagera na Lindi.
Zoezi la Uorodheshaji wa Kaya
linafanyika mikoa yote ya Tanzania Bara na linatarajia kumalizika mwishoni mwa mwezi Julai, 2017.
Utafiti kama huu mara ya mwisho ulifanyika Mwaka 2011/12 ambao ulionesha
kuwa asilimia 28.2 ya Watanzania wanaishi chini ya mstari wa Umaskini wa mahitaji
ya Msingi.
Utafiti wa Mapato na Matumizi
ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 unafanywa na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na baadhi ya Wadau wa
Maendeleo kwa lengo la kupata viashiria vya kupima hali ya umaskini nchini.
Mdadisi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akihoji taarifa za kaya
wakati wa zoezi la kuorodhesha kaya kwa ajili ya Utafiti wa Mapato na Matumizi
ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18 linaloendelea kufanyika nchini ikiwa
ni maandalizi ya utafiti huo unaotarajia kufanyika hivi karibuni.
Mdadisi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akiwaoneyesha wasimamizi
namna alivyojaza taarifa za kaya wakati wa zoezi la kuorodhesha kaya kwa ajili
ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18
linaloendelea kufanyika nchini ikiwa ni maandalizi ya utafiti huo unaotarajia
kufanyika hivi karibuni. (PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA)
SHARE
No comments:
Post a Comment