Kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba.
****
JESHI
la Polisi mkoani Singida linawashikilia watu wawili kutokana na kifo
cha mashaka cha mfanyabiashara, Tausi Hamisi au Angel Edward (39) mkazi
wa eneo la Ipembe mjini Singida.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Singida, Debora Magiligimba aliwataja wanaoshikiliwa
kuwa ni Haruna Athuman (34) mlinzi wa Katala Beach Hotel (KBH) ambaye
anaishi eneo la Kindai mjini Singida na Salma Mohamed (28) mkazi wa
Majengo katika Manispaa ya Singida.
Magiligimba
alisema kuwa tukio hilo ni la Agosti 24, mwaka huu saa 11.30 alfajiri
ambapo inadaiwa kuwa mwili wa mfanyabiashara huyo ulikutwa pembeni mwa
choo cha wanawake katika hoteli hiyo.
Alisema
kuwa siku ya Jumatano Agosti 23, mwaka huu majira ya jioni marehemu
aliondoka nyumbani kwao akiwa na gari yake ndogo kisha kuungana na
wenzake kwenda ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu (TIA) eneo la Ginnery mjini
hapa ambapo kulikuwa na harusi.
Hata
hivyo, Magiligimba alidai kuwa baadae usiku huo marehemu akiwa na
wenzake walienda Skyway Night Club eneo la Kibaoni alikokuwa anatumbuiza
mwanamuziki mashuhuri, Christian Bella kuendelea na starehe.
Inadaiwa
baada ya muda, alitoka Skyway na kwenda KBH akiwa ameambatana na rafiki
yake aitwaye Salma Mohamed pamoja na mwanaume mmoja ambaye hakufahamika
jina wala makazi yake mara moja ambapo inasemekana waliendelea na
starehe hotelini hapo.
"Ilifika
muda marehemu alienda kujisaidia chooni ndipo mwanaume huyo aliyekuwa
amekaa naye alimfuata. Hakuweza kurejea tena hadi mlinzi alipogundua
mwili wa marehemu alfajiri. Muuaji aliondoka na simu ya marehemu huku
akiacha gari lake hotelini hapo", alisema.
Kwa
mujibu wa Kamanda Magiligimba, uchunguzi wa daktari unaonesha kuwa
chanzo cha kifo cha marehemu ni kukosa hewa na kwamba hakuna dalili
zozote za kunyongwa shingo.
Ametoa
wito kwa wakazi wa mkoa huo kubadilika na kuacha tabia ya kuambatana na
watu wasiowafahamu kwenye maeneo ya starehe na inapotokea wawe wepesi
wa kudadisi na ikiwa watamtilia shaka watoe taarifa polisi haraka.
Na Abby Nkungu- Malunde1 blog Singida
SHARE
No comments:
Post a Comment