Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameelezea kutoridhishwa kwake na hatua zinazochuliwa na Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji dhidi ya watu waliouziwa viwanda na kisha
kuvitelekeza na amemtaka Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Charles Mwijage
kuvinyang’anya na kuwapatia wawekezaji wanaoweza kuviendeleza.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana muda mfupi kabla ya kufungua
kiwanda cha kuzalisha saruji cha Kilimanjaro kilichopo katika eneo la
Maweni Mjini Tanga ambako alikuwa akiendelea na ziara yake ya siku 5
Mkoani Tanga.
Magufuli
alisema nchi nzima ina viwanda 197 vilivyotelekezwa baada ya
kubinafsishwa takribani miaka 20 iliyopita, vikiwemo viwanda vilivyopo
Mkoani Tanga lakini anashangaa kuona Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji havinyang’anyi licha ya kutoa maelekezo ya kufanya hivyo mara
kadhaa.
Magufuli
pia aliwaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kufanya tathmini ya viwanda
vyote vilivyobinafsishwa katika maeneo yao ili kubaini ambavyo havifanyi
kazi na kutafuta wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha.
Kiwanda
cha Saruji cha Kilimanjaro kina uwezo wa kuzalisha tani 300 za saruji
kwa siku na kinatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 3,000 kwa
siku mwaka ujao.
Baada
ya kufungua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro Rais aliweka jiwe la
msingi la upanuzi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga (Tanga
Fresh) ambacho kinatarajia kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita
50,000 kwa siku hadi kufikia lita 120,000 hatua ambao inatarajiwa
kuongeza idadi ya wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.
Kiwanda
hicho kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya wafugaji 24 kwa asilimia
42 na mwekezaji kutoka Uholanzi kwa asilimia 58 na upanuzi unaofanywa
utaongeza uwekezaji kutoka Shilingi Bilioni 12 hadi kufikia Shilingi
Bilioni 26.5.
Akiwa
kiwandani hapo Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kukabidhi hati miliki ya kiwanda hicho kwa
menejimenti ya kiwanda, na ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
iliyokuwa ikidai kodi ya ongezeko la mtaji kuelekeza madai hayo kwa
mmiliki wa awali wa kiwanda hicho aliyewauzia wakulima.
Rais
Magufuli alimuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.
Charles Mwijage kuchukua hatua dhidi ya kiwanda cha maziwa cha Arusha
ambacho baada ya kubinafsishwa kimegeuzwa kuwa kituo cha kukusanyia
maziwa na kuyasafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kusindikwa.
Pia amemuagiza Waziri Mwijage kuwa nchi yoyote itakayozuia maziwa ya Tanzania nayo izuiwe kuingiza maziwa yake hapa nchini.
Aidha,
Rais Magufuli alitoa siku 5 kwa Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvivu Dkt.
Charles Tizeba kufika kiwandani hapo na kushughulikia changamoto
zinazokikabili kiwanda hicho.
Rais
Magufuli amefungua awamu ya kwanza ya mradi wa kituo cha matanki ya
mafuta cha GBP kilichopo katika eneo la Raskazone Mjini Tanga ambacho
kina uwezo wa kuhifadhi lita Milioni 122.6 na ambacho kinatarajia
kupanuliwa hadi kufikia lita Milioni 300 ifikapo katikati ya mwaka ujao.
Magufuli
alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa GBP Bw. Badar Sood kwa uwekezaji huo
mkubwa wa Shilingi Bilioni 60 utakaojumuisha ujenzi wa kiwanda cha
vilainishi na kiwanda cha kusindika gesi na alimhakikishia kuwa Serikali
itaendelea kumuunga mkono wakati wowote.
Pia
alimpongeza Bw. Sood kwa kulipa kodi ipasavyo ambapo katika mwaka miaka
miwili iliyopita ameongeza malipo ya kodi kutoka Shilingi Bilioni
208.950 hadi kufikia Shilingi Bilioni 293.263 na amewahakikishia
wawekezaji wote wanaolipa kodi ipasavyo kuwa wapo salama na Serikali
itawalinda.
Rais
Magufuli alielezea kutoridhishwa kwake na kusuasua kwa mchakato wa
ununuzi wa mita za kupimia mafuAta yanayoshushwa kutoka melini (Flow
Meter) na ametaka Wizara zinazohusika katika mchakato huo kununua mita
hizo haraka ili mafuta yanayoingia nchini yapimwe kwa usahihi na
kukusanya kodi stahili.
Leo Rais Magufuli atahitimisha ziara yake Mkoani Tanga kwa kuzungumza na wananchi wa Wilaya za Korogwe na Handeni.
SHARE
No comments:
Post a Comment