
Mratibu wa shirika la Singida IR
Vicoba Net work (SIRVICONET) Happy Francis, akitoa ufafanuzi wa jambo
kuhusu mafunzo juu ya umiliki ardhi kwa wanawake. Mafunzo hayo
yamefanyikia kwenye ukumbi wa mikutano kituo cha walimu barabara ya
Nyerere mjini hapa.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo juu
ya umiliki wa ardhi kwa wanawake yaliyoandaliwa na shirika la
SIRVICINET na kufadhiliwa na shirika la The Foudation For Civil Society.

Mwezeshaji Lilian Msasi, akitoa
mafunzo juu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake yaliyoandaliwa na shirika
la SIRVICONET na kufadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil
Society.
Picha/habari na Nathaniel Limu
……………………..
Wanawake Mkaoni Singida
wamehimizwa kujenga utamaduni wa kujiamini na kuondoa woga, ili waweze
kufanikiwa kupigania haki zao za msingi, ikiwemo ya haki ya kumiliki
ardhi.
Wito huo umetolewa na diwani wa
kata ya Mungumaji Hassan Shabani Mkata, wakati akichangia mada juu ya
haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake kwenye mafunzo yaliyofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha walimu mjini hapa.
Mafunzo juu ya haki ya mwanamke
kumiliki ardhi yaliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Singida
IR Vicoba Net Work (SIRVICONET) na kufadhiliwa na shirika la The
Foundation for Civil Society kwa ajili ya wanawake wa Singida.
Mkata amefafanua kuwa katiba ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uhalali wa umiliki ardhi kwa
wanawake, isipokua wanawake wenyewe wanakosa haki hiyo kutokana na woga
wao uliopitiliza.
Amesema umefika wakati sasa
wanawake wawe mstari wa mbele kupingania haki zao na kutokomeza mila
kandamizi, ziliyopitwa na wakati ambazo zinawakandamiza kwamba hawana
haki ya kumiliki ardhi.
“Kwa hilo wanawake watafanikiwa tu
endapo wataondoa woga, wakajiamini na wakaunganisha nguvu zao.
Nasisitiza, wanawake wanapaswa kutambua kuwa wanahaki sawa na wanaume,
katika kumiliki ardhi”, amefafanua.
Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo
Afisa Ardhi kutoka Manispaa ya Singida, Lilian Msasi amesema ardhi ni
mali ya umma na imekabidhiwa kwa rais, kwa niaba ya Watanzania wote.
“Raia wote…. wanawake na wanaume
wana haki sawa ya kupata, kumiliki, kutumia na kugawana ardhi. Miliki za
ardhi zilizopo zinatambuliwa na kulindwa kisheria”, amesema Msasi.
Msasi amesema mwanamke ana haki
sawa na mwanaume katika kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi. Haki
hiyo imetamkwa kwenye kifungu cha tatu (92) cha sheria ya ardhi mjini na
sheria ya vijiji za mwaka 1999.
Kuhusu sifa za kuomba haki ya
kumiliki ardhi, Lilian amesema kuwa ni mtu ye yote mwanamke au mwanaume,
mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anaweza kupatiwa hati ya
kumiliki ardhi.
“Pia kikundi cha watu ambao sio
raia wa Tanzania, wanaweza kuomba haki ya kumiliki ardhi (delivative
righs), kwa ajili ya uwekezaji”, amesema.
Ameongeza kuwa kwa vile wanawake
ni watumiaji wakuu wa ardhi, vyombo vinavyohusika na masuala ya
usimamizi na utendaji wa ardhi, vihakikishwe kuwa wanawake na wanaume
wanashirikishwa ipasavyo katika masuala yahusuyo ardhi
Awali Mratibu wa Shirika la
SIRVICONET, Happy Francis, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea
uwezo zaidi wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata, maafisa watendaji wa
kata na maafisa maendeleo ya jamii, ili waweze kutekeleza majukumu yao
kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa dhamira ya
SIRVICONET ni kuwezesha wanachama wake kuwa na nguvu kiuchumi katika
kupambana na umaskini, ujinga na maradhi na kuwa na mahusiano mazuri
miongoni mwao.
SHARE
No comments:
Post a Comment