![]() |
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akiwahutubia Wananchi wa Wilaya ya Sikonge Mjini Agosti.10.2017
katika viwanja vya Tasaf Waziri Mkuu yupo Mkoani Tabora kwa ziara
ya Kikazi
|

NA OWM, SIKONGE
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya Sikonge, Bw.
Evans Shemdoe ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80 ya
makusanyo ya ndani.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo asubuhi (Alhamisi, Agosti 10, 2017) wakati
akizungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.
“Nataka
maelezo yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya
halmashauri ambacho ni kiwango cha chini. Nzega TC wamefikisha asilimia 112,
Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana asilimia 80, ni kwa nini wewe umeshindwa
kufikisha kiwango hicho?,” alihoji Waziri Mkuu.
“Ninataka
nipate maelezo pia ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato kwa maeneo
mliyoshindwa kufanya vizuri, na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa fedha.
Niyapate maelezo hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” amesema.
Alipopewa
nafasi ya kujieleza, Bw. Shemdoe alisema wamefikisha asilimia 76.7 na
wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu uliopita,
hali ambayo ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku miongoni mwa
wakulima.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na
watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia
watendaji wa kata peke yao.
Jana, mara baada ya
kupokea taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri tano kati
ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini zimeshindwa kufikisha asilimia 80
ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa na Serikali.
“Halmashauri
zilizovuka malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega DC. Nataka taarifa za
halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni kwa nini hawajafikia
malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni asilimia 80,” alisema.
Taarifa
ya mkoa huo inaonyesha makusanyo kwa kila Halmashauri ni kama ifuatavyo:-
Tabora Manispaa asilimia 64.1; Nzega Mji (asilimia 112); Nzega Wilaya (asilimia
80.8); Igunga (asilimia 64.6); Tabora (asilimia 77.3); Sikonge (asilimia 76.7);
Urambo (asilimia 70.9) na Kaliua (asilimia 91.5).
Pia
amezitaka Halmashauri zote zihakikishe zinafanyamakusanyo kwa kutumia mfumo wa
kielektroniki. “Ukusanyaji wote wa mapato ni lazima ufanyike kwa mfumo wa
kielektroniki. Halmashauri ambazo hazijafanya hivyo, zitumie makusanyo ya mwaka
jana kununulia mashine za EFD. Hatutaki kuona risiti za kuandika kwa mkono
zinatumika,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora uhakikishe
wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wilaya hiyo
ili waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya mapato.
“Hapa
Sikonge naambiwa hakuna ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa TRA katika kila
Halmashauri ili watoe elimu na washirikiane na madiwani, watendaji wa vijiji na
watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji mapato,” alisema.
SHARE
No comments:
Post a Comment