
Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akimkabidhi msaada wa
vifaa vya maabara, stuli za kukaliwa wanafunzi wakati wa mazoezi kwa
vitendo kwa aliyekuwa mkuu wa shule ya sekondari Kishapu ambaye sasa ni
mratibu elimu kata ya Sekebugora, mwalimu Hosea Somi.

Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akikagua mojawapo ya
vyoo va nyumba za walimu katika shule ya sekondari Kiloleli kata ya
Kiloleli wilayani humo.

Sehemu ya nyumba za walimu katika
shule ya sekondari Kililoli kata ya Kiloleli wilayani humo ambazo ni
mojawapo ya mpango wa halmashauri kuboresha sekta hiyo muhimu.
……………………..
Na Robert Hokororo, Kishapu DC
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
mkoani Shinyanga inaendelea na mkakati wake wa kuboresha mazingira ya
sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu katika shule zake mbalimbali.
Inafanya hivyo kupitia programu
mbalimbali zikwemo Mpango wa kuboresha Miundombinu katika shule za
sekondari (SEDP) ili kumpa mwanafunzi mazingira mazuri ya kujifunza.
Pia halmashauri hiyo kupitia Idara
ya Elimu Sekondari ina jukumu kubwa la kuhakikisha shule zake zinafanya
vizuri katika mitihani ya kitaifa na hatimaye kuitoa kimasomaso wilaya
kitaaluma.
Imekuwa ikitekeleza miradi
mbalimbali ikiwa na lengo la kupanua wigo wa elimu katika shule
mbalimbali za sekondari na hivyo wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya
kujifunza.
Wanafunzi wanapokuwa na mazingira
mazuri ya elimu ikiwemo miundombinu rafiki kwao wanakuwa na ari ya
kujifunza na hatimaye kufaulu.
Vile vile walimu nao wanapokuwa na
wamewekewa mazingira mazuri ya kufundishia huweza kufanya kazi kwa
nguvu moja na kwa moyo wote.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi
wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo endapo vikiwa
katika ubora vinakuwa motisha kubwa kwa walimu na wanafunzi.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga alikabidhiwa miradi
ya miundombinu ya shule za sekondari iliyokamilika ujenzi wake.
Katika shule ya sekondari Bubiki
tayari vyumba vinne vya madarasa pamoja na matunda ya vyoo 18 yamejengwa
kwa ajili ya wanafunzi na walimu, hali itakayosaidia kuboresha maisha
yao.
Akibainisha hayo katika makala
haya, Magoiga anasema mradi huo ambao umegharimu jumla ya sh. milioni
147.8, umetekelezwa katika kata ya Bubiki na hivyo kupunguza au kutatua
kabisa changamoto ya uhaba wa vyoo na vyumba vya kwa wanafunzi.
Si hivyo tu bali pia
halmashauri imeendeleza miradi hiyo katika kata zingine zikiwemo
Mwakipoya, Mwamalasa na Masanga ambapo imeborsha miundombinu katika
shule zake.
Magoiga anafafanua kuwa shule ya
sekondari Mwakipoya yamejengwa matundu 18, Mwamamalasa matundu 18 na
Bulekela iliyoko kata ya Masanga jumla ya matundu 18 pia.
Mkurugenzi mtendaji huyo anaweka
wazi kwa kusema gharama za mradi huo ni sh. milioni 115.9 ambapo tayari
umekabidhiwa katika shule hizo tayari kwa matumizi.
Hata hivyo ili wanafunzi wafanye vizuri shuleni ni muhimu walimu kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na hata makazi yao.
Kwa kuliona hilo halmashauri
imekuwa ikijitihadi kuwawekea mazingira mazuri walimu katika shule
mbalimbali kama ambavyo mkurugenzi amekuwa akisisitiza.
Kama inavyofahamika mwalimu ni mtu
muhimu katika ustawi wa wanafunzi na ni mzazi kwa kuwa hutumia muda
mrefu na wanafunzi kuliko alivyo mzazi.
Pia kazi ya ualimu ni wito kama
walivyo wafanyakazi wa sekta ya afya hivyo mwalimu anapaswa kujengewa
uwezo na mazingira mazuri ya kazi yake.
Ikumbukwe hivi karibuni Mkurugenzi
Mtendaji Magoiga aliwataka wakuu wa shule wilayani Kishapu kutoa
motisha kwa walimu wanaofanya vizuri katika ufundishaji.
Ni dhahiri kuwa motisha hiyo ni
pamoja na kuwajengea miundombinu ya makazi kwa maana ya nyumba bora
karibu na maeneo yao kazi kwenye shule.
Katika kata ya Kiloleli wilayani
humo, jumla ya nyumba sita za walimu zimejengwa kwa sanjari na tangi la
kuvunia maji ya mvua lenye ujazo wa lita 30,000.
Magoiga anasema kuwa mradi wa
nyumba hizo zenye kila aina ya huduma umegharimu jumla ya sh. milioni
149.1 na tayari umeanza kutumika.
Kutokana na kukamilika kwa mradi
huo sasa walimu wameondokana na adha ya kupanga mbali na shuleni hali
iliyowasababishia kuchelewa kufika vituo vyao vya kazi.
Kutokana na kupata makazi karibu na shuleni walimu hao wataweza kufanya kazi zao za kufundisha kwa ufanisi mkubwa kwa kuwahi.
Miongoni mwa vitu muhimu kwa
ufundishaji ni mafunzo kwa njia ya vitendo (practical) hususan katika
masomo ya Sayansi ambapo kupitia hivi mwanafunzi anakuwa na uwanja mpana
wa kujifunza.
Tayari mkurugenzi mtendaji ametoa
vifaa vya maabara vikiwemo stuli 135 kwa ajili ya shule tano za
sekondari zilizopo kata mbalimbali wilayani humo.
Mradi huo wenye thamani ya sh.
milioni 6.75 umefadhiliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) chini ya mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R).
Magoiga anabainisha kuwa nchi ya
viwanda kama ambavyo ilivyo sera ya Serikali ya Awamu ya tano inatokana
na masomo ya sayansi na hivyo mojawapo ya vipaumbele vyake ni kuboresha
sekta ya elimu.
Mradi mwingine ni vitanda kwa
mabweni ya Shule ya Sekondari Kishapu ambapo Magoiga alikabidhi jumla ya
vitanda 31 vyenye thamani ya Sh. 4,650,000 ikiwa ni kutokana na fedha
zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Mkurugenzi alitoa ahadi ya vitanda
hiyo Septemba 2016 alipofanya ziara shuleni hapo na kukuta changamoto
ya uhaba wa vitanda ambavyo vilikuwa ni 10 tofauti na mahitaji ya
wanafunzi wake.
Shule hiyo ambayo katika matokeo
ya kidato cha nne mwaka 2016 ilishika nafasi ya pili kimkoa kati ya
shule nane sasa imeondokana na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi
kukosa vitanda.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa
Idara ya Elimu Sekondari Wilaya, Paul Kasanda akizungumza na makala haya
anasema halmashauri inaendelea kutekeleza miradi katika sekta hiyo.
Anasema mradi wa vifaa vya maabara
ni miongoni mwa miradi mitatu kwa shule za sekondari zilizopo wilayani
humo ikiwa ni njia ya kuboresha sekta ya elimu.
Anataja baadhi ya miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mangu iliyopo kata ya Shagihilu.
Kasanda anasema kuwa kutokana na
misaada hiyo inayotolewa kutoka Serikali Kuu, sekta ya elimu katika
halmashauri hiyo itasonga mbele na hivyo ufaulu kwa wanafunzi utapanda.
SHARE








No comments:
Post a Comment