Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José
Graziano da Silva, Jumanne wiki hii ataanza ziara rasmi nchini Tanzania
ambapo anategemewa kufanya mikutano na mazungumzo na maofisa waandamizi
wa serikali na wadau.
Bw.
Graziano da Silva anategemewa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Mkurugenzi
Mkuu wa FAO amepanga kufanya mikutano na Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi (Tanzania Bara), Dkt. Charles Tizeba, na Waziri wa Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed.
Ziara
hii ya Mkurugenzi Mkuu inakuta wakati FAO ikiadhimisha miaka 40 toka
kuanza shughuli zake hapa Tanzania. Wakati wa ziara hii, Bw. Graziano da
Silva atakutana na uongozi na wafanyakazi wa FAO hapa Tanzania kabla ya
kuhudhuria hafla maalum hapa Dar es Salaam kusherehekea maadimisho
hayo. Hafla hiyo itahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Bi. Samia Suluhu Hassan.
Mwakilishi
Mkazi wa FAO hapa nchini, Bw. Fred Kafeero, amethibitisha kuwa Bw.
Graziano da Silva atakuwa hapa nchini kufuatia mwaliko wa Serikali ya
Tanzania. “Mkurugenzi Mkuu wa FAO atabadilishana mawazo na Serikali ya
Muungano wa Tanzania kwenye masuala makuu yanayohusiana na uhakika wa
chakula na maendeleo ya kilimo, ikijumuisha juhudi za FAO kitaifa na
kikanda,” alisema. Bw. Graziano da Silva pia atajadili mambo mengine
yanayohusiana na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
FAO, pia masuala mengine ya umuhimu kati ya pande hizo mbili, aliongeza.
Mbali ya Maafisa wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu atakutana na wadau
wengine wa FAO hapa nchini wakiwa ni pamoja na asasi za kiraia, taasisi
za elimu, na taasisi za utafiti.
Baadae
Mkurugenzi Mkuu ataenda Zanzibar ambapo, miongoni mwa mambo mengine,
anategemewa kuweka jiwe la msingi katika jingo la Mradi wa Kuzalisha
vifaranga vya samaki unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea
kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa KOICA. Pia Bw. Graziano
da Silva atapata fursa ya kutembelea mradi wa kilimo cha mwani na pia
kuona maonesho ya bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa na wanawake
wanaojihusisha na kilimo cha mwani.
Tanzania
ilijiunga na FAO mwaka 1962, na mwaka 1977 FAO ilifungua ofisi zake
hapa Tanzania. Katika miaka 40 ya uwepo wake, FAO imeisadia Serikali ya
Tanzania katika kupanga na kutekeleza sera, mikakati na mipango ya
kilimo hapa nchini. Kazi ya FAO imejikita katika kuboresha usalama wa
chakula na lishe pamoja na maisha ya wakulima wadogo na hivyo kuwa
chachu ya kukua kwa uchumi kupitia sekta ya kilimo.
SHARE
No comments:
Post a Comment