
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo mbele ya wajumbe wa
Bodi ya Kampuni ya Simu ya TTCL katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi
hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Maria
Sasabo na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Omary Nundu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya
Simu za Mkononi ya TTCL Mhandisi, Omary Nundu akielezea jambo wakati wa
hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Katikati
ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo
akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi ya Kampuni ya Simu ya
Mkononi ya TTCL leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa TTCL, Bw. Waziri Kindamba, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL
Mhandisi Omary Nundu na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa.

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya TTCL
wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa
Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na Frank Shija – MAELEZO
……………………..
Thobias Robert-Maelezo
21, sept 2017
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Mkame Mbarawa ameitaka Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya
kampuni ya mawasiliano nchini (TTCL) kuhakikisha kuwa inasimamia vyema
kazi na majukumu yake ili kuiwezesha kampuni hiyo kujiendesha kibiashara
na kuimarisha huduma za mawasiliano hapa nchini.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar
es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo ambapo aliwasisistiza kuwa
wachape kazi ili kurahisisha huduma mbalimbali za kimawasiliano hapa
nchini na kuhakikisha kuwa wanaendana na kasi ya serikali ya awamu ya
tano yenye sera ya hapa kazi tu.
“Nataka bodi mjue tunakwenda wapi
katika kampuni hii lakini pia tunahitaji kufanya kazi kwa juhudi,
kushindana na makampuni mengine ya simu, mhakikishe mapato makubwa
yanatoka kwenye data halikadhalika tujue mnapaswa mjue strenght (nguvu)
yenu iko wapi maana tusipojibu maswali haya hatuwezi kufanya ushindani
na makampuni mengine,” alifafanua Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa alisema kuwa,
Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji katika sekta ya mawasiliano
kiasi ambacho kimeongeza mapato pamoja na ushindani wa huduma ya
mawasiliano na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo hapa
nchini.
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa
serikali imefanya mabadiliko yaliyofanywa na serikali ili kuipa nguvu
Kampuni ya TTCL ikiwa ni pamoja na kuondoa ubia wa umiliki wa TTCL na
wawekezaji asilimia 35 na kuzirejesha serikalini, kujenga mkongo wa
taifa wa mawasilino, kujenga kituo cha taifa cha kuhifadhi kumbukumbu
(Data center) pamoja na kulipa madeni ya kampuni hiyo.
Aidha Prof. Mbarawa ameitaka Bodi
ya Wakurugenzi kuhakiksha kuwa TTCL inaleta mabadliko na maendeleo
katika kufikia sera ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda,
kuongeza wateja na watumiaji wa huduma zitokanazo na TTCL, kuwafikia
watumiaji wengi zaidi nchini kote na kuendelea kuwa kampuni bora ya
mawasiliano.
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa, TTCL
ni lazima wabadilike katika utoaji wa huduma zake, ili kuendana na
manadiliko ya teknolojia ambapo amewaeleza kuwa kwenye sekta ya
mawasiliano mambo yanabadilika kila siku, sekta inakua haraka na hata
uendeshaji wake unabadilika.
“Mathalani ukiangalia makampuni
makubwa kwa sasa, mapato yao yamebadilika kutoka kwenye sauti hadi data
pamoja na miamala ya pesa hivyo TTCL wanapaswa wajipime waangalie uwezo
wao uko wapi na nguvu zao ziko wapi ili waweze kujipanga vizuri
kuhakikisha wanashindana na makampuni mengine ya mawasiliano hapa
nchini,” alifafanua Prof. Mbarawa.
Awali akizungumza katika hafla
hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Mhandisi Omary Nundu, alisema
kuwa tangu ateuliwe katika bodi hiyo mambo mengi wameyafanya hadi sasa
ikiwemo kuifufua kampuni hiyo, kushirikiana na wadau wengine wa
mawasiliano pamoja na kuanzisha TTCL Pesa.
“Kwa sasa tunahudumia watu laki
tatu hapa nchini, lakini tumenuia mwisho wa mwaka huu wa fedha 2017/2018
tufikie wateja milioni moja na baada ya miaka mitano yaani ifikapo
2021/2022 tuwe na wateja milioni tano ambapo tutakuwa tumefikia asilimia
10 ya wateja wa soko la mawasiliano hapa nchini,” alifafanua Mhandisi
Nundu.
Aidha, Mhandisi Nundu aliendelea
kusema kuwa mwaka 2016, TTCL ilipata bilioni 0.21 katika soko lake na
zaidi mwaka huu wanatarajia kupata bilioni 0.3 na kwamba wanatarajia
kupata faida ya zaidi ya bilioni 40 ifikapo 2022 baada ya makato ya
kodi.
“Katika kuyafanikisha matarajio
yote haya, tunapaswa kupata jumla ya dola za kimarekani milioni 673,
ambapo dola milioni 300 tunatarajia kuzipata kama mtaji wa uwekezaji
kutoka serikalini, huku kampuni ikitafuta njia nyingine za kuapata fedha
zilizobaki katika mpango na matarajio yetu,” alifafanua Mhandisi Nundu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Mawasiliano Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo
alisema sekta ya mawasiliano ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi kwa
kurahisisha mawasiliano ya kati ya mtu na mtu na taifa kwa ujumla kwa
kurahisisha usambazaji na upatikanaji wa huduma na bidhaa kutoka sehemu
moja na nyingine.
“Sera ya serikali ya kuelekea
uchumi wa viwanda inatoa fursa kubwa kwa sekta ya mawasiliano kukua, pia
ukuaji wa shughuli za uchumi unachochea mahitaji ya mawasiliano
kuongezeka ikiwemo serikali mtandao, tiba mtandao, elimu mtandao,
biashara mtandao, utangazaji mtandao kwa njia ya runinga na radi,”
alifafanua Dkt.Sasabo.
Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL
iliteuliwa rasmi mwezi Februari 2017,na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni jitihada za kufufua na
kurejesha kampuni hiyo katika ushindani, kusimamia mawasiliano yote ya
serikali na kujiendesha kwa faida. Kwa sasa serikali inajiandaa kupeleka
muswada bungeni ili kuirasimisha TCCL iwe na bajeti ya kujitegemea.
SHARE








No comments:
Post a Comment