Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan akiwaonyesha wajumbe walioshiriki Kongamano la kwanza la
Kimataifa la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mpango mkakati
wa miaka mitano wa Kamisheni hiyo (kulia) Mtendaji Mkuu wa Kamisheni
Prof. Kenneth Simala na (kushoto) Rais Mstaafu wa Tanzania Ali Hassan
Mwinyi.
…………………………………………………………………………….
Maryam Kidiko na Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar.
KUANDALIWA kwa kongamano la
kwanza la Kimataifa la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ni
miongoni mwa juhudi za kuendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda huo
na Duniani kwa jumla.
Hayo ameyasema Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan wakati wa
ufunguzi wa Kongamano la Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki huko katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip iliopo Malindi
Mjini Zanzibar.
Alisema kongamano hilo
lililowashirikisha wataalamu wa lugha ya Kiswahili wa nchi wananchama wa
Afrika Mashariki lina umuhimu mkubwa katika historia ya maendeleo ya
Kiswahili duniani pamoja na kupanga mikutano na kubadilishana utalaamu .
Hivyo Alieleza kuwa ni muhimu
kwa kamisheni kusimamia kwa makini hadhi ya Kiswahili kama lugha ya
mawasiliano ikitambuwa kwamba ukanda wa Afrika Mashariki ni sehemu ya
Dunia yenye lugha tofauti.
Samia alisema uratibu na
uendelezaji wa Maendeleo na matumizi ya Kiswahili utaimarisha mchakato
na utengamano wa Jumuiya kwa maendeleo endelevu.
“Utengamano wa Jumuiya sio tukio
bali ni mchakato ambao unapaswa kuendeshwa na watu wenye kuelewa vizuri
matumizi endelevu ya Kiswahili “Alisema Makamo wa Rais.
Hata hivyo alielezea kuwa
mafanikio kamili yanategemea mkabala wa mawasiliano na ushiriki wa raia
wote katika maendeleo endelevu ya Jumuiya .
Alisema Kiswahili ni kiungo
muhimu kati ya wana Afrika Mashariki katika kujenga utambuzi na kubaini
changamoto pamoja na fursa zinazofungamana na maendeleo.
Alitaka kongamano hilo kuonyesha
namna ambavyo Kiswahili kinaweza kufanikisha utangamano na malengo ya
kuimarisha maendeleo ya nchi wanachama Afrika Mashariki
Waziri Samia alionyesha
kkufurahishwa kwake na nchi wanachama kutenga bajeti kila mwaka kwa
lengo la kuimarisha na kuendeleza shughuli za Kamisheni hiyo.
Nae Waziri wa Habari Utamaduni
Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe alisema baadhi ya Nchi za ukanda
wa Afrika Mashariki ambazo zilikuwa nyuma katika kutumia lugha ya
Kiswahili wamepiga hatua na kimeweza kusaidia katika kuharakisha
maendeleo yao.
Aliitaka Kamisheni hiyo kushirikiana na Wadau mbali mbali ili iweze kuleta maendeleo kupitia lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wa Waziri wa Habari
Utalii , Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alisema Serilkali ya
Zanzibar inathamini kuwepo Makao Makuu ya Kamisheni Zanzibar na
ameahidi itaendelea kuunga mkono kutokana na umuhimu wa lugha hiyo.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya
Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Profesa Kenneth Simala alisema
Kamisheni itafanya juhudi ya kuziunganisha nchi wanachama na asasi za
kiraia kukikuza Kiswahili.
Sambamba na hayo alisema
Zanzibar imeweza kutowa mchango mkubwa katika Nchi za Afrika Mashariki
kupitia lugha ya Kiswahili katika kukuza lugha hiyo.
Kauli mbiu ya Kongamano hilo la siku mbili ni ‘KULETA MABADILIKO KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUPITIA KISWAHILI.
SHARE
No comments:
Post a Comment