NA OWM, DODOMA
SERIKALI imesema hivi sasa inatoa sh. bilioni 22.2
kila mwezi ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana (Jumamosi, Septemba 2, 2017)
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. George Simbachawene wakati
akizungumza na wahitimu 166 wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Martin
Luther, kwenye sherehe za mahafali ya 10 zilizofanyika shuleni hapo katika
Manispaa ya Dodoma.
Waziri Simbachawene ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye
mahafali kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Serikali itaendelea
kuboresha elimu ya sekondari kwa kuajiri walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi.
“Wazazi wa wanafunzi wanaohitimu tunawakaribisha
kwenye shule za sekondari kwa sababu zote zina walimu wa kutosha, madawati na
vifaa vya kufundishia. Kila mwezi tunatenga sh. bilioni 22.2 kuendesha shule za
msingi na za sekondari hadi kidato cha nne,” alisema.
Alisema hivi sasa, baadhi ya shule zinakabiliwa na
changamoto ndogo ya upungufu wa walimu wa sayansi lakini nayo itatuliwa hivi
karibuni kwa sababu vibali vya ajira vimeanza kutolewa.
“Tunaendelea kuziboresha na tumeshuhudia miaka ya karibuni
wanafunzi bora kitaifa wakitoka katika shule za Serikali ambazo wengi wamezoea
kuziita ni shule za kata. Hakuna shule za kata. Zote ni zimejengwa na
Serikali,” alisisitiza.
“Ukienda vyuo vikuu, wanafunzi na ufaulu wa juu wengi
wao ni wale waliotoka kwenye shule za Serikali,” aliongeza.
Aliwataka wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao
Septemba 6 na 7, wasiwe na hofu kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwafanya
wachanganye mambo na kisha kufeli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Bw. Rabbiely Mmanga aliwaasa wazazi na
kuwaomba wasiwaingize watoto kwenye migogoro kwani matendo hayo yanawajisi
watoto na kuwaathiri kisaikolojia hata wawapo shuleni.
“Ninawaomba sana wazazi, tofauti zenu ziishie chumbani
na zisifike masikioni mwa watoto kwa sababu zinawasumbua kisaikolojia na
kuwaharibia concentration yao kimasomo. Tumewahoji baadhi na wamesema wanaumia
kwa kukumbuka adha ambayo mama anaipata kutoka kwa baba, au baba anaipata
kutoka kwa mama,” alisema.
Katika mahafali hayo, wanafunzi mbalimbali walipewa
vyeti kwa kufanya vizuri kwenye masomo mbalimbali huku Ismail Milambo na
Nise-Magreth Malila wakiibuka kidedea kwenye masomo yote (best academic
performers). Tuzo za nidhamu bora (discipline) zilichukuliwa na Michael Nyalusi
na Sayuni Kampuni.
Wanafunzi wengine waliopata tuzo na masomo yao kwenye
mabano ni Ismail Milambo (Hisabati), William Terry William (Kiingereza),
Majaliwa K. Majaliwa (Sayansi), Nise Malira (Kiswahili), Clinton Dotto (Social
Studies) na Justin Kilimali (Kompyuta).
Wengine walipewa tuzo kwenye vipengele vya michezo,
uchoraji na sanaa, usafi, uongozi shuleni, uimbaji na uongozi wa ibada.
Katika risala yao, wanafunzi wanaohitimu walisema wanaamini misingi ya elimu
walioipata kwenye shule ya Martin luther haitapotea bure na wakaahidi kufanya
mitihani yao kwa umakini ili watoke na ufaulu wa hali ya juu.
Wanafunzi wa darasa la saba kote nchini, wanatarajiwa
kufanya mitihani yao ya kitaifa Septemba 6 na 7, mwaka huu.
SHARE
No comments:
Post a Comment