Kaimu Mkrugenzi Mkuu wa TACAIDS
Bw.Jumanne Issango akieleza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo
pichani) wakati wa mkutano kuhusu changamoto na mafanikio katika
kupambana na ukimwi nchini uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za TACAIDS
leo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkrugenzi Mkuu wa TACAIDS
Bw.Jumanne Issango akieleza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo
pichani) wakati wa mkutano kuhusu changamoto na mafanikio katika
kupambana na virusi vya ukimwi nchini kulia ni Kaimu Mkurugenzi Muitiko
wa kitaifa wa TACAIDS Bi.Audrey Njelekela mkutano uliofanyika katika
ukumbi wa ofisi za TACAIDS leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na Paschal Dotto-MAELEZO
………………..
Na Fatma Salum – MAELEZO
21/09/2017
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania
(TACAIDS) imeendelea kuiasa jamii kuhusu kubadili tabia ili kuepuka
maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani ugonjwa huo bado ni janga kwenye
nchi yetu.
Hayo yamesemwa na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo Bw.Jumanne Issango alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio na changamoto
za tume tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake.
“UKIMWI bado ni changamoto katika
maendeleo ya Taifa letu na umeendelea kuathiri kila sekta, kila imani,
matajiri na masikini nchini kote hivyo ni wajibu wa kila mmoja
kujitathmini mwenendo wake na kuacha tabia hatarishi ambazo zinachangia
kuongeza maambukizi ikiwemo uasherati, ngono zembe, ulevi na kadhalika,”
alisema Issango.
Alieleza kuwa kwa miaka ya
karibuni hali ya maambukizi ya UKIMWI imeendelea kupungua ingawa kuna
tofauti kwenye mikoa, wilaya na makundi ya kijamii.
Issango alibainisha kuwa kiwango
cha maambukizi Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na takwimu hizo ni kutokana
na Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI mwaka 2012.
Kwa mujibu wa utafiti huo wanawake
walioambukizwa ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8 ambapo idadi
ya Watanzania wanaokadiriwa kuishi na VVU ni zaidi ya milioni 1.5.
“Mikoa inayoongoza kuwa na
maambukizi makubwa ni Njombe asilimia 14.8, Mbeya asilimia 9 na mikoa
yenye maambukizi ya chini zaidi ni Manyara asilimia 1.5, Tanga asilimia
2.4 na Dodoma asilimia 2.9,” alifafanua Issango.
Aidha alisema kuwa licha ya
maambukizi mapya kupungua kwenye jamii bado kiwango cha maambukizi
kwenye makundi maalum kimeendelea kuongezeka.
Akitaja makundi hayo Issango
alisema kuwa ni pamoja na madereva wa magari ya masafa marefu, wachimba
madini, wavuvi, wafungwa na wale wanaofanya biashara ya ngono.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Idara ya Muitikio wa Kitaifa kutoka Tume hiyo Bi. Audrey Njelekela
alisema Serikali kupitia TACAIDS inaendelea kufanya jitihada mbalimbali
za kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuandaa na kutekeleza mikakati
madhubuti itakayosaidia kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.
“Mkakati wa Tatu wa Taifa wa
Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18 unalenga ifikapo 2018 kiwango cha
maambukizi kishuke kufikia asilimia 0.16 ikilinganishwa na mwaka 2012
ambapo utafiti unaonesha maambukizi ni asilimia 0.32,” alisema
Njelekela.
Alitaja hatua nyingine
zinazochukuliwa na tume hiyo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma
hasa kwa vijana, wanawake wajawazito na makundi maalum ikiwemo kujenga
Vituo vya Maarifa vinavyotoa huduma za VVU/UKIMWI kwa madereva wa magari
ya masafa marefu.
Aliongeza kuwa juhudu za Serikali
kutoa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zimesaidia
kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo ambapo kwa sasa wanaotumia
dawa hizo ni zaidi ya watu laki 8.
Pia Serikali imeanzisha Mfuko wa
Udhamini wa Shughuli za Kudhibiti UKIMWI kwa ajili ya kusaidia kununua
dawa, kutoa elimu ya UKIMWI, kupima, kufanya tafiti na kutoa elimu ya
uzazi kwa vijana.
TACAIDS ilianzishwa kwa Sheria ya
Bunge Na. 22 ya mwaka 2001 kwa lengo la kutoa uongozi wa kimkakati,
uratibu na kuimarisha juhudi za wadau wote wanaojishughulisha na
kudhibiti UKIMWI nchini.
SHARE
No comments:
Post a Comment