TRA

TRA

Monday, September 18, 2017

Tuondoe silaha mikononi mwa raia

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !



Julian Msacky

VITA ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) na Vita ya Pili ya Dunia (1939-1945), vilipomalizika watu walishusha pumzi.

Walifanya hivyo kutokana na watu wengi kupoteza maisha, kujeruhiwa na uharibifu mkubwa wa mali.

Baada ya vita wengi waliamini matumizi ya silaha yatapungua, lakini hakuna nchi iliyofanya hivyo zaidi ya kuendelea kujikusanyia silaha.

Mashindano ya mataifa makubwa kuendelea kutengeneza silaha kali kali na makombora ya masafa mafupi na marefu yalizidi zaidi na zaidi.

Nchi ziliendelea kufanya hivyo licha ya uwepo mikataba ya kimataifa, lakini zimekuwa vichwa ngumu na kimsingi hali inazidi kuwa tete.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba athari za silaha zimebaki kwa raia pekee yao na kuonekana ndiye kiumbe anayewindwa nazo.

Ni kana kwamba zinatengenezwa ili kuendelea kukatisha maisha ya watu, wakiwemo wasio na hatia kama inavyotokea nchi nyingi hivi sasa. 

Hata hivyo, wanasayansi walipojifungia na kuanza kutengeneza silaha hawakujua kama zingeleta athari kubwa kama ilivyo leo. 

Mwanafizikia wa Sweden, Alfred Benhard alifurahi alipotengeneza silaha za milipuko akiamini zitasaidia kuleta amani duniani.

Pamoja na umaarufu aliyojipatia na mchango wake kwa maendeleo ya dunia, Benhard alionekana kama ‘muuaji’.

Hii ni kwa sababu mara baada ya ugunduzi alianza kulaaniwa kwa kubuni kifaa hicho kwa madai kuwa ametupa moto duniani.

Swali ni je, Benhard na wanafizikia wenzake wanastahili kulaumiwa kwa ubunifu huo au anatakiwa kushangiliwa?

Kwa hakika chombo alichobuni kimeleta madhara makubwa duniani kuliko faida. Dunia yetu ipo katika wakati mgumu.


Silaha zimeifanya dunia isiwe sehemu salama ya kuishi. Leo hii tunashuhudia mauaji ya kutisha yanayosababishwa na silaha.

Kinachotisha zaidi serikali nyingi zimeshindwa kudhibiti matumizi holela ya silaha na hivyo kutumbukia mikononi mwa raia ambao si wema.

Ni kawaida siku hizi kusikia huyu au yule ameuawa au kujeruhiwa kwa kupigwa risasi. Ilivyo sasa matumizi ya silaha yamekuwa ya kiholela mno. 

Hali hii ipo sehemu nyingi dunia. Marekani kuwa na silaha ni jambo la kawaida. Inakatisha tamaa. Kimsingi hali si nzuri si Marekani wala Tanzania.

Ilivyo sasa ni kwamba watu wakitofautiana badala ya kukaa kwenye meza ya mazungumzo, nguvu ya ziada inatumika ili awe na adabu. 

Siku hizi hata kwenye mikusanyiko watu wanakaa kwa wasiwasi maana lolote linaweza kutokea. Hakuna anayemwamini mwenzake. 

Tunaishi kama chui na mbuzi. Upendo unapungua. Amani inatupungia mkono. Silaha si suluhisho la kuleta amani hata kidogo. 

Ingekuwa hivyo leo Afghanstan, Nigeria, Somalia, Iraq, Syria na maeneo mengine yenye vita kungekuwa na amani, lakini hakuna.

Ni kweli kabisa kwamba mwanafizikia huyo ameleta moto duniani. Watu wanauawa ovyo na kujeruhi mithili ya wanyama pori. 

Kinachohuzunisha zaidi ni kuwa silaha hizi hawatengenezewi ndege pori. Ni kwa ajili ya kumwangamiza mwanadamu. 

Hivi mnakumbuka kijana mdogo wa miaka 29 nchini Marekani ambaye alifanya mauaji ya kutisha na kuitetemesha nchi hiyo?.

Huyu ni Omar Mateen aliyeua watu takriban 50 na kujeruhi wengine 53. Ilibidi Rais Obama kwa wakati huo aangue kilio kwa huzuni.

Rais Obama alisikitika kuona watu wanavyouana nchini humo. Siku za hivi karibuni kumekuwa na mauaji ya mara kwa mara nchini humo. 

Hali si nzuri. Nchi hiyo ilibidi ianze kupitia upya mfumo wa utoaji silaha. Ni baada ya kubaini madhara yake kwa wananchi.


Hapa kwetu tulihakiki silaha, lakini hali bado si nzuri maana matumizi yake yamekuwa ya holela holela na madhara yake yapo wazi.

Hakuna mwenye kujua ni lini viongozi wa dunia watakaa chini kuangalia namna kupiga marufuku matumizi ya silaha kwa raia wake.

Ninadhani ni muhimu kuondoa silaha mikononi mwa raia. Silaha zibaki mikononi mwa Serikali tu.  Tusiruhusu uuzaji wa silaha. 

Marekani imejikuta katika matatizo makubwa ya utumiaji wa silaha ovyo baada ya kutoa mwanya kwa raia wake kuwa nazo. 

Leo inahaha huku na kule ili iwe salama. Hata hapa kwetu tunahaha vivyo hivyo. Hii ni hatari kwa sababu madhara yake yanaonekana wazi.

Kwa msingi huo zikiondolewa mikononi mwa raia bila shaka tutaepuka mauaji ya mara kwa mara yanayotokea nchini kwetu na Afrika kwa ujumla. 

Tunafahamu silaha ni biashara, hivyo hata azimio ninalopendekeza halitaungwa mkono na wengi, lakini kwa hali ilivyo sasa lazima tuchukue hatua. 

Tuchukue hatua za kuiponya nchi yetu kwani tunakoelekea ni giza tupu. Tunasema hivi kwa sababu Afrika imeathiriwa mno na silaha. 

Afrika ndiko penye soko kubwa la silaha kwani ndiko penye migogoro mingi. Migogoro inasaidia watengenezaji waendelee kuvuna fedha. 

Kwa msingi huo Afrika ikatae kugeuzwa gulio au jalala la silaha kutoka China, Marekani, Urusi na Ufaransa. Tuwaambie hatutaki.

Tumeathirika vya kutosha. Tumeua watu wetu vya kutosha. Tumewajeruhi vya kutosha. Tubakiwe tu na silaha za kujilinda kama nchi.










Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger