
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali imewataka watumishi wa
Mikoa, Halmashauri na vituo vya kutolea huduma na kutoa taarifa za
mapato na matumizi kwa wakati kwa wananchi katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa wakati akizindua Mfumo
wa Kielektroniki wa Kuandaa Mipango, Bajeti na Ripoti za Mamlaka ya
Serikali za Mitaa (PlanRep) iliyoboreshwa na Mfumo Mpya wa Uhasibu na
Utoaji Taarifa (FFARS) jana mjini Dodoma.
“Ukamilishaji wa mifumo hii
utasaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji kwa watumshi hasa katika eneo la
mapokezi na matumzi ya fedha za umma kuanzia katika vituo vya kutolea
huduma mpaka ngazi ya Halmashauri”.
“Kuanzia sasa sitegemei kuona
kituo chochote cha kutolea huduma kilichopo chini ya Halmashauri
kinakuwa na matumizi yasiozingatia taratibu na kanuni za fedha au
kubadilisha matumizi ya fedha bila kuwasiliana na Mamlaka husika”
amesisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, alisema kuwa lengo la
matumizi ya mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi
katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali na zisitumike kukwamisha
shughuli na utaratibu wa kazi za Serikali.
Vilevile, Waziri Mkuu alisema kuwa
Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kipindi kirefu imekuwa ikitumia
gharama kubwa, muda mwingi katika kukamilisha zoezi zima la uandaaji wa
Mipango, Bajeti. Hivyo kupitia mfumo changamoto hizo zimetatuliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais-TAMISEMI George Simbachawene amesema kuwa kupitia mfumo
huo umeweza kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni nne gharama ya Serikali
zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya kufanya maandalizi ya
kuandaa bajeti.
“Mifumo hii itasaidia kutaleta
ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa huduma kwa wananchi,
utasaidia kupunguza muda na kuleta maendeleo kwa kasi na pia utasaidia
kutunza taarifa ya mapato yote katika ngazi ya Halmashauri” ameongeza
George Simbachawene.
Naye Kaimu Balozi wa Marekani
nchini Imni Patterson amesema kuwa pamoja mifumo hiyo itaongeza ufanisi
na kuboresha usimamizi wa fedha na kuwezesha Serikali ya Tanzania kutoa
fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na mahitaji ya wananchi kwa ufasaha.
“Marekani inajivunia kushirikiana
na Tanzania, mnapofanya kazi kwa malengo ya kuwa na Serikali yenye
uwazi, maendeleo endelevu na ustawi wa pamoja” amesema Kaimu Balozi wa
Marekani nchini.
Akitoa salamu, Mkurugenzi wa Mradi
wa PS3 Dkt. Emmanuel Malangalila amesmea kuwa mifumo hiyo imeundwa na
kutengenezwa na vijana wa Kitanzania kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI
wakishirikiana na watumishi wa mradi wa uimarishaji wa mifumo ya sekta
ya umma (PS3).
“Mifumo hii miwili itaimarisha
uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa matumizi ya fedha katika Halmshauri na
ngazi za vituo vya kutolea huduma na hivyo utoaji wa huduma kwa wananchi
kuboreka zaidi” amesema Dkt. Malangalila.
Mradi wa uimarishaji Mifumo ya
Sekta za Umma (PS3) ni mradi wa miaka mitano ulioanza Julai 2015 na
kumalizika 2020 na unafanya kazi katika Halmashauri 93 katika mikoa 13
Tanzania Bara ikiwa na lengo la kutoa msaada wa kitaalamu kwa Serikali
ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya Serikali katika ngazi ya
Taifa na Halmashauri ili kuboresha utoaji wa huduma za jamii.
SHARE
No comments:
Post a Comment