
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene
anawajulisha wazazi, walezi na wananchi wote kuwa Mitihani ya kumaliza
Elimu ya Msingi itafanyika tarehe 6-7/09/2017 kwa kuzingatia sheria,
Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Baraza la Mitihani Tanzania.
Kwa mwaka huu wa 2017 jumla ya
wanafunzi watakaofanya mitihani hiyo ni 917,030 kutoka katika shule za
Msingi 16,581 ambazo ni za Serikali na binafsi zilizoko Tanzania Bara.
Maandalizi ya uendeshaji na
usimamizi wa Mitihani hii umekwishakamilika katika ngazi zote ikiwa ni
pamoja na kusafirishwa kwa mitihani na wasimamizi kutoka ngazi ya
halmashauri kwenda kwenye vituo vya kufanyia mitihani na fedha kwa ajili
ya gharama za usimamizi na uendeshaji wa mitihani.
Gharama zitakazotumika hadi
kukamilika kwa zoezi la Mitihani ya darasa la saba ni Tsh Bil
29,474,964,600 na fedha hizo zitatumika kwa ajili ya uendeshaji na
usimamizi wa mitihani tu.
Waziri Simbachawene amewaagiza
Wakurugenzi wote Nchini kutumia Fedha hizo zilizopokelewa kwa ajili ya
mitihani kwa kufuata muongozo na kuhakikisha wanakamilisha mahitaji yote
na kuwalipa wasimamizi staili zao ili waweze kufanya kazi hii kwa moyo
na kwa uadilifu.
Aidha Waziri Simbachawene
amewatakia heri na baraka watahiniwa wote watakaoanza mitihani yao hapo
kesho na kuwataka kuwa watulivu katika kipindi chote cha Mitihani na
kufuata taratibu na maelekezo ya wasimamizi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais
Tamisemi.
SHARE
No comments:
Post a Comment