TRA

TRA

Latest

Tuesday, March 6, 2018

Watanzania wahimizwa kujiunga na mtandao wa mitaji

No comments:


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora amewataka wafanyabiashara nchini kuhamasika kujiunga na mtandao wa mitaji ya ubia ili kuimarisha vitega uchumi vyao na pia kusaidia kuanzisha viwanda hapa nchini.

Profesa Kamuzora alisema hayo wakati akizindua Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network jijini Dar es salaam jana.Aidha Katibu Mkuu huyo amesema uzinduzi wa mtandao huo umefanyika wakati mwafaka ambapo serikali ya awamu ya tano ipo katika mikakati ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda,

Aliwataka wananchi kuacha uoga katika ushiriki wa kuwawezesha kuwepo kwa mitaji ya kutosha kwa ajili ya uimarishaji wa uwekezaji nchini Tanzania.Alisema serikali kwa sasa inafanya kila linalowezekana kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa bora, ndio maana wameanzisha mchakato wa kutengeneza sera ya maendeleo ya viwanda hasa katika sekta binafsi.

Alisema ni vyema wenye viwanda na wananchi wengine kushiriki katika mchakato huo ili kufanikisha nia ya kuipeleka Tanzania katika nchi ya viwanda. Alisema kwa kuwa na sera sheria nyingi zitabadilika na hivyo kupunguza urasimu na pia vikwazo vya kuwezesha kazi katika masuala ya viwanda na biashara.

Pia alitaka wamiliki wa Ubia huo kushirikiana na Costech katika kuhakikisha kwamba viwanda vinaanzishwa na kuendelezwa.Alitaka kuwepo na elimu ya fedha na mitaji ili wananchi waweze kuthubutu na kufanikisha mitaji.

Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi amewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa uwazi, kwa kuzingatia sheria za nchi, na kuwa tayari kujifunza maarifa mapya kila fursa inapojitokeza.

Akisitikishwa na mahudhurio duni ya wafanyabiashara katika hafla hiyo alisema kutofahamu undani wa soko la mitaji na fursa zake kunatokana na kutokuwa wazi na kufanya biashara kwa kufuata kanuni.Akizungumzia kuhusu madai ya kuwapo kwa hali kuwa ngumu nchini Dr. Mengi pia amewataka Watanzania kuichukulia hali hiyo kama fursa ya kubuni biashara itakayowawezesha kupata faida kubwa.

Akiutambulisha Mtandao wa Tanzania Venture Capital kwa wadau, Muasisi wake Bw. Salum Awadh amesema Mtandao huo ni fursa kwa wawekezaji nchini kujipatia mitaji ya kuanzisha ama kuendeleza biashara zao kwa ubia kwa masharti rahisi.Alisema kwamba wakati umefika kwa Tanzania kusonga mbele kutumia fursa zilizopo duniani za mitaji na kusema jirani zetu wa Kenya wamesonga mbele katika hilo.

Alisema kwamba kutokana na kutojua umuhimu na ushiriki katika mitaji yenye ubia, wananchi wengi wanakimbilia katika mabenki ya biashara ambako pia wanapambana na vikwazo vingine.Alisema kwa kuwa na kampuni ya mitaji inayoweza kutafuta pia mtaji inayomilikiwa na wananchi wenyewe kupitia mitaji yao kutawezesha kuwapo na uimara wa viwanda na kuongeza idadi zake kwa kuwa mfumo wa fedha wa mitaji ni tofauti na kwenda benki.

Tanzania kwa sasa ina zaidi ya mabenki 50 ambayo yanajishughulisha na mambo mbalimbali yanayogusa biashara na hifadhi ya kawiada.Alisema mazingira ya sasa yanahitaji mfumo mwingine wa ziada kusaidia upatikanaji wa mitaji nje ya mabenki na kuzinduliwa kwa mtandao wa ubia wa mitaji kutasaidia kuziba pengo lililopo.

Kwa sasa Tanzania kwa rekodi zilizopo inapata asilimia 17 ya mitaji ya ubia ya dola bilioni 2.4 iliyopo duniani huku Kenya ikiwa na nfasi nzuri zaidi.Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi nchini-TPSF Bw. Godfrey Simbeye, baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali na wafanyabiashara mbalimbali.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi (kushoto), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora (katikati) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye (kulia) wakiwasili kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akifafanua jambo kabla ya kuanza kwa uzinduzi wa Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Wanaomsikiliza ni Muasisi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital, Bw. Salum Awadh (wa pili kushoto aliyesimama), Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi (wa pili kulia) pamoja Mkurugenzi wa Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda –TPSF, Edward Furaha (kulia).

Muasisi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital, Bw. Salum Awadh akitoa maelezo kuhusu Mtandao wa Tanzania Venture Capital kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora (kushoto) kabla ya kuelekea kwenye hafla ya uzinduzi wa mtandao huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye (wa pili kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi (kulia).
Muasisi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital, Bw. Salum Awadh akitoa neno la ukaribisho na kutambulisha mtandao huo ambapo amesema ni fursa kwa wawekezaji nchini kujipatia mitaji ya kuanzisha ama kuendeleza biashara zao kwa ubia kwa masharti rahisi wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mtandao huo ilyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi akitoa neno la ufunguzi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora kutoa hotuba ya uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora akitoa hotuba ya uzinduzi rasmi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital ambapo amesema umefanyika wakati mwafaka ambapo serikali ya awamu ya tano ipo katika mikakati ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda –TPSF, Bw. Edward Furaha na Aliyekuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mh. Abdullah Mwinyi wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
  

Pichani juu na chini ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi akisalimiana na kubadilishana mawazo na wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi akibadilisha na mawazo na Afisa Mtendaji Mkuu wa DOB Equity, Brigit van Dijk-van de Reijt wakati wa hafla ya uzinduzi wa wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora (wa tatu kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi nchini-TPSF Bw. Godfrey Simbeye (kushoto).
Tanzania Venture Capital Network-TVCN katika picha ya pamoja na mdau aliyewezesha kufanyika kwa uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

ALIYEKUWA DIWANI WA KATA YA GIHANDU AJIUZULU

No comments:

 

Na Jumbe Ismailly -HANANG . 


ALIYEKUWA diwani wa kata ya Gihandu,wilayani Hanang,Mkoani Manyara kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo,Mathayo Samuhenda amejiuzulu udiwani wa kata hiyo na kujiunga na Chama Chama Mapinduzi (CCM)

Akitangaza azma yake hiyo ya kujiuzulu katika nafasi yake ya udiwani wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Gihandu,Samuhenda alisisitiza kwamba aliamua kujiuzulu na kuwaacha wapiga kura wake siyo kwa njia ya ukatili bali alifikia maamuzi hayo kwa lengo la kuwaunganisha wananchi wote wa kata hiyo.  

Aidha alifafanua kwamba katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa wananchi wa kata hiyo wana matatizo ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kutokana na wanasiasa kutumia mtaji huo kuomba kura.
“Inatosha wanasiasa sisi tutumie shida ya maji ili tuoate kura tuondoke,inatosha..na watu wa Gihandu nawaomba sana hiyo ikiletwa kama sehemu ya mnada mzuri tu wa mtu kujinadi mkataeni inatosha tumeumia vya kutosha.”alisisitiza Samuhenda. 

Hata hivyo diwani huyo aliyejiuzulu aliweka bayana kwamba umefika wakati sasa kwa wanasiasa kubadili ajenda za kupatia kura za Gihandu na isiwe upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwani hiyo sasa imekuwa ni kejeli

Akimpokea diwani huyo,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara,Simon Lulu alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoendeleza makundi licha ya kuwa hivi sasa siyo wakati wa kumpeni na badala yake aliwataka kuvunja makundi hayo na kusisitiza juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisisitiza pia kwamba suala la kuvunja makundi siyo la hiyari bali ni la lazima kutokana na makundi hayo baadhi ya wanachama mchana wanakuwa CCM huku usiku wanatumikia Vyama vya upinzani.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang,Methew Darema alimpongeza diwani huyo kwa kitendo chake cha ujasiri cha kujiuzulu nafasi aliyokuwa nayo pamoja na kwamba ni hivi karibuni alitembelewa na kiongozi wake wa kitaifa kwa lengo la kuhamasisha watu kujiunga na chama hicho.

Kwa upande wake baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Gihandu,Stephano Ngudu alisema mwaka 2008 kila mwananchi alichangia shilingi 86,500/= kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari na Hosteli mbili,lakini mpaka leo hakuna ujenzi wowote wa majengo hayo uliokamilika na fedha walizochanga hawajarudishiwa.
 Ni Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,DK.Mary Nagu (wa kwanza kutoka kushoto) akimpongeza aliyekuwa diwani wa Kata ya Gihandu,Mathayo Semuhenda mara baada ya kutangaza azma yake ya kujiunga na CCM.
 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara,Simon Lulu akipokea kadi ya Chama Cha ACT Wazalebdo kutoka kwa aliyekuwa diwani wa kata ya Gihandu,Mathayo Semuhenda.
 Aliyekuwa diwani wa kata ya Gihandu kwa tiketi ya ACT Wazalendo,MATHAYO SEMUHENDA akipokea kadi ya CCM baada ya kutangaza azma yake ya kujiunga na CCM.
 baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) wa wilaya na Mkoa wa Manyara wakishiriki kikamilifu pamoja na wanachama wapya kula kiapo cha uadilifu baada ya kuwakabidhi kadi za chama wanachama wapya wa chama hicho.
Aliyekuwa diwani wa kata ya Gihandu,Mathayo Semuhenda akila kiapo cha uadilifu mara baada ya kukabidhiwa kadi ya chama cha mapinduzi(ccm)

Friday, March 2, 2018

Shirika la TTCL lazinduwa ‘Fiber Connect Bundle’

No comments:



Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba akizungumza katika uzinduzi huo.

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL CORPORATION) limezinduwa rasmi huduma mpya inayojulikana kama ‘Fiber Connect Bundle’ inayokwenda pamoja na kauli mbiu ya “Rudi nyumbani, kumenoga” kuchagiza uzinduzi huo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba alisema huduma hiyo ni mwendelezo wa ubunifu wa kampuni ya kizalendo katika kuwapatia Watanzania huduma za kipekee, nafuu na zenye ubora wa hali ya juu.
Bw. Kindamba alisema TTCL Corporation imedhamiria kuwafuata wateja nyumbani na kufanya mapinduzi makubwa ya kimawasiliano hasa ya mtandao wa intanenti yenye kasi ya juu.
Alisema kupitia huduma hiyo mpya ya Fiber Connect Bundle, wateja wao watapata huduma nne kwa pamoja zikiwa na unafuu mkubwa wa gharama na ubora wa hali ya juu ukilinganisha na mitandao mingine ya simu.
Bw. Kindamba amefafanua huduma kwa kuanzia wanatarajia kuzifikia nyumba 500 katika maeneo ya Mikocheni na nyumba nyingine 500 katika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam pamoja na nyumba 200 eneo la Medeli mkoani Dodoma.
Aidha aliongeza kuwa baada ya hapo wataendelea na maeneo mengine kwani lengo lao ni kuhakikisha kila mahali katika nchi yetu kunakuwa na huduma za mawasiliano ya Shirika hilo hasa kwa kuzingatia wao ndio wanaousimamia mkongo wa Taifa wa mawasilano.
Kindamba amesema kupitia kifurushi cha Fiber Connect, mteja wao atanufaika na huduma mbalimbali ikiwamo ya kupata intanenti yenye kasi isiyo na kikomo (Unlimited). Pia mteja atapata huduma ya simu za sauti kwa simu za mezani na simu card ambayo ataitumia kwenye simu yake ya mkononi na kupata huduma ya Intanenti sawa na simu ile anayopata katika simu ya mezani.
Ameongeza kuwa mteja wao pia atapata huduma za Wireless Service (WIFI) katika nyumba yake ambapo vifaa vyote vinavyotumia teknolojia ya intaneti vitaunganishwa ili kutumia kutumia huduma hiyo.
Ametoa mfano kuwa huduma ambayo wameizundua mteja anaweza kuunganisha kwenye Smart Tv, Tablets na kompyuta mpakato.Pia mteja atapatiwa vifaa vyote bure na uhakika wa huduma za baada (After Sell Services) endapo itahitajika.
Amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa ajili ya Watanzania ambao kimsingi shirika hilo ni mali yao na wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo.
“Tumeendelea kujipanga ili kufikia malengo yetu ambayo kimsingi ni kuwatumikia Watanzania kwa kiwango bora katika eneo la mawasiliano na kwa gharama nafuu,” amesema Bw. Kindamba.
Akizungumzia shirika hilo, Kindamba amesema, Februari moja mwaka 2018, Shirika la Mawasiliano Tanzania lilizaliwa kwa sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania Na. 12 mwaka 2017. Amesema kwa sasa shirika hilo limechukua sura ya iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania( TTCL), ambayo shughuli zake ziliisha Januari 31 mwaka 2018.
Amemshukuru Rais, Dk. John Magufuli kwa kuona umuhimu wa kuwa na Shirika madhubuti la mawasiliano la Taifa kwa maslahi mapana ya Taifa. Pia amemshukuru kwa kuendelea kuonesha imani kubwa kwa uongozi wao.

Benki ya NMB yazinduwa tawi jipya Wilaya ya Kigamboni

No comments:


 
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Bw. Hashim Mgandilwa (kushoto) pamoja na Mkurungezi Mtendaji
wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker (kulia) wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Tawi
jipya la Benki ya NMB Wilaya ya Kigamboni.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Bw. Hashim Mgandilwa (wa tatu kushoto) akikata utepe kuashiria
uzinduzi wa Tawi jipya la Benki ya NMB Wilaya ya Kigamboni. Wengine ni viongozi waandamizi
wa Benki hiyo na Mkurungezi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker (wa pili kulia).
Mkurungezi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker (kulia) akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo.

BENKI ya NMB imezinduwa tawi jipya la Benki hiyo eneo la Kigamboni ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma za kibenki kwa wateja na Wananchi kwa ujumla. Tawi hilo la kwanza kwa taasisi za fedha kuzinduliwa Wilaya ya Kigamboni, limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Bw. Hashim Mgandilwa.
Akizungumza atika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ms. Ineke Bussemaker alisema huo ni mwendelezo wa Benki ya NMB katika kusogeza huduma kwa wateja wake.
Alisema tawi hilo jipya la Kigamboni litarahisisha utoaji huduma za kibenki kwa wateja wetu hali ambayo itapunguza mzunguko wa wananchi kuzifuata huduma za kibenki. Aliongeza kuwa NMB imezingatia shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa Kigamboni kwa wafanyabiashara, wavuvi, wakulima, utalii wa ndani na kufungua tawi hilo hivyo wateja hawata lazimika kuvuka maji kwenda mjini kupata hudumaza kibenki kama zamani.
Bi. Bussemaker aliongeza kuwa kwa kutumia Fanikiwa Account, wafanyabiashara wanaweza kunufaika nanmikopo inayotolewa kuanzia shs 500,000 na kuendelea kukuza biashara zao. NMB tunakuwa pamoja na biashara yako kupitia Akaunti ya Fanikiwa.
Alisema NMB sio kwamba tu ni Benki kubwa nchini, bali inatoa mchango mkubwa katika shughuli za kijamii kwani inatenga takribani shilingi bilioni moja kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika jamii hasa kuinua elimu, afya.
“Huduma hii ya kibenki kutumia simu za wateja zinamwezesha mteja wetu kupata huduma saa 24 na siku saba za wiki kwa uhuru zaidi…tunawashauri wateja wetu kutembelea ATM zetu au matawi kwa ajili ya kujiunga na huduma ya NMB Mobile na kufurahia huduma hiyo kupitia namba *150*66#,”.
Kwa kuona umuhimu wa kusongeza huduma kwa wateja hasa maeneo ya vijijini Bdenki ya NMB inaendelea kuwawezesha mawakala watakaosaidia kutoa huduma hizo jambo ambalo litasaidia kusogeza hudumakwa wateja wetu.
Alisema hadi sasa Benki hiyo ina matawi 218 na zaidi ya mashine za kutolea fedha (ATM) 800 nchi nzima pamoja na vituo vya mawakala 947 wa jijini Dar es Salaam, kwa kufungua tawi hili NMB inakuwa benki ya kwanza kufungua Tawi Kigamboni.
Benki ya NMB imekuwa ikitoa kipaombele katika utoaji huduma kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha huduma kwa wateja wake pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za wateja hadi sasa NMB ina zaidiya wateja milioni1.5 wanaonufaika na huduma bora za kibenki kupitia simu za mkononi.

DC MATIRO AWARUDISHA KAZINI WATUMISHI WA AFYA

No comments:


Watumishi wa afya 22 katika hospitali ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga wamerudishwa kazini na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro mara baada ya kutumbuliwa na uongozi wa hospitali hiyo kutokana na kutoa malalamiko yao mbele  Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Athony Mavunde alipofanya ziara yake Februari 27,2018.


Watumishi hao walifukuzwa kazi siku moja baada ya ziara ya Naibu Waziri huyo kwenye hospitali hiyo ambayo aliifanya  Februari 27 mwaka huu mara baada ya kutoa malalamiko yao juu ya kunyanyaswa na hospitali hiyo ambapo kesho yake wale waliojifanya wazungumzaji 'kiherehere' wakatimuliwa kazi na kutolipwa stahiki zao zote.


Akiongea Machi 1, 2018 na uongozi wa hospitalini hapo mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro alisema mara baada ya kupewa taarifa hizo juu ya watumishi hao kuwa wametimuliwa kazi baada ya kusema ukweli kwenye ziara ya Naibu Waziri huyo, jambo hilo limemkera na kuamua kufika kwenye hospitali hiyo kuwarudisha kazini.

“Kuanzia sasa watumishi wote mliowafukuza kazi wanarudi kazini na ninatoa siku 14 wawe wameshalipwa haki zao zote wanazodai, ikiwamo malimbikizo ya mishahara, makato ya NSSF,TUGHE, pamoja na kulipwa mishahara kiwango cha serikali, na msipofanya hivyo ndani ya siku hizo tutawachukulia hatua,”alisema.
"Kwanza hospitali hii mmeidharau serikali kwa sababu haiwezekani kiongozi mkubwa kama yule Naibu waziri anafanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za watumishi, halafu ninyi kesho yake mnawafukuza kazi, huo ni utovu wa nidhamu”,alisema Matiro.
Naye mmoja wa watumishi hao walifukuzwa kazi Elizabeth Zabron alisema baada ya kutoa malalamiko yao juu ya kunyanyaswa kwenye mishahara na madai mbalimbali, muda mfupi tu baada ya kuondoka Naibu Waziri huyo wakaona majina ya watu 22 yakiwa yamebandikwa kwenye ubao wa matangazo wakiitwa kesho kuonana na uongozi wa hospitali hiyo.
Alisema baada ya kwenda kuonana na uongozi huo wakajua tayari kilio chao kimesikika cha kulipwa mishahara na madai yao, ambapo wakashangaa wanaambiwa kuwa wamefukuzwa kazi na wanatakiwa kusaini barua hizo bila ya kuzisoma, ndipo wakagoma na kuamua kwenda kushitaki kwa mkuu huyo wa wilaya ili wapate haki zao.
Barua hizo kwa ndani zilikuwa zimeandikwa kuwa "unafukuzwa kazi na hutakiwa kulipwa haki yako yoyote na kutakiwa kuondoka eneo la kazi mara moja".
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt .Maganga Dohoi alikiri kuwafukuza kazi watumishi hao na kudai kuwa bodi ya hospitali hiyo ilikaa na kuagiza watumishi wote wasio na sifa ya kuwa na vyeti vya kidato cha nne lakini wana taaluma ya uuguzi wafukuzwe kazi, ndipo naye akafuata maagizo hayo.
Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa Bodi ya hospitali hiyo Magezi Magedi ambaye pia ni ofisa utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga, alikana kukifahamu kikao cha kufukuza watumishi hao , na kudai kama suala la kufukuza kazi kuna taratibu zake zinatakiwa kufuatwa na siyo kuwafukuza hovyo hovyo. 
Alisema  hospitali hiyo isitumie kivuli cha serikali kufukuza watumishi hao ikiwa suala la vyeti vya darasa la Saba lilikuwa la watumishi tu wa serikali.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na watumishi wa afya katika hospitali ya Kolandoto waliotimuliwa kazi.-Picha na Marco Maduhu - Shinyanga News blog & Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akionyesha masikitiko namna walivyotendewa ndivyo sivyo watumishi hao wa afya katika hospitali ya Kolandoto kwa kutimuliwa kazi kisa wametoa malalamiko yao mbele ya Naibu waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Anthony Mavunde.
Mmoja wa watumishi waliofukuzwa kazi Elizabeth Zabroni akielezea kisa cha kufukuzwa kazi
Emmanuel Makungu naye alidai wamekuwa wakilipwa mishahara lakini hawapewi Salary Slip wala kusaini popote na kutokujua umeingia mshahara wa mwezi gani na pia michango ya NSSF wamekuwa wakiambiwa imeingizwa lakini wakifuatilia hakuna pesa yoyote iliyowekwa pamoja na fedha za likizo kutopewa, na kubainisha kuwa walipotoa malalamiko yao mbele ya Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Antony Mavunde iliwapate haki zao wakaonekana kuwa kikwazo na kutimuliwa kazi.
Sara Mkem akionyesha kusikitishwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa kuwafukuza kazi kisa wametoa matatizo yao mbele ya Naibu Waziri huyo ili yapate ufumbuzi, na kuonekana kuwa kero na kutimuliwa kazi, bila hata ya kujali utu wao pamoja na kulazimishwa kusaini barua bila ya kuzisoma  na kudai uongozi huo una roho ya kinyama kwani huenda ina dhamira ya kutaka arudi uraiani akauawe na watu wabaya kwa kumkata viungo vyake.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt Maganga Dohoi akijitetea kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Baadhi ya watumishi waliofukuzwa kazi na uongozi wa hospitali ya Kolandoto wakiwa kwenye kikao na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na uongozi wa hospitali hiyo kutatua suala lao la kufukuzwa kazi mara baada ya kutoa kilio chao kwa Naibu Waziri wa Kazi,Ajira na Vijana Antony Mavunde juu ya manyanyaso wanaoyapata .
Watumishi wa afya waliofukuzwa kazi katika hospitali ya Kolandoto wakiwa kwenye kikao cha kutatuliwa matatizo yao na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro mara baada ya kumpelekea matatizo yaliyowakumba ya kutimuliwa kazi kinyemela bila ya kufuata sheria za kazi.
Kikao kikiendelea.
Watumishi wa afya katika hospitali ya kolandoto waliofukuzwa kazi kenyemela wakiwa wameshika bango la kutaka haki yao
 Ofisa utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,Magezi Magedi ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya hospitali hiyo ya Kolandoto akikana kukifahamu kikao cha kufukuza kazi watumishi hao na wala tangu achaguliwe kuwa mjumbe wa bodi hiyo hajawahi kuitwa hata kikao kimoja  na kudai kama suala la kufukuza kazi watumishi hao kuna taratibu zake zinatakiwa kufuatwa, na siyo kuwafukuza hovyo hovyo na kuwalazimisha kusaini barua bila ya kuzisoma. 
 Ofisa kazi mkoa wa Shinyanga Revocatus Mabula alisema taratibu za kuwafukuza kazi watumishi hao zilikiukwa ambapo hawakupewa notes na walistahili kupewa haki zao zote ndani ya siku 14,kulipwa kiinua mgongo,malimbikizo ya likizo zao zote pamoja na kusafirishwa mahali walipotoka makwao na siyo kuambiwa tu wamefukuzwa kazi na hawatolipwa pesa yoyote.
Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi TUGHE, Tabu Mambo alisema hawajahi kuona mchango wowote wa watumishi hao waliofukuzwa kazi licha ya kuambiwa kuwa wanalipiwa na kubainisha kuwa walipokuwa wakifika kuzungumza na watumishi hao walikuwa wakikosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wao, na wale watumishi ambao walioonekana kuwa wanajua kuongea ndiyo kidogo walikuwa wakitolewa michango hiyo.
Picha na Marco Maduhu - Shinyanga News blog & Malunde1 blog

SERIKALI IMETENGA SHILINGI BILIONI 11.4 KUBORESHA WAKALA WA NDEGE ZAKE

No comments:


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiongea na wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo jijini Dar es Salaam. Anayemsikiliza ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Bwana Tito Kasambala
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bwana Richard Mayongela (kushoto) akimkaribisha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua Wakala wa Ndege za Serikali
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akipanda kukagua mojawapo ya ndege za Wakala wa Ndege za Serikali inayosafirisha viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali wakati wa ziara yake kwa Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam
Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali Mhandisi Bernard Mayila akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akifanya ukaguzi ndani ya ndege mojawapo inayosafirisha viongozi wa ngazi za juu wa Serikali wakati wa ziara yake alipotembelea Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiteremka baada ya kukagua mojawapo ya ndege za Wakala wa Ndege za Serikali wakati wa ziara yake kwenye Wakala hiyo kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam

……………….

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuboresha Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambayo inasimamia na kuendesha ndege ambazo zinasafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea na kukagua utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Ndege za Serikali ambayo inasimamia na kuendesha ndege ambazo zinasafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali ambapo alizungumza na Menejimenti na wafanyakazi na kuwaeleza kuwa Serikali imejipanga kuboresha Wakala hiyo

Mhandisi Nditiye alisema kuwa azma ya Serikali ya Awamo ya Tano inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa Taasisi za Serikali zinafanya kazi zake kwa weledi na uadilifu ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananchi. “Serikali inatambua umuhimu wa Wakala hii na ina imani kubwa nanyi katika kuhakikisha kuwa mnafanya kazi zenu za kusafirisha viongozi kwa usalama na kwa uhakika ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi na tayari ina nia ya kuboresha taasisi hii”, amesema Mhandisi Nditiye.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TGFA Bwana Tito Kasambala amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa taasisi yake ina ndege nne ambazo zinatumika kusafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali katika kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia watanzania na tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 11.4 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa ajili ya shughuli mbali mbali za Wakala ikiwemo matengenezo ya ndege, mafunzo kwa wanahewa na ukarabati wa karakana.

Mhandisi Nditiye amewaeleza wajumbe wa Menejimenti na wafanyakazi wa Wakala hiyo kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao na umuhimu wa wahandisi wa ndege na marubani wa kupata nafasi ya kuendesha ndege na kozi za mafunzo mbali mbali kuendana na taaluma zao ambapo tayari makubaliano yamefanyika baina ya Wizara na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ya kuwapatia nafasi marubani wa ndege za Wakala wa Ndege za Serikali nafasi ya kurusha ndege mara kwa mara ili kuendana na matakwa ya taaluma zao.

Ameongeza kuwa Serikali inashughulikia suala la miundo ya watumishi wa umma ambapo Wakala wa Ndege za Serikali ni mojawapo ya taasisi ambayo muundo wake unafanyiwa kazi ili kuweza kuzingatia taaluma, kada za watumishi na maslahi yao. “Natumaini wote mnatambua na kuelewa kuwa kipindi cha hapo nyuma kidogo utumishi wa umma uliingiwa na baadhi ya watu wachache ambao walikuwa wanafanya ujanja ujanja na kuharibu utumishi wa umma ambapo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu, imelifanyia kazi jambo hili na ameunda bodi maalumu ambayo inafanyia kazi suala la muundo, kada na maslahi ya watumishi wa umma,” amesema Mhandisi Nditiye.

Aidha, wafanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali wamemuomba Mhandisi Nditiye kuwasilisha ombi lao kwa Serikali la kuwaongezea mishahara yao kuendana na hali ya soko la ajira ya marubani ilivyo nchini kwa sasa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

TGNP Mtandao wakutanisha madiwani 20 kujadili kushirikiana

No comments:


Zaidi ya madiwani 20, kutoka mikoa mitano na wilaya Nane wamekutana jijini Dar Es Salaam, kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao.

Madiwani hao ni kutoka Halmashauri za wilaya za Kishapu (Shinyanga), Tarime (Mara), Mbeya (Mbeya), Morogoro Vijijini (Morogoro) na manispaa za Ilala, Kinondoni na Ubungo (Dar es salaam).

Madiwani hao ambao walikutana katika ofisi za TGNP Mtandao, zilizopo Mabibo Dar Es Salaam, pia walipata nafasi ya kutembelea Kipunguni na kujionea mradi unaotekelezwa katika eneo hilo.

Pamoja na kujifunza masuala mbalimbali, Madiwani hao walipata fursa ya kushirikisha masuala ya kijinsia ambayo bajeti za Halmashauri zao zimezingatia na jinsi walivyofanikiwa kutenga rasilimali za kuhakikisha bajeti zao zinakidhi mahitaji ya kijinsia.

Wakiwa kata ya Kipunguni iliyopo manispaa ya Ilala madiwani hao walikutana na Diwani wa Kata hiyo na kujifunza jinsi ambavyo wananchi waliopo katika Kituo cha Taarifa na Maarifa walivyofanikiwa kuleta maendeleo kwa kushirikiana na viongozi ikiwepo kupambana na ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji.Eneo hilo maarufu kwa wakazi wa kutoka mikoa ya kaskazini ambako yapo makabila yanayofanya ukeketaji nalo limekumbwa na tatizo hilo.

Aidha katika ziara hiyo, waheshimiwa madiwani walipata nafasi ya kujifunza, faida za mabunge ya jamii, na kujifunza miradi ya maendeleo ya kuwezesha wananchi kiuchumi ambayo inatekelezwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na wananchi wa Kipunguni.

Katika mabadilishano ya uelewa mmoja wa wajumbe ambaye ni Diwani wa Ijombe wilayani Mbeya, Stimar Hepa John alisema kwamba wakati umefika kwa wananchi wengi kutambua shughuli za TGNP Mtandao.

Alisema awali alikuwa akidhani kwamba asasi hiyo ina mlengo wa kisiasa kiasi cha kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwao lakini baada ya elimu hii amebadili uelekeo na kuitaka taasisi hiyo kupeleka elimu Tanzania nzima.

Alisema, "Anaona kwamba TGNP ina jukumu kubwa nchini Tanzania na hivyo inastahili kuwa kila mahali kuwasaidia watanzania kujiimarisha katika nyanja zote."Diwani huyo wa Ijombe ambaye pia ni Mkuu wa shule ya sekondari Igawii alisema pamoja na kubadili mwelekeo aliwataka wabunge kuona kwamba wanapoandaa miradi hawaandai mbunge mpya bali kusaidia wananchi kujiinua kiuchumi.

Katika mkutano huo walitoa maazimio kadhaa ya kufanyiwa kazi katika halmashauri.Miongoni mwa maazimio hayo ni namna ya kusimamia Mfuko wa Maendeleo wa wanawake kuhusu ile asilimia 5 na kutekeleza dhana ya viwanda.

Kwa mujibu wa Ofisa Programu uchechemuzi wa TGNP Mtandao, Deo Temba mambo mengine waliyokubaliana ni kushawishi na kufuatilia ongezeko kila zahanati na vifaa vya kujifungulia na kuhimiza uwekaji wa mikakati ya kupambana na ukatili wa jinsia na kuunda kamati za ulinzi za mtoto.

Pia imeelezwa haja ya TGNP Mtandao kuendelea kutoa elimu kwa kusaidiwa na mabaraza ya halmashauri kuhusu rasilimali fedha na kufuatilia uwekezaji katika ujenzi wa hosteli kupunguza umbali wa watoto wa kike kutembea kufuata shule.Mambo mengine ni kuona kwamba uandaazi wa bajeti unaanzia ngazi ya kijiji au mtaa badala ya kata na kukosekana kwa sauti za wananchi katika bajeti.

TGNP Mtandao ni asasi ya kiraia inayo fanya kazi na wanajamii kwa kipindi cha miaka 25 sasa, kwa kipindi chote hicho kimeshirikiana na taasisi za serikali, Wizara, Halmashauri na Kamati za Bunge za kisekta kwa ajili ya majadiliano, mashauriano na mafunzo ya namna ya kuboresha huduma za jamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

 Ofisa Programu uchechemuzi wa TGNP Mtandao, Deo Temba akifafanua jambo wakati akiendesha mjadala kwa Madiwani 20 kutoka mikoa 5 na wilaya 8 walioshiriki mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam.  Diwani wa Kata ya Songwa wilayani Kishapu, Shinyanga, Ngoromole Abdul akibadilishana uzoefu na madiwani wenzake wakati wa mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam. Diwani wa Ijombe wilayani Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa shule ya sekondari Igawii, Stimar Hepa John akichangia kwenye mjadala wakati wa mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam.Diwani wa Kata ya Mshewe ya Wilaya ya Mbeya vijijini, mkoani Mbeya, Esther Mbega akishiriki kwenye mjadala wakati wa mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam. Diwani wa Kata ya Ukenyenge ya wilaya Kishapu mkoani Shinyanga, Anderson Mandia akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam. Pichani juu na chini ni washiriki wakiendelea kujadiliana wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam. Sehemu ya Madiwani 20 kutoka mikoa 5 na wilaya 8 walioshiriki mkutano wa kubadilishana uzoefu na kujifunza jinsi ya kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo katika kata zao uliondaliwa na TGNP Mtandao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo jijini Dar es Salaam.
 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger