Katibu
Mkuu wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, wazee na watoto,
Dkt. Ulisubisya Mpoki akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo kuhusiana na Siku ya saratani, huadhimishwa duniani kote kila
mwaka ifikapo tarehe 4 ya Mwezi februari.
Kaulimbiu
ya Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani mwaka huu ni ‘TUNAWEZA,
NINAWEZA. KWA PAMOJA TUWAJIBIKE KUPUNGUZA JANGA LA SARATANI DUNIANI.”
(We can, I can. How everyone, as a collective or as an individual can do
their part to reduce the global burden of cancer).
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ocean Road, Julius Mwaiselage
akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
kuhusiana na huduma za matibabu zinazotolewa na Taasisi ya Ocean Road.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, wazee na watoto, Dkt. Ulisubisya Mpoki leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Avila Kakingo wa Globu ya Jamii.
Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii
WIZARA
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana
na Taasisi ya Ocean Road pamoja na wadau mbalimbali kuadhimisha siku ya
Saratani kuanzia kesho kwa kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na
kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na maradhi ya Saratani ambayo
hufanyika kila Februali 4 ya kila mwaka .
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Dk. Ulisubisya Mpoki amesema kuwa Saratani ni ugonjwa ambao
unaathiri watu wa rika na jinsia zote; watoto, watu wazima, wake kwa
waume.
Amesema
takwimu za Shirika la Kimataifa la Atomiki la Utafiti wa Saratani
(IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaelezea kwamba kila mwaka
duniani kunatokea wagonjwa wapya wa saratani wanaokadiriwa kufikia
milioni 14.1, kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 8.2 hufariki dunia
kutokana na ugonjwa wa Saratani, hii husababishwa kwa wagonjwa kuchelewa
kufikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Vifo vya ugonjwa wa
Saratani ni asilimia 13 ya vifo vyote vinavyotokea duniani (WHO).
Kaulimbiu
ya Maadhimisho ya Siku ya Saratani duniani mwaka huu ni ‘‘Tunaweza ,
Ninaweza.Kwa pamoja tuwajibike kupunguza janga la saratani duniani’’.
Dk.Mpoki
amesema kuwa hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba
stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la Saratani litaongezeka na
kufikia makadirio ya wagonjwa wapya milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku
ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea ikiwemo
Tanzania.
Amesema
tatizo la Saratani limekuwa likiongezeka na kukua, kila mwaka,
Takribani wagonjwa wapya wapatao 44,000 hugundulika na saratani za aina
mbalimbali nchini, hii ni sawa asilimia 10 tu (4,400) kati ya wagonjwa
wote wanaofanikiwa kufika katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ili
kuweza kupata tiba. Kati ya hao wanaobahatika kufika katika Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road (takribani asilimia 80) hufika wakiwa katika
hatua za mwisho za ugonjwa (Hatua ya 3 na ya 4), hali ambayo hupunguza
uwezekano wa wagonjwa kuweza kupona maradhi hayo.
Dk.Mpoki
kwa mujibu wa taarifa kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road hapa
nchini zinaonyesha kwamba aina za Saratani zinaoongoza ni kama
ifuatavyo:
Kwa
upande wa wanaume,Saratani ya Ngozi ,Saratani ya Koo, Saratani ya Tezi
Dume, pamoja na Saratani ya Tezi,na wanawake ni Saratani ya Shingo ya
Kizazi, Saratani ya Ngozi, Saratani ya Matiti, pamoja na Saratani ya
Koo.
Amesema
ugonjwa wa Saratani umekuwa na vyanzo mbalimbali vinavyosababisha
tatizo hili kukua kwa kasi hapa nchini na Duniani ambayo yamegawanyika
katika sehemu tatu ambazo Virusi vinavyosababusha Saratani ya Shingo ya
Kizazi, Bakteria vinavyosababusha Saratani ya Tumbo, Parasaiti vimelea
vya kichocho vinavyosababisha Saratani ya Kibofu cha mkojo.
Aidha
amesema mtindo wa kimaisha wa Uvutaji wa sigara, kula vyakula ambavyo
si mlo kamili na vyenye mafuta kwa wingi, kutokula matunda na mboga
mboga, kunywa pombe kupita kiasi, matumizi ya dawa za kulevya na
kutokufanya mazoezi,Mionzi ya Miale ya jua ambayo inaathiri ngozi hasa
kwa walemavu wa ngozi,Urithi katika familia kwa mfano Saratani ya
Matiti, na Utumbo.
Amesema
Saratani ni ugonjwa ambao huweza kuchukua muda mrefu mpaka kujitokeza
(Miaka 10-20), hivyo wakati mwingine inakuwa ni vigumu sana kujua chanzo
cha Saratani pale inapokuwa imejificha.
Dk.Mpoki
amesema mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa haya yasiyo ya
kuambukiza ikiwa ni pamoja na saratani ni ulaji usiofaa mafuta na
sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa
sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, na unywaji pombe kupita kiasi.
Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto
inatumia maadhimisho haya kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama
ilivyo kwenye nchi zote duniani. Aidha,Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
inahamisisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuanzi Februali 3 mpaka 4
ili kufanyiwa uchunguzi Saratani zifuatazo, Uchunguzi wa Saratani ya
Tezi Dume , Saratani ya Shingo ya Kizazi, Saratani ya Matiti na saratani
ya ngozi kwa walemavu wa Ngozi. Uchunguzi huu utafanyika bure bila ya
malipo yoyote.
‘‘Mwanzoni,
wengi wetu hawajitambui ya kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na
dalili lakini hawachukui hatua mapema. Dalili kubwa ya ugonjwa wa
Saratani ni uvimbe,ambao hauna maumivu mwanzoni, kupungua uzito,
upungufu wa damu mwilini na dalili zingine kwa aina ya Saratani na
sehemu ilipo mwilini’’.amesema Mpoki.
SHARE
No comments:
Post a Comment