Mratibu
wa kitaifa wa Mradi wa CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo akizungumza
machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu
Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda (hayupo pichani) kufungua
rasmi mafunzo ya Tehama kwa walimu nchini.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
MAFUNZO
kwa walimu watakaotumia teknolojia ya mawasiliano na habari (Tehama)
kufundisha masomo ya sayansi ikiwamo hesabu yamefunguliwa katika maabara
za Chuo Kikuu Huria jijini Dar es salaam.
Mafunzo
hayo yanayohusisha walimu kutoka Vyuo vya Monduli, Tabora na Morogoro
yamelenga kuoanisha ufundishaji na matumizi ya Tehama katika program ya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya
kuboresha elimu Tanzania kupitia ufadhili wa taifa la China.
Programu
hiyo inayotoa ushirikiano mpya kati ya China na shirika hilo la Umoja
wa Mataifa inafanyakazi katika mataifa manane ya kusini mwa jangwa la
sahara inatekelezwa kwa lengo la kuwezesha mafanikio kwa malengo ya
2030.Nchi zinaozhusika na mpango huo ni Tanzania Kongo ya Kinshasa
(DRC), Congo, Liberia, Uganda, Côte d’Ivoire, Ethiopia na Namibia.
Mpango
huo ambao kwa ujumla wake , awamu ya kwanza na ya pili unachukua miaka
minne umelenga kuwezesha vyuo vya walimu kutoa walimu wa kufunza wenzao
kwenye stadi za kufundisha kwa kutumia Tehama.
Mradi
huo unaojulikana kama UNESCO-China Funds-in-Trust (CFIT) wenye lengo la
kuziba pengo la ubora wa elimu wa kuwawezesha walimu kufundisha kwa
kutumia Tehama ulizinduliwa Novemba 22,2012 kwa nchi tatu za kwanza na
baadae kuongezwa nchi nyingine tano kufikia nane mwaka 2013.Mpango huo
ni wa dola za Marekani milioni 8 kutoka China mahususi kwa mataifa ya
Afrika kuboresha elimu kupitia Unesco.
Makamu
wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda
akifungua mafunzo ya wiki mbili kwa walimu watakaotumia teknolojia ya
mawasiliano na habari (Tehama) kufundisha masomo ya sayansi ikiwamo
hesabu yanayoendelea katika maabara za Chuo Kikuu Huria (out) jijini Dar
es salaam. Walioketi
kutoka kushoto ni Basiliana Caroli Mrimi kutoka Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa
CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo pamoja na Kiongozi wa kitaifa wa timu
ya mradi wa CFIT kit, Prof. Ralph Masenge.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku 10 katika Chuo Kikuu Huria,
Mtaalamu wa program za elimu kutoka makao makuu ya Shirika la Unesco
mjini Paris, Ufaransa, Gabriel El Khili alisema kwamba program hiyo
imelenga kutatua chnagamoto zinazokabili elimu ili elimu iwe
ileinayotakiwa kuwezesha maendeleo ya kasi katika sayansi.
Alisema
ni lengo la Unesco kupitia ufadhili huo kuhakikisha kwamba kunapatikana
walimu bora watakaowezesha matumizi ya Tehama katika kufundisha masomo
ya sayansi ikiwamo hesabu ili kutengeneza wataalamu wa baadae katika
taifa hili.
Alisema
kuna pengo kubwa kuhusiana na ubora wa elimu na kwamba baada ya
kumaliza program ya elimu kwa wote mwaka jana nguvu sasa inastahili
kuelekezwa katika ubora wa elimu ili kufikia malengo ya 2030. Alisema
changamoto kubwa ni kuleta karibu matumizi ya digitali kwa kuzingatia
ukweli wa sasa kwamba matumizi yake ni madogo ukizingatia na haja kubwa
inayoambatana na haja ya kuwa na elimu bora.Alisema ni vyema kuiga mfano
wa China kwamba kuna tatizo la kidunia la kielimu lakini linalohitaji
suluhu ya eneo la husika kwa kuzingatia rasilimali zilizopo eneo hilo.
Mtaalamu
wa program za elimu kutoka makao makuu ya Shirika la Unesco mjini
Paris, Ufaransa, Gabriel El Khili (kulia) akizungumzia madhumuni ya
programu hiyo inayoratibiwa na UNESCO wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
ya wiki mbili kwa walimu yanayoendelea katika maabara ya Tehama Chuo
Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
Alisema
mapinduzi ya kitamaduni ya China baada ya kujikomboa yalizingatia elimu
na kwa kutumia rasilimali za nyumbani waliweza kusonga mbele na nia yao
ya sasa ni kufikiri shida ya elimu na maendeleo kimataifa lakini kupata
suluhu ya tatizo hilo kwa nchi husika kwa kuhakikisha rasilimali
zilizopo zinatumika kuboresha elimu.
Anasema
mafunzo kwa Tehama maana yake kusambaza elimu bora kwa kutumia nyenzo
za Tehama zilizopo kuanzia redio televisheni, CD na kadhalika.Alisema ni
matumzi ya Unesco kwamba mafunzo yanayotolewa yatasaidia kuboresha
elimu ya walimu na wanafunzi wao kwa kutumia Tehama, matumizi yake
yaliyotukuka ambayo yatasaidia kuimarisha na kutoa ubora wa elimu pamoja
na kuwa na walimu wachache.
Naye
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda
akifungua mafunzo hayo aliwataka walimu hao kutambua umuhimu wao katika
kusukuma mbele lengo la mafunzo hayo na wala si kujipatia cheti cha mahudhurio.
Kiongozi
wa kitaifa wa timu ya mradi wa CFIT kit, Prof. Ralph Masenge
akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo katika hafla fupi ya
ufunguzi.
Alisema
ulimwengu wa sasa ni wa walimu kutoa mwongozo wa namna ya kujifunza kwa
kumuelekeza mwanafunzi kwa kuwa ulimwengu wa digitali umerahisisha
mambo mengi.
Alisema
wasishangae wakigundua kwamba wanafunzi wao ni weledi zaidi kuliko wao
ila wasaidie kuhakikisha kwamba Tehama inatoa nafasi ya wanafunzi wengi
kujifunza na kupata elimu wanayohitaji katika kubadili maisha na uchumi
katika jamii.
Alisema
kwamba ni matumaini yake kwamba kwa mafunzo hayo elimu ya Tanzania
itapaa hasa kutokana na ukweli kuwa China imesema wazi kuwa haitapenda
Tanzania kushindwa katika mradi huu wa kuleta maboresho makubwa katika
elimu ya Tanzania ili iweze kutumika kutengeneza maarifa.
Profesa
Bisanda alisema kwamba kwa sasa Tanzania ina shida kubwa katika masomo
ya sayansi (bayolijia,kemia na fizikia ) pamoja na hesabu na kwamba
uwapo wa program hiyo kutasaidia kufikisha mafunzo kwa wanafunzi kwa
namna bora na yenye uhakika zaidi hata kama walimu wapo wachache.
Pichani
juu na chini walimu kutoka Vyuo vya Monduli, Tabora na Morogoro
wakishiriki mafunzo ya matumizi ya Tehama kwa vitendo katika program ya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya
kuboresha elimu Tanzania kupitia ufadhili wa taifa la China.
Alisema
ni vyema walimu wakajifunza namna ya kufanya na kutafuta majawabu ya
matatizo kwa kutumia tehama na kuambukiza mwenendo huo kwa wenzao na kwa
wanafunzi.
Alisema
ni kweli kuwa Tanzania ipo gizani katika ICT kutokana na matumizi yake
madogo na hivyo walimu wakielewa na kuwafunza wengine taifa hili
litaondoka katika giza hilo na kupata mapinduzi makubwa ya fikira na
elimu.Aidha alisema kwa kutumia ICT wanaweza kupunguza gharama za
uendeshaji na uzalishaji hasa katika masomo na mafunzo.
Alitolea
mfano kwamba kama wakipata softwea ya mitihani ambayo ipo wanaweza
kuokoa zaidi ya shilingi milioni 700 wanazotumia kwa ajili ya mitihani
na michakato yake.
“Fikiria
unaweka program ambayo mwanafunzi anafanya mitihani moja kwa moja na
hii inawezekana, utafanya nini na fedha hizo ambazo unazitumia sasa kwa
ajili ya uandazi wa mitihani kuifanya na kuisahihisha” aliuliza na
kusema kwamba zingelisaidia vitu vingine.
Alisema
kihistoria walikuwa wanakazi kubwa ya kuandaa mitihani na kusambaza
lakini mwanzo wa kuwafanya wanafunzi wajieleze kama wanataka kufanya
mitihani kwa kutumia Tehama sasa wanatengeneza mitihani kwa kadiri ya
maombi na kupunguza gharama.
Picha ya pamoja ya wakufunzi na washiriki.
Makamu
wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda
(kushoto), Mtaalamu wa program za elimu kutoka makao makuu ya Shirika la
Unesco mjini Paris, Ufaransa, Gabriel El Khili (katikati) pamoja na Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo (kulia) mara baada ya zoezi la picha ya pamoja.
SHARE
No comments:
Post a Comment