Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitembelea Shule ya Sekondari Lindi baada ya shule hiyo kuteketea kwa moto hivi karibuni.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na
heater za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya
moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.
“Kuna
tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa
vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari kwani
linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi
kutumia vifaa hivyo,” alisema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 17, 2016) katika harambee ya
kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi
yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.
Katika
ajali hiyo shule imeathirika kwa asilimia 34 ambapo vyumba tisa vya
madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na
fizikia yameungua na kusababishia hasara ya sh. milioni 682.78.
Waziri
Mkuu amesema kwa namna ambavyo majengo hayo yameungua ni vema yakavunjwa
na kujengwa upya ambapo aliwataka kutumia nafasi hiyo kwa kujenga jengo
la ghorofa ili kutumia eneo dogo kwa kujenga madarasa mengi.
Pia
alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kuhakikisha fedha
zitakazopatikana katika harambee hiyo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Harambee
ilihudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa, mke wa Rais mstaafu
wa awamu ya nne, mama Salma Kikwete, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima
Dendego pamoja na wadau wa maendeleo na wanafunzi waliosoma shule hiyo
akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu amezitaka taasisi mbalimbali nchini kufunga
vifaa vya kuzimia moto katika majengo yao kwa ajili ya kuvitumia pindi
ajali za moto zinapotokea.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment