
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema hakina mpango wa kufanya mazungumzo
au makubaliano na Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na suala la
Uchaguzi uliopita.
Msimamo
huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF
Ismail Jussa Ladhu katika Mahojiano Maalum na Gazeti moja hapa nchini
Juzi.
Alisema
Uchaguzi umekwisha kazi iliyokuwepo mbele ya CCM ni kusimamia
utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya mwaka 2015/2020 ili kuhakikisha
ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mkuu na viongozi wa CCM
zinatekelezwa kwa vitendo.
Vuai
alieleza kwamba kupitia Mazungumzo na Gazeti la NIPASHE Juma Pili
Octobar 9, mwaka huu, Jussa alinukuliwa akisema CUF inaangalia uwezekano
wa kufanya mazungumzo na CCM kuhusiana na suala la uchaguzi, jambo
ambalo CCM haipo tayari kukaa meza moja na Chama hicho kujadili jambo
ambalo lishafanyiwa uamzi halili kwa mujibu wa kanuzi,taratibu na Sheria
za nchi.
Alisema
Chama hicho kinaweza kukikaribisha Chama chochote cha upinzani kufanya
mazungumzo juu ya namna gani ya kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa
Ilani ya CCM na siyo suala la Uchaguzi Mkuu kwani umepita kisheria na
serikali zinaendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Alisema
kitendo cha kujadili serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa sasa ni kwenda kinyume na Sheria za nchini
kwani serikali hizo zimetokana na maamuzi halali ya wananchi kupitia
mfumo wa Uchaguzi wa kidemokrasia.
Aliwataka
wafuasi wa Chama hicho na Wananchi kwa ujumla kupuuza madai
yaliyotolewa na Kiongozi huyo hasa mantiki ya kuundwa kwa serikali ya
mpito Zanzibar , hatua ambayo haiwezekani na inaashiria kuvunja Katiba
ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
“CCM
hatuna mpango wa kukaa meza moja na Chama chochote cha upinzani na sio
CUF tu, kujadili Uchaguzi kwani tayari umepita kwa vigezo vyote vya
uhalali wa kisheria.
Pia Hoja
na Ajenda ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Mpito Zanzibar kwa sasa ni ndoto
za mchana ama kujifurahisha kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa usiokuwa na
uzani wala mafanikio kwa wafuasi wa Chama kinachojenga hoja hizo hapa
nchini.”, alisema Vuai na kuongeza kuwa CCM inaamini kwamba Uchaguzi
umekwisha na sasa inajipanga na maandalizi ya Uchaguzi ujao wa mwaka
2020.
Naibu
Katibu Mkuu huyo, alifafanua kwamba CUF kwa sasa imekosa muelekeo ndiyo
maana viongozi wake wanafikia hatua ya kuwadanganya wafuasi wao kwa
mambo ambayo kiuhalisia wanajua kuwa hayawezekani kufanyika katika
historia ya uwanja wa kisiasa Zanzibar.
Alisema
Chama cha kisiasa chochote pamoja na kuwa na jukumu la kushinda na
kusimamisha Dola katika uchaguzi mkuu bado kinatakiwa kuwa na miongozo
imara ya kusimamia ukweli, haki na uwazi kwa wafuasi na wananchi, vigezo
ambavyo vimekosekana ndani ya CUF toka kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa
2015.
Alisisitiza
kwamba kazi iliyopo mbele ya Chama hicho ni pamoja na kujiandaa kwa
mambo mbali mbali yakiwemo Uchaguzi wa ndani wa CCM wa mwaka 2017, kwa
ajili ya kupata viongozi makini na mahodari ambao pia watakuwa na jukumu
la kusimamia maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Alilitaja
jukumu la msingi linalotekelezwa na chama hicho ni pamoja na uhakiki wa
Mali za CCM ili kujiridhisha zaidi ikiwa ni mkakati wa uimarishaji hali
ya siasa na uchumi ndani ya CCM.
Aliwasihi
wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu
na kushirikiana kikamilifu na serikali zote mbili Serikali ya Awamu ya
saba ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya awamu ya Tano ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania .
Aidha aliwataka wananchi kuwafichua baadhi ya wanasiasa wanaojihusisha na vitendo vya kuharibu amani na utulivu wa nchi.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment