
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza
na mkandarasi wa Kampuni ya China Civil pamoja na viongozi wa Serikali
mkoani Tabora wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Ndono-Urambo yenye
urefu wa KM 52 kuona hatua iliyofikiwa.

Meneja wa
Wakala wa Majengo Nchini (TBA), mkoa wa Tabora Qs.Tutu Lusama, akitoa
maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya
ya Urambo Bi Angelina Kwingwa wakati akikagua ujenzi wake.

Muonekano wa Nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Urambo mkoa wa Tabora, ambayo ipo kwenye hatua za mwisho za ujenzi wake.

Mkandarasi
wa Kampuni ya Chicco kutoka China (kushoto), akitoa taarifa ya ujenzi
wa barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 kwa Waziri wa
Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia),
alipokagua barabara hiyo kuona maendeleo yake.

Mbunge wa
Jimbo la Kaliua mkoani Tabora, Mhe. Magdalena Sakaya akifafanua jambo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
wakati alipokagua barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56
kuona maendeleo yake.
Serikali
imesema itaongeza mabehewa ya abiria na mizigo katika Shirika la Reli
la Tanzania (TRL), kwa lengo la kutatua adha ya usafirishaji kwa
watumiaji wa reli ya kati katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.
Akizungumza
katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa uhaba wa mabehewa ya
abiria umesababisha wananchi wa maeneo hayo kutumia njia zisizo rasmi
za ununuzi wa tiketi kwa ajili ya usafiri huo.
“Serikali
imetambua changamoto kubwa ya usafiri inayowakabili wakazi wa mikoa
hii, hivyo ni wakati muafaka kwa TRL kuongeza mabehewa matatu ili
kupunguza adha ya usafiri”, amesema Prof. Mbarawa
Aidha,
Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza uongozi wa TRL kwa kuokoa matumizi ya
zaidi ya Shilingi milioni 100 kwa kukarabati mabehewa ya mizigo 23 kwa
kutumia wataalam wazawa wa shirika hilo.
Ameongeza
kuwa Shirika hilo limetekeleza dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
kupunguza matumizi ya fedha na kuzingatia thamani ya fedha na kazi
inayofanyika.
“Nawapongeza
kwa kazi nzuri mnayofanya ya kupunguza matumizi ya fedha mnazopata
kwenye Shirika, ninaomba muendelee kutumia vyanzo vya ndani ili shirika
lifikie hatua ya kujitegemea” amesema Profesa Mbarawa.
Naye,
Meneja wa Usafirishaji wa TRL, mkoa wa Tabora Fredrick Masangwa ameiomba
Serikali kuendelea na maboresho katika miundombinu ya reli kwa kiwango
sawa na jinsi inavyoboresha miundombinu shindani ya barabara ili kuwepo
na ushindani sawa katika sekta hizo mbili za usafirishaji.
Katika
hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya
Ndono-Urambo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 52 na barabara ya
Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 na kuridhishwa na maendeleo ya
ujenzi na ukarabati wake.
Profesa
Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo iende sambamba na
viwango bora vya ujenzi wa barabara vilivyomo kwenye mikataba
iliyosainiwa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abeli Busalama ameipongeza
Serikali kwa juhudi za ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara
katika wilaya hiyo kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza fursa za
kiuchumi katika wilaya yake na wilaya za jirani pamoja na mikoa
inayozunguka wilaya hiyo.
Mbunge wa
Jimbo la Kaliua Mhe. Magdalena Sakaya amemuomba Waziri huyo kufikisha
mawasiliano ya simu kwenye wilaya hiyo hususan vijijini ili kuweza
kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Waziri
Mbarawa amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili katika Mkoa wa Tabora
ambapo amekagua miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, reli na
mawasiliano.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment