Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo (09,03,2017)
mjini Brussels katika mkutano wa kilele uliogubikwa na ajenda kadhaa
ikiwemo suala la uchaguzi wa Rais wa Baraza la Ulaya.
Mkutano huo wa kilele pia unatarajia kuangazia masuaala mengine ikiwa
ni pamoja na suala linalohusiana na uchumi barani ulaya, hali ya sasa
ya ukanda wa magharibi wa nchi za Balkan pamoja na suala la ulinzi na
ushirikiano wa kijeshi.Mkutano huo huenda ukawa wa mwisho viongozi wa Umoja wa Ulaya kukutana kabla ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kuanzisha rasmi mchakato wa kujitoa kwenye umoja huo kwa kutumia ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon.
Uingereza inatarajia kutangaza rasmi kusudio lake la kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi na hivyo kuanza rasmi kipindi cha miaka miwili cha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Mkutano huo unafanyika mnamo wakati kukiwa na mvutano kati ya Waziri Mkuu wa Poland Beata Szydlo na viongozi wengine wa mataifa yanayounda umoja huo ambao wanaonekana kuiunga mkono hoja ya Donald Tusk kuendelea tena na wadhifa huo huku Waziri Mkuu wa Poland akimshutumu Tusk ambaye alitokea katika chama cha upinzani nchini Poland cha Civic Platform (PO) na alikuwa afisa wa serikali nchini Poland kwa kujihusisha na siasa za ndani za Poland.
Hata hivyo kwa upande wake Tusk amesema yuko tayari na anasubiri uamuzi wa viongozi wa mataifa 28 yanayounda Umoja wa Ulaya katika kuelekea uchaguzi huo huku pia akikanusha hoja zilizoibuliwa na waziri mkuu wa Poland Beata Szydlo kuwa amekiuka tarataibu zake za kazi kwa kuingilia siasa za ndanai za Poland.
Tusk amesisitiza kuwa hausiki hata kidogo na migongano hiyo na kuwa haigemei upande wowote na wala hatarajii kufanya hivyo hata katika siku za usoni.
Serikali ya Poland ambayo haiungalii kwa jicho jema Umoja wa Ulaya na ambayo imekuwa ikirumbana naUmoja wa Ulaya juu ya utawala wa sheria Jumamosi iliyopita ilipendekeza jina la Mbunge wa Ulaya Jacek Saryusz- Wolsk kuwania nafasi hiyo badala ya Donald Tusk.
Tusk apewa nafasi kubwa ya kuchaguliwa tena
Ujerumani kwa upande wake imesema kuna dalili njema za kuchaguliwa tena kwa Tusk ambaye kipindi chake cha sasa cha uongozi kinamalizika mwezi Mei kuendelea kuwa Rais wa Baraza la Ulaya mnamo wakati wanadiplomasia wa ualaya wakiishutumu serikali ya Poland kwa kutaka kuhusisha masuala ya ndani na masuala ya kimataifa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuchaguliwa kwa Tusk ni ishara ya uthabiti ndani ya Umoja wa Ulaya.
Mvutano huo kati ya serikali ya Poland na Umoja wa Ulaya unaelekea kuleta mgawanyiko katika kipindi ambacho viongozi wa umoja huo wametoa mwito wa kuimarishwa umoja mnamo wakati Uingereza ikijiandaa kuanzisha rasmi mchakato wa kujiondoa kwenye umoja wa ulaya.
SHARE
No comments:
Post a Comment