TAREHE 1 APRILI, 2017 WASHINGTON
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
fursa hii. Pia niwashukuru ninyi nyote mlioweza kufika hapa. Vilevile
nawashukuru wote walioanza kuunga mkono harakati hizi na hatimae
tumeweza kufikia hatua hii ya kuwepo kwa mkutano huu muhimu sana katika
mstakabali wa taifa letu.
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Tumekutana hapa kwa nia ya kukumbushana sisi kwa sisi, wapi hapajakaa sawa na ni vipi tutaweza kurekebisha kwa haraka, ili taifa letu liwe katika hali ya kuridhisha na kuheshimika.
Katika kutimiza nia hii ya kukumbushana,
imeonekana ni muhimu tutumie njia ya kuweka Shindano la Hoja juu ya
“jambo mtambuka” ambalo likisimamiwa na kuenziwa inavyostahili, tutaweza
kuondokana na hali ya sintofahamu inayolikumba taifa letu sasa.
Shindano hili litajenga hoja juu ya Sifa za Rais Bora wa Nchi kama
Tanzania.
Shindano hili ni mwendelezo wa Kampeni
ya Kuinua Maadili Kitaifa ambayo ilizinduliwa tarehe 14 Januari 2017 na
kilele chake ni tarehe 10 Disemba, 2017. Taarifa zaidi ya Kampeni hii
inapatikana: www.maadilkitaifa.blogspot.com
Lengo Kuu la Shindano hili la Hoja:
Ndugu Wanahabari na Watanzania Wenzangu;
Lengo kuu la shindano hili la hoja ni kulinda na kudumisha uhuru na umoja wa Taifa, ambavyo ndio ngao yetu.
Katika kutimiza lengo kuu hilo shindano hili litasaidia mambo yafuatayo:
i) litadhibiti kauli zenye kushusha hadhi ya kiti cha Urais
ii) litasaidia vyama vyetu vya siasa kupata muongozo wa sifa za wagombea Urais zenye kulenga maslahi ya taifa na sio ya chama
iii) litaiongezea nguvu katiba yetu katika suala la sifa za mgombea Urais
iv) litawasaidia wale wote wenye ndoto
za kuwania nafasi ya kiti cha Urais siku za mbeleni, waweze kujipima
kabla hawajatangaza nia zao na kabla hawajaingia kwenye mchakato wa
kupimwa na vyama vyao, ili taifa liwe na chaguzi zenye wagombea wenye
hadhi ya uongozi unaoenzi ngao ya taifa
v) litajenga umoja wa kitaifa katika masuala yote ya kuliimarisha na kuliendeleza taifa letu
Washindanaji: Wasimamizi/Viongozi wa Vyombo vya Habari vyote Tanzania
Muda wa Shindano: 3 Aprili – 3 Mei, 2017 (Siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani)
Maelezo ya Msingi juu ya Shindano hili:
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Katika mstakabali wa Taifa lolote
duniani, suala la wadhifa wa Urais wa nchi ni muhimu sana kuliangalia
kwa jicho la tatu kwani Rais wa nchi ni taswira ya taifa analoliongoza.
Maana yake, hadhi ya Rais wa nchi, inawakilisha hadhi ya watu wake.
Inapotokea mtu yeyote wa ndani au nje ya nchi kumdhalilisha au kumbeza
Rais wa nchi kwa namna yeyote ile, mtu huyo anakuwa amedhalilisha na
kubeza taifa zima.
Katika nyakati hizi, tumekuwa tukisikia kauli zenye utata zinazoligawa, kulidhalilisha na kulidhoofisha taifa letu.
Kwa mfano utasikia; Rais aliyepo
madarakani ni wa kundi fulani (wa chama fulani; au Rais wa wanyonge;
masikini; au wa dini fulani). Kauli kama hizi kwa hakika zinashusha
hadhi na pia zinadharilisha, kubeza na kudhoofisha nafasi ya kiti cha
urais.
Vile vile utasikia watu wanatumia lugha
zisizo na staha kudhalilisha, kubeza na kudhoofisha nafasi ya kiti cha
Urais. Hii yote imetokana na kutokuwa na muongozo wa kitaifa katika
kubainisha wadhifa wa kiti cha urais wa nchi.
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu;
Taifa linaundwa na watu wa aina zote
(Wanyonge, wenye nguvu za kifedha, kifikra, kitaaluma, masikini,
matajiri, wabaya, wazuri, wenye Imani tofauti na watanzania wa aina
zote).
Jukumu la msingi katika nafasi ya Urais
wa nchi yoyote ile ni kuinua na kuboresha ubora wa taifa, na sio kuibua
na kuthibitisha ubaya wake. Mfano; Rais anapoona baadhi ya watu wake
hawako vizuri, hapaswi kuwathibitishia mabaya yao, bali anatakiwa atumie
mkakati wa kiuongozi kuhakikisha watu wake wanakuwa sawa; na hivyo
kutunza hadhi na heshima ya taifa zima. Ule msemo wa “Samaki mmoja
akioza ni wote” hujidhihirisha sana katika hadhi na heshima ya taifa.
Daima tuwe makini sana katika kauli
zinazodhalilisha, kubeza na kudhoofisha hadhi ya kiti cha urais kwani
tusipokuwa makini tutaondoa heshima ya taifa letu ambayo ni heshima yetu
wenyewe. Daima tukumbuke maana ya taifa ni watu. Na watu wenyewe ndio
mimi, wewe na watanzania wote. Tuwe makini, tusikubali kujidhalilisha,
kujitukana wala kujidhoofisha kwa namna yoyote ile kupitia kwa kiti cha
urais.
Tumesikitika sana, tumesononeka sana, na
tumeumiza sana mioyo yetu, hatuwezi kuendelea kuvumilia, lazima
tuchukue hatua madhubuti za kudhibiti hali hii ili tustiri utu wetu na
hatimae kwa furaha tulionee fahari taifa letu Tanzania.
Wapi Hapajakaa Sawa?
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu,
Uchunguzi nilioufanya kupitia tasnia ya
Maendeleo ya Watu unaonyesha kuwa, kauli za kushusha hadhi ya kiti cha
Urais zimetokana na vigezo vinavyotumika kupata wagombea wa nafasi ya urais hapa nchini Tanzania.
Imeonekana kwamba vyama vya siasa vinatumia vigezo vya kichama kutafuta
mgombea urais , vigezo ambavyo havikidhi maslahi ya taifa. Kwa kuwa
hali ya kudhihakiwa na kufedheheshwa kwa taifa inashusha kasi ya
maendeleo nchini, ni jambo la busara taifa likachukua hatua za haraka
kuondokana na hali hii ili tuweze kuwa na kasi katika kutafuta
maendeleo.
Kwa kuwa tupo katika ulimwengu wa
sayansi na teknolojia, ulimwengu wa digitali, ni lazima mfumo wetu wa
maendeleo ufuate kasi ya sasa. Kwa minajili hiyo imetulazimu tutafute
mbinu yenye nguvu ya haraka ya kuondoa kabisa hali hii, ambayo siyo
mbinu nyingine bali ni: Shindano la Hoja juu ya Sifa za Rais Bora wa Nchi.
Ni vipi tutaweza kuparekebisha kwa haraka?
Ndugu Wanahabari na Watanzania wenzangu,
Katika kufikia malengo ya kuendesha
shindano hili ilibidi tubuni njia ya uhakika na itakayokuwa na ufanisi
mkubwa. Ndio maana tukaamua kuchagua viongozi/wasimamizi wa vyombo vya
habari wawe washindanaji katika shindano hili la kihistoria. Nia ya
kuwashindanisha hawa ni kwa sababu:
i) Wanauwezo wa kusambaza ujumbe kwa haraka nchi nzima
ii) Wanarasirimali watu yenye uwezo mkubwa wa kuchambua na kupanga hoja vizuri
iii) Wana mbinu za kukusanya hoja kwa namna nyingi kuliko viongozi/wasimamizi wa tasnia zingine
iv) Tutakapo hitimisha shindano hili na
kupata vigezo vya sifa za mtu anayefaa kuwa rais bora, washindanaji hawa
wanauwezo wa kufikisha taarifa kwa jamii nzima na hasa wanasiasa
wanaotuletea wagombea urais na wale wote wenye ndoto za kuwainia nafasi
ya kiti cha urais siku za usoni.
v) Wanauwezo mkubwa wa kuitengeneza
jamii kimtazamo na hivyo watasaidia sana kufanya chaguzi za nafasi ya
kiti cha Urais kuwa za ushabiki wa kitaifa Zaidi na sio wa kichama.
Vigezo vya kupata washindi:
Kwa kuwa suala la sifa za Rais bora ni
kwa ajili ya kulinda na kutunza hadhi ya Taifa letu tunasisitiza
washindanaji wote watumie mbinu mbalimbali kuwashirikisha watanzania
wote katika kuchangia hoja za sifa za rais bora.
Katika mchujo wa kutafuta mshindi wa kwanza hadi wa kumi (1-10) vigezo vifuatavyo vitazingatiwa:
1. Hoja zenye mantiki zinazoelezea vigezo/sifa za rais bora
2. Mbinu zilizotumika kuwashirikisha wadau wengine katika kukusanya hoja
3. Idadi ya watanzania walioshiriki
kuchangia hoja kwenye chombo cha habari husika (takwimu zitahitajika
ziainishwe) – tunahitaji Watanzania wa fani zote washiriki katika utoaji
wa sifa za rais wanaemtaka.
Zawadi:
Zawadi za washindi zitakuwa kama zifuatazo:
A: Washindanaji wote watapata Cheti cha
Ushiriki wa Shindano. Kwa washiriki wote wa shindano waliotoa hoja zao
kwa kupitia vyombo vya habari wa washindanaji wanaowaunga mkono
watapata:
Nakala za kitabu cha Kampeni ya Kuinua
Maadili Kitaifa 2017 (Kinaitwa: Chombo Mhuhimu kwa Maendeleo Yako)
zitakabidhiwa kwa washindanaji (Tunaomba wadau Zaidi wajitokeze
kufadhili uchapishwaji wa nakala zaidi) kupitia email yetu:
maadilikitaifa2017@gmail.com.
B: Mshindi wa kwanza hadi wa kumi (1-
10) waliokidhi vigezo vya shindano hili watapata zawadi zilizotajwa
kwenye A pamoja na pesa kwa viwango vifuatavyo:
1. 10m
2. 9m
3. 8m
4. 7m
5. 6m
6. 5m
7. 4m
8. 3m
9. 2m
10. 1m
(Pesa hizi tayari zimepatikana).
Zawadi zote zitatolewa siku ya kilele
cha Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa tarehe 10 Disemba, 2017 ambapo
washiriki wote waliochangia hoja kwa kupitia ofisi za vyombo vya habari
watapewa nakala ya kitabu cha kampeni ya kuinua maadili kitaifa.
Kwa heshima na taadhima Mwenyekiti wa
Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) Dr. Reginald
Mengi amependekezwa kuwa mgeni rasmi siku ya utoaji zawadi hizo. Hivyo
nachukua fursa hii kumtaarifu rasmi Dr. Reginald Mengi ili aweke siku
hiyo katika ratiba yake. Na tunamuomba atutumie email ya kukubali
pendekezo letu hili kupitia: maadilikitaifa2017@gmail.com
Maelezo juu ya Kampeni ya Kuinua Maadili Kitaifa pamoja na maelezo kuhusu kitabu yanapatikana: www.maadilikitaifa.blogspot.com
Wito kwa Watanzania:
Ndugu Wanahabari na watanzania wenzangu;
Shindano hili ni la kihistoria na linamhusu kila mtanzania.
Nichukue fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza watanzania walio hapa Marekani kwa kukubali kuunga mkono
shindano hili. Wamefanya jambo muhimu sana katika kutunza heshima na
hadhi ya taifa letu zuri la Tanzania.
Kwa ajili ya mstakabali wa taifa letu
tunaomba sana vyombo vyote vya habari vishiriki kwa dhati shindano hili
ili tuwafikie makundi yote ya watanzania nchi nzima.
Pia nichukue fursa hii kuwaomba watu
mbalimbali wajitokeze kuwezesha (kifedha au kihuduma) shindano hili ili
tufanikiwe. Katika kufanikisha Shindano hili tunahitaji kukamilisha
mambo yafuatayo:
1. Fedha taslimu TSh. 55 milioni pamoja na vyeti kwa ajili ya washindanaji – tayari wadau wamejitokeza kukamilisha
2. Watoa hoja nchi nzima – Tunategemea washindanaji walisimamie
3. Uchambuzi na uchujaji wa hoja – Tunategemea washindanaji walishughulikie na kututumia hoja za msingi
4. Nakala za kitabu kinachoambatana na
shindano (zinahitajika nakala za kusambaza kwa wapiga kura nchi nzima
ili tuwajenge kifikra kama msingi wa umadhubuti wa taifa letu) –
Tunaomba wadau waliohamasika na shindano hili wasaidie gharama za
uchapishaji pia wanaweza kulipia moja kwa moja kwa mchapishaji. Tunaomba
tuwasiliane nasi kupitia email: maadilikitaifa2017@gmail.com
SHARE
No comments:
Post a Comment