TRA

TRA

Monday, April 24, 2017

Unga wa ugali kama almasi!

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !

Said Mwishehe

MAISHA yamebadilika na kuna wakati huwa nawaza sijui yanakwenda mbele au nyuma?

Angalia mambo yanavyokwenda halafu hata yale ambayo zamani yalikuwa yanaonekana magumu leo hii yanawezekana na yale yaliyokuwa yanawezakana zamani leo yanaonekana kuwa na ugumu wake.

Nadhani maisha ndivyo yalivyo acha yaendelee kwani kuishi kwingi ndiko kuona mengi. Macho yetu kodoo yaani tunasubiri kuona yanayotokea.

Kwa kuna mambo mengi yanaendelea basi na mijadala nayo haiishi. Ukienda huku wanazungumza hili na ukienda kule nako wanazungumza la kwao. Kila mmoja anazungumza lake.

Wapo ambao wanazungumza kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa kwa ajili ya treni ya mwendo kasi ambayo tunaambiwa itakuwa inatumia umeme.



Pia wapo wanaojadili kuhusu kupotea kwa ndugu yetu, rafiki yetu na Mtanzania mwenzetu, Ben Saanane ambaye amepotea yapata miezi sita sasa.

Wengine wanajadili matukio ya kutekwa kwa baadhi ya watu wakiwamo wasanii. Wapo wanaozungumzia namna ambavyo ipo haja ya vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga zaidi ili kudhibiti matukio ya mauaji hasa yanayofanywa dhidi ya Polisi kama yale ya Kibiti mkoani Pwani.

Kwa kuwa maisha yanasonga ndivyo ambayo mambo yanaendelea kuibuka na kuzua mjadala achilia mbali la kuzuia filamu za nje kuuzwa nchini kwetu ili kulinda soko la waigizaji wa ndani. Wamewaza wakaona hiyo ndio suluhu pekee ya kuwaisaidia waigizaji wa ndani. Ama kweli mengi yanatokea.

Kwa Ujinga Wangu sina hata moja ninayowaza kati ya hayo ambayo nimeyaeleza hapo juu. Acha wenzangu wajadili, wachambue na kisha watapata majibu yao kulingana na aina ya mijadala yao.

Nachojadili kwenye kichwa changu ni hili la bei ya unga ambapo imefikia kilo moja Sh. 2,200 kwenye maeneo mengi ya nchi yetu.

Kila mahali wanajadili kuhusu bei ya unga. Imefika mahali ugali unaonekana kama ni chakula cha anasa. Eti leo hii ugali unaliwa na wenye fedha na wasio na fedha wanaanza kukimbilia mchele maana bei yake kidogo.

Kwa Ujinga Wangu ni jambo la kushangaza ugali ambao ulionekana kama hauna thamani mbele ya wali a.k.a ubwabwa leo mambo yamegeuka. Ugali leo unaoneka ni chakula cha gharama kuliko wali. Ama kweli maisha yanabadilika.

Bei ya unga hivi sasa inaumiza vichwa vya watu.Bei imekuwa kubwa kuliko ambavyo watu wamezoea. Nyumba nyingi hivi sasa watu wanakuka vyakula ambavyo bei yake ina unafuu zaidi ya unga.

Kwa Ujinga Wangu bei ya unga imesababisha hata wenye mamlaka nao kukaa kimya maana hakuna ambaye anaizungumzia. Nadhani wapo kimya si kwa sababu wanashindwa kuizungumzia bali nao wanashangaa kwanini imekuwa hivyo.

Bei ya unga imesababisha kila mtu anapotaka kula ugali aanze kufikiria wapi atapata fedha. Kwa bei hii ya unga kama haitapata ufumbuzi wake kuna hatari ya huko tunakoelea watu kutokula kabisa ugali.





Kilo moja ya unga Sh 2,200 na iwapo familia inahitaji kilo mbili au tatu kwa siku unaweza kuona fedha inayohitajika. Kwa hali ya uchumi wa Watanzania walio wengi ni ngumu kumudu kula ugali kila siku.

Kibaya zaidi kwenye unga huwezi kuchagua bei maana ni moja angalau kwenye mchele unaweza kupata wa bei ya chini kulingana na ubora wake.

Kwa Ujinga Wangu naiona haja ya wakulima kujikita zaidi kwenye kilimo cha mahindi kwani ndiko soko lilipo. Ni wakati wa wakulima kuangalia nini kifanyike kuhakikisha mahindi yanapatikana ya kutosha ili angalau bei ishuke na tuimudu.

Huenda hali ya ukame imechangia mahindi kukosekana na hata yakipatikana yanashindwa kutosheleza mahitaji ya soko. Kwa Ujinga Wangu unga hivi sasa tunauhitaji zaidi kuliko ambavyo unga unatuhitaji sisi. Tunakoelekea mwenye unga ndani ataonekana kama vile anamiliki almasi ndani.









Unga ambao ulikuwa kimbilio la wengi unaonekana kimbilio la wachache. Kwa Ujinga Wangu lazima tutaendelea kulalamika hali ngumu ya maisha na kwa asiye lalamika ana namna nyingine ya kumfanya aishi kwa raha mustarehe.

Kwa Ujinga Wangu Serikali itoe tamko kuhusu bei ya unga, ukimya wake nao unaibua maswali mengi. Natamani Serikali iagize mahindi hata nje ya nchi kama kwetu hayapo ili bei ya unga iwe chini kidogo. Tunaumia bwana.

Simu 0713 833822

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger