Madaktari walipokuwa kwenye mgomo nchini Kenya
NAIROBI,
Kenya
SHIRIKA la
Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), ambalo hutumiwa na taifa hilo kutoa
misaada kwa nchi za nje, limesitisha ufadhili wake kwa miradi ya afya nchini.
Kwa mujibu
wa taarifa kutoka katika shirika hilo, ilisema hatua ya kusitisha ufadhili kwa
miradi yote ya Wizara ya Afya ya Kenya imetokana na hatua ya Kenya kutotimiza ‘masharti
ambayo hayajaelezwa’.
Maofisa wa
USAID wameagizwa kutojishughulisha na ‘shughuli zozote za kibiashara’ na
taasisi za Serikali ya Kenya pamoja na mashirika mengine yenye uhusiano na Serikali.
Hatua hiyo
ya Marekani inatarajiwa kuathiri miradi mbalimbali ya Serikali, ikiwemo mipango
ya kukabiliana na malaria, kifua kikuu na ukimwi pamoja na miradi ya uzazi wa
mpango, huduma za afya kwa wajawazito na watoto.
Kwa miezi
kadhaa sasa, Wizara ya Afya nchini, imekumbwa na tuhuma za ulaji rushwa. Sekta
hiyo pia ilitatizwa na mgomo wa taifa wa madaktari ambao ulidumu kwa siku 100
kuanzia Desemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu.
Mwaka
uliopita, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini alisema jumla ya dola za
Marekani milioni 50 (sh bilioni 110 za Tanzania) hazikubainika zilivyotumiwa
katika wizara hiyo.
Maofisa
wakuu katika wizara hiyo pamoja na jamaa za baadhi ya viongozi wakuu Serikalini
walidaiwa kuhusika katika kufujwa kwa fedha hizo.
Hata hivyo, Wizara
ya Afya ilijitetea na kudai hayo yalikuwa kwenye ripoti ambayo ilifichuliwa
mapema kabla ya wahasibu wa wizara hiyo kujibu maswali yaliyoibuliwa na mkaguzi
huyo kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Mwandishi wa
BBC, Abdinoor Aden alisema hatua hiyo ya Marekani itaibua maswali zaidi kuhusu
usimamizi wa fedha katika Wizara ya Afya nchini, licha ya hatua ya Rais Uhuru Kenyatta
ya kumhamisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Hatua ya
USAID inatarajiwa kuathiri miradi ya Serikali pamoja na miradi ya mashirika
mengine ya afya ambayo hutumiwa na USAID kutoa huduma maeneo mbalimbali nchini.
BBC
SHARE
No comments:
Post a Comment