NA MWANDISHI
WETU, ZANZIBAR
CHAMA cha Ushirika cha Msingi cha Masoko cha Mtule
(Mtule AMCOS) kinachojishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda
kimeweka bayana nia yake ya kuchangamkia fursa za mikopo nafuu
inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuwasaidia
katika kuendeleza kilimo chao.
Akizungumza wakati ugeni kutoka TADB ulipotembelea
kijijini Mtule, Mwenyekiti wa Mtule AMCOS, Mzee Mgana Zidi Khamis amesema kuwa
Chama chake kimejidhatiti katika kufikia soko kubwa la matunda na mboga mboga
ila wanarudishwa nyuma na uduni wa mtaji pamoja miundombinu ya masoko.
“Tulisikia uwepo wa Benki ya Kilimo ila hatukuwa
tunajua namna ya kuwapa, leo tunaamini kuja kwenu kijiji hapa kumefufua
matumaini yetu ya kupatiwa mikopo ili kuongeza tija kilimo chetu na kipato
chetu kwa ujumla,” alisema.
Akiwasilisha malengo ya safari yao na umuhimu wa Benki
hiyo kwa wakulima nchini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis
Assenga amesema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini kote
ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza
mapinduzi katika kilimo nchini.
Bw. Assenga aliongeza kuwa kilimo cha mbogamboga na
matunda ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili
ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa
thamani wa mbogamboga na matunda nchini.
Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza
uongezaji wa thamani wa kilimo cha mazao yote yatokanayo na mbogamboga na
matunda ili kuongeza tija kwa wakulima nchini kote.
“Benki inatoa mikopo na kusaidia uwekezaji kwa ajili
ya uongezaji tija wa kilimo cha mboga mboga na matunda, uongezaji wa thamani wa
mazao ya mboga mboga na mtunda ili kuchagiza uongezaji wa kipato kwa mkulima,”
alisema.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw.
Augustino Chacha amesema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo
ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2
hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka
Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika
kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha
kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na
kupunguza umaskini nchini,” alisema.
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw.
Augustino Chacha (kulia) akizungumza kuhusiana na mikopo na huduma zinazotolewa
na TADB katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Chama cha Ushirika cha Msingi
cha Masoko cha Mtule.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
(kulia) akizungumza na wanachama wa Mtule AMCOS (hawapo pichani) kuhusu
dhima ya Benki ya Kilimo kuwapatia mikopo nafuu wakulima nchini. Kushoto
ni Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo na Afisa Mipango kutoka
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Bw. Nassor
Mohammed (katikati).
Wanachama wanawake wa Mtule AMCOS wakifuatilia
mawasilisho ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB (hayupo pichani) kuhusu uwepo
wa mikopo nafuu kutoka Benki hiyo.
Katibu wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Masoko cha
Mtule (Mtule AMCOS), Bw. Ali Fadhil Ali akiongea wakati Benki ya Kilimo
ilipotembelea Kijiji cha Mtule kukagua miradi ya kilimo inayohitaji mikopo.
SHARE
No comments:
Post a Comment