Julian Msacky
UKITEMBELEA nchi kama Burundi au Uganda ni jambo la kawaida
kuona askari wakirandaranda barabarani na silaha.
Hali ya namna hii huonesha kwamba usalama wa nchi husika si
mzuri ndiyo maana askari hawabanduki na silaha.
Ni tofauti na hapa kwetu ambako ukiona askari ana silaha
aidha atakuwa lindo au yupo kwenye tukio maalumu.
Kwa maana nyingine ni kuwa Watanzania hawajazoea kuona silaha
hadharani, lakini siku hizi hali imeanza kubadilika.
Silaha zimeanza kuonekana hadharani na wakati mwingine
zikitumika vibaya. Hii si dalili njema ni lazima tuikomeshe.
Ni ukweli usiopingika kuwa silaha sasa ni tishio nchini
kwetu. Zinakatisha maisha ya raia wasio na makosa karibu kila siku.
Ukikaa hivi utasikia kiongozi huyu au yule kauawa na raia
vivyo hivyo. Ndiko silaha zilikotufikisha sasa.
Inavyoonekana silaha nyingi zipo mikononi mwa watu ambao si
waaminifu ndiyo maana madhara yake yamekuwa mengi.
Yanayotokea Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani ni mfano hai. Tusipoangalia
tunaweza kutengeneza kizazi cha ajabu.
Tunaweza kutengeneza vikundi vya kihalifu kama ilivyo kwa
baadhi ya anchi ambazo zinatuzunguka.
Matokeo yake tutashindwa kulala usingizi. Ili tusifikie huko
na kuepuka kujitumbukiza kwenye mafuta ya moto tuchukue hatua.
Hii ni kwa sababu hali si nzuri. Ndiyo maana baadhi ya
wabunge walipendekeza wanajeshi wapelekwe Pwani kuweka mambo sawa.
Hii ni kwa sababu Mkoa wa Pwani hali si shwari hata kidogo.
Nguvu za ziada zinahitajika ili kurejesha hali ya utulivu.
Amani haitarejea hivi hivi. Ni lazima kama nchi tuhakikishe
utumiaji holela wa silaha unakomeshwa mara moja nchini kwetu.
Kitendo cha askari saba kuuawa Wilaya ya Kibiti huku viongozi
na baadhi ya wananchi wakiendelea kuuawa, kinaibua maswali kuliko majibu.
Wapo wanaohoji tunaelekea wapi kama nchi katikati ya mauaji
ya namna hiyo?
Tunadhani ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kuhakikisha
silaha zote zinaondolewa mikononi mwa raia.
Lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha usalama wa nchi yetu
unaimarika zaidi na kukomesha matumizi holela ya silaha kwani ilivyo sasa hali
si nzuri.
Kwa nini tunashauri hivyo? Ni juzi tu Mkuu wa Polisi Wilaya
(OCD), Amedeus Malenge aliuawa na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake
Kinyerezi, Dar es Salaam.
Kama hiyo haitoshi, mfanyabiashara mwingine mkoani
Kilimanjaro aliuawa na watu wanaodaiwa majambazi na kuondoka bila kuiba kitu
chochote.
Mauaji hayo yametekelezwa kwa kutumia silaha ambazo wakati
mwingine zipo mikononi mwa watu walioaminiwa au kinyume chake.
Kwa sababu hiyo ni lazima tuhakikishe silaha zote
zinarejeshwa mikononi mwa Serikali na kama ni kutolewa zitolewe upya baada ya
kuweka mazingira safi.
Tunasema hivi kwa sababu inavyoonekana kuna silaha nyingi
uraiani ambazo zinatumiwa vibaya na baadhi ya watu.
Haiwezekani kwa nchi ambayo hakuna vita watu wanauawa ovyo
kwa kutumia silaha za moto. Hili halikubaliki.
Ni lazima tuhakikishe tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa
haraka kwa ustawi wa nchi na watu wake.
Tunasisitiza hivyo kwa vile matukio ya namna hiyo tulizoea
kusikia nchi zenye migogoro, lakini kwa nchi kama yetu si sahihi hata kidogo.
Tunashauri mchakato wa kuzirejesha mikononi mwa Serikali uwe
wa haraka kwa sababu kama askari wanauawa raia wa kawaida itakuwaje?
Inawezekana uaminifu wa kumiliki silaha umepungua kwa kiwango
kikubwa miongoni mwetu na kusababisha madhara tunayoshuhudia leo.
Kama nchi hatuna sababu ya kujitakia matatizo yanayoepukika.
Jambo la msingi ni silaha kubaki mikononi mwa Dola.
Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia pamoja na mali
zao hivyo tunaamini wanatosha badala ya silaha kubaki kwa watu ambao
hawaaminiki.
Ni matumaini yangu kuwa kwa kufanya hivyo tutakomesha
utumiaji holela wa silaha kwa ustawi wa nchi na watu wake.
SHARE
No comments:
Post a Comment