Mkuu
wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amewasisitiza wananchi kutoa ushirikiano
kwa jeshi hilo kwa kutoa taarifa za wahalifu waliopo katika maeneo yao jambo
ambalo litapunguza au kuondoa kabisa uhalifu nchini.
IGP
Sirro ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada
ya kuapishwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi
la Tanzania.
Amesema
kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kulinda na kuhakikisha usalama wa raia na mali
zao hivyo ni wajibu wa jeshi hilo kuhakikisha nchi nzima ina ulinzi wa kutosha
utakaopelekea wananchi kuishi kwa amani na utulivu na kuwawezesha kufanya kazi
zao bila kubugudhiwa.
“Uhalifu
hauwezi kupungua kwa kutegemea Jeshi la Polisi pekee bali tunahitaji nguvu ya
pamoja ili kushinda vita hiyo, ushirikiano wa wananchi unahitajika kwa kiasi
kikubwa”,Alisema IGP Sirro.
Ameongeza
kuwa kipaumbele cha kwanza katika utendaji wake kwenye nafasi hiyo ni kupambana na uhalifu pamoja
nidhamu ya watendaji kazi kwani bila nidhamu, kazi ya kupambana na wahalifu
haiwezi kufanikiwa.
Aidha,
amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Pwani ambao umekuwa na mauaji na uhalifu wa
mara kwa mara kuwa atafanyia kazi changamoto zinazowakabili na kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani
na utulivu.
Kwa
upande mwingine, IGP Sirro amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumuamini na kumteua
katika cheo hicho pia amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda
kwa ushirikiano wake wakati alipokuwa akitumikia cheo cha Kamishna wa Polisi wa
Kanda maalum ya Dar es Salaam.
Kabla
ya uteuzi huo, IGP Sirro alishika nyadhifa mbali mbali zikiwemo za Kamanda wa
Polisi mkoa wa Mwanza, Kamanda wa kikosi cha operesheni maalum na Kamanda wa
Kanda Maalum ya Dar es salaam.
SHARE
No comments:
Post a Comment