Julian
Msacky
MEI 3 ya
kila mwaka imetengwa maalumu na Umoja wa Mataifa (UN) kuadhimisha Siku ya Uhuru
wa Vyombo vya Habari Duniani.
Siku hii iliidhinishwa
kwa mara ya kwanza na umoja huo mwaka 1993 kutokana na mabadiliko makubwa ya
kisiasa na uchumi duniani.
Lengo la
siku hii ni kuangalia changamoto zinazokabili waandishi na mazingira
wanayofanya kazi kama yanaridhisha au la.
Dk Harrison Mwakyembe Waziri mwenye dhamana ya habari
Si hivyo tu
bali kutambua pia mchango wa waandishi waliopigania taalamu ya uandishi wa habari
hadi tone la mwisho la maisha yao.
Kwa lugha
nyingine ni siku muhimu kwa waandishi wa habari kutathmini na kupitia
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo duniani.
Hata hivyo,
wakati siku hii ikidhimishwa jambo la kusikitisha ni kuwa vyombo vya habari
vinafanya kazi katika kipindi kigumu hususan Afrika.
Sababu kubwa
ni kwamba viongozi wengi wanaviona vyombo hivyo kama adui wao wakati kwa vile
tu vinasema mambo ya ukweli.
Ndiyo maana
waandishi wanakamatwa, kushtakiwa na wakati mwingine maisha yao kuwa hatarini
kutokana na kazi wanayofanya.
Ripoti ya
Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ya mwaka huu (2017) imeeleza mengi kuhusu
hali halisi ya vyombo hivyo ilivyo duniani.
Kwa mujibu
wa ripoti hiyo Namibia, Ghana na Cape Verde ndiyo zinazotoa uhuru mkubwa kwa
vyombo vya habari kwa upande wa Afrika.
Hii maana
yake kinachoendelea katika mataifa mengine ya Afrika ni ukandamizaji wa uhuru
wa habari. Hii si habari njema hata kidogo.
Matokeo yake
ni kwamba viongozi hawataki kuambiwa ukweli hata kama wanaongoza nje ya misingi
ya utawala bora na sheria.
Nchi ambazo
hazizingatii misingi hiyo kusema kweli maendeleo huwa duni na ujenzi wa utawala
wa kidemokrasia hukosa mwenyewe.
Amani ndani
ya nchi na mtu mmoja mmoja hufifia na watu kuishi kwa hofu kwa sababu tu ya
kuwa na viongozi ambao si rafiki wa vyombo hivyo.
Ni katika
mazingira hayo vyombo vya habari vinafanya kazi kwa kuchechemea na wakati
mwingine vingine kukuta vikifungwa.
Si hivyo tu
bali ni Afrika hii viongozi hutumia nguvu kubwa kutengeneza sheria kali ili
vishindwe kufanyakazi kwa uhuru unaotakiwa.
Viongozi
wanasahau kuwa bila uhuru wa vyombo vya habari hakuna maendeleo endelevu kwani
mambo mengi hufanyika gizani.
Nchi
zinazobana uhuru wa waandishi huishia kutumia nguvu nyingi katika mambo yasiyostahili
na uonevu hutawala.
Ni kwa nini
tunashindwa kujifunza kutoka nchi nyingine namna zinavyotoa uhuru mpana kwa
vyombo vya habari na hakuna kinachoharibika?
Ripoti hiyo
inasema Norway, Sweden, Finland zimeendelea kufanya vizuri katika kutoa uhuru
wa vyombo hivyo pamoja na waandishi.
Swali ni je,
kuna tatizo gani katika nchi zetu za Afrika na mataifa mengine ambayo kuwa
mwandishi ni sawa na kujitakia kifo.
Nchi zetu za
Afrika hazitakiwa kuwa kama China, Vietnam, Korea Kaskazini au Syria ambako
waandishi wanapitia tanuru la moto.
Viongozi
hawana sababu ya kuogopa waandishi wala vyombo vya habari kwani vipo kwa ajili
ya kutetea maslahi ya nchi na watu wake.
Mwasisi wa
Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa muumini mkubwa uhuru wa vyombo vya
habari (freedom of press).
Mwaka 1970
alisisitiza uhuru wa vyombo vya habari ni jambo muhimu katika kujikita kwenye
mijadala inayojenga nchi na maslahi ya watu.
Nyerere
hakuishia hapo bali alisema vyombo hivyo ni ruksa kukosoa serikali pamoja na
chama (TANU) na kuweka udhaifu wote hadharani.
Alitilia pia
mkazo kuheshimu uhuru wa watu kujieleza akitambua kwamba hiyo ni haki ya msingi
ikiwa ndani ya Katiba.
Ni Nyerere
huyo huyo aliyesema vyombo vya habari ni jicho la serikali kwa maana kuwa ili
ifanyie kazi vizuri lazima imulikwe.
Katika
mazingira ya namna hii hatuoni sababu ya viongozi wa zama hizi kuhofia vyombo
vya habari na badala yake wanatakiwa kuvilea.
Kiongozi
mwadilifu, mkweli na asiyetumia madaraka yake vibaya hana sababu ya kuhofia
vyombo hivyo pamoja na waandishi wake.
Hii ina
maana kuwa viongozi wanaochukia waandishi wa habari wana lao jambo na si
kupigania maslahi ya nchi na watu wake.
Ni kwa
sababu hiyo ninapenda kuwasilisha hapa kuwa viongozi wavilee vyombo vya habari
kwa ustawi wa jamii pana na si vinginevyo.
Kwa msingi
huo vitakuwa mhimili muhimu katika ujenzi wa taifa na kurutubisha utawala wa
sheria ndani ya bara letu la Afrika.
Ni lazima
tukumbuke kuwa kukandamiza vyombo vya habari ni sawa na kuruhusu shetani
kutamba altareni jambo ambalo si sahihi hata kidogo.
SHARE
No comments:
Post a Comment