BODI ya Utalii Tanzania
(TTB) imetoa wito kwa Watanzania kupenda kutembelea vivutio vya utalii vya
ndani kwa lengo la kukuza na kuinua pato la Taifa.
Wito huo ulitolewa jana
na Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bodi ya Utalii, Geofrey Tengeneza alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya kuhusiana na kampeni ya
kuhamasisha utalii wa ndani iliyozinduliwa mkoani Mbeya.
Tengeneza alisema Bodi
ya Utalii ilifanya utafiti mwaka 2006 na kubaini kuwa idadi kubwa ya Watanzania
hawatembelei vivutio vya Utalii vya ndani na badala yake wanajua kazi ya Utalii
ni ya wageni kutoka nje ya Nchi.
Alisema baada ya
kugundua uwepo wa changamoto hiyo Bodi ilianzisha kampeni mbali mbali za
kuhamasisha utalii wa ndani mwaka 2007 ambapo idadi ilianza kuongezeka kutoka
watalii 250,000 hadi zaidi ya 800,000 sasa.
Geofrey Tengeneza |
Twiga |
Alisema matarajio ya
Bodi ni kuona utalii wa ndani unaingiza pato kubwa kwa Taifa bila kutegemea
Utalii wa Kimataifa hivyo kuendelea kuendesha kampeni zingine zaidi.
Alisema kutokana na
kuonekana Wananchi bado wanahitaji elimu zaidi kuhamasishwa kutembelea vivutio
vya utalii vya ndani Mei 3, mwaka huu Bodi ilizindua kampeni mpya.
Aliitaja kampeni hiyo
ambayo ilizinduliwa katika Mkoa wa Kigoma na kuendelea katika mikoa minne kuwa
ni “Utalii wa ndani uanze na mtanzania mwenyewe”.
Aliongeza kuwa baada ya
kuzindua kampeni hiyo mkoani Kigoma Bodi ilizindua tena katika Mkoa wa Iringa
na sasa Mbeya kisha Mkoa wa Mwanza.
Akizungumzia uzinduzi wa
kampeni hiyo katika Mkoa wa Mbeya alisema itafanyika katika viwanja vya Uhasibu
kuanzia majira ya saa moja jioni ambapo Agape Television Network(ATN) itakuwa
ikionesha matukio ya utalii kupitia skrini kubwa.
Aidha alitoa wito kwa
mashirika binafsi kujitokeza katika kuwekeza kwenye miundombinu ya malazi
kwenye maeneo yenye vivutio vya Utalii ili kuwavutia watu wanaotembelea.
Alisema kupitia kampeni
hiyo mashindano mbali mbali yataendeshwa ambapo washindi watapelekwa kwenye
hifadhi za Taifa kutembelea ikiwemo kujishindia zawadi mbalimbali.
Habari hii imendaliwa na Venance Matinya
SHARE
No comments:
Post a Comment