Kwanini Tanzania ni Masikini Miaka Zaidi ya 50 Baada ya Uhuru? Tumedharau Kilimo.
[Sehemu
ya 1 na ya Mwisho ya Hotuba ya ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (MB)
kuhusu Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2017/18]
Mheshimiwa Spika,
Serikali
yeyote makini lazima ihangaike na masuala yanayowahusu wananchi wake
walio wengi, na hapa Tanzania watu hao (walio wengi) ni Wakulima. Hivyo
basi, kipimo kikuu cha kuondoa umasikini wa Watanzania ni kuondoa
umasikini wa wakulima.
Sekta
ya kilimo ndio msingi wa Uchumi wa watanzania. Waziri wa kilimo katika
hotuba yake hapa ametuambia kuwa 65.5% ya watanzania wameajiriwa kwenye
kilimo au wanategemea kilimo kwa kipato chao cha kila siku, kwamba 100%
ya chakula nchi inategemewa kutoka kwenye sekta hii. Kilimo kinachangia
29.1% ya pato la taifa (GDP), karibia theluthi moja ya thamani yote ya
shughuli za Uchumi nchini kwetu.
Hivyo
basi, unapowekeza kwenye sekta ya kilimo unawekeza kwa theluthi mbili
ya watanzania. Unapokuza kilimo unakuza uchumi wa theluthi mbili ya
watanzania, na unapoacha kilimo kishuke maana yake umewafukarisha
theluthi mbili ya Watanzania.
Kwa
mujibu wa wataalamu wa Uchumi, ili kupunguza umasikini Tanzania kwa
kiwango kikubwa, sekta ya kilimo inapaswa kukua kwa asilimia zaidi ya 8%
angalau kwa miaka mitatu mfululizo, na ukuaji huo uendelee kukua kwa
wastani wa 6% kwa muda miaka kumi mfululizo.
Hali
ikoje nchini? Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Kilimo, kwa miaka hii
mitatu mfululizo ukuaji wa Kilimo umekuwa ukishuka nchini (Na hivyo
ukuaji zaidi wa umasikini). Mwaka 2014 sekta ya Kilimo ilikua kwa 3.4%,
Mwaka 2015 Kwa 2.3% na Mwaka 2016 Kwa 2.1%.
Taarifa
ya ya robo mwaka ya Benki Kuu nchini (BOT quarterly economic bulletin)
inayoishia Disemba 2016 inaonyesha tofauti na anachosema Waziri. Kwa
mujibu wa tarifa ya BOT ni kuwa sekta ya Kilimo ilikua kwa kasi ya 0.6%
tu kutoka ukuaji wa 2.3%. 65.5% ya Watanzania wote wamejiajiri katika
sekta ya Kilimo, hivyo mdororo huu ya sekta ya Kilimo kutoka ukuaji wa
2.5% mpaka ukuaji wa 0.6% ni ishara mbaya mno kwa ustawi wa zaidi ya
robo tatu ya Watanzania.
Kwa
Vijijini 78% ya Watanzania wanajihusisha na Kilimo. Hii maana yake ni
kwamba wananchi wengi vijijini hawafanyi uzalishaji, jambo hili ni
hatari sana, ni dalili kuwa ufukara wa watu wetu unazidi. Ni kwa sababu
hii, pamoja na uchumi wetu kukua kitakwimu, 7% kwa mwaka, lakini bado
wananchi wetu walio wengi wanaishi kwenye dimbwi la ufukara. Maana
ukuaji huo wa Uchumi hauhusishi kilimo, hauhusishi zaidi ya robo 3 ya
Watanzania.
Tunajenga
uchumi unaowaacha pembeni theluthi 2 ya watanzania wote. Ukuaji huu
mdogo wa Kilimo unapaswa kuishtua Serikali kwani ni hatari sana, ni
hatari mno. Maana unajenga uchumi unaowaacha karibu zaidi ya robo 3 ya
Watanzania kwenye ufukara huko vijijini, ni uchumi unaopanua matabaka ya
mafukara na matajiri. Ndio msingi wa umasikini wa wananchi wetu miaka
50 baada ya Uhuru.
Tatizo
hasa ni nini? Kwanini ukuaji wa kilimo unashuka na hivyo umasikini wa
Watanzania kuzidi? Tatizo kubwa ni sera za Serikali pamoja na
utekelezaji wake. Serikali haiwekezi vya kutosha kwenye kilimo, Na hata
ikipanga mipango juu ya kilimo haitekelezi kabisa mipango husika.
Katika
bajeti ya mwaka 2015/16, bajeti ya mbolea ya Ruzuku katika Wizara hii
ilikuwa ni shilingi bilioni 78. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya
tano ilishusha fedha za ruzuku ya mbolea mpaka Shilingi bilioni 10
katika mwaka wa Fedha wa 2015/16. Hii ilikuwa ishara ya dhahiri ya
kukipuuza kilimo, kuwapuuza 65.5% ya Watanzania wote, kutokujali chanzo
cha 100% ya chakula chote cha Watanzania, kupuuza sekta inayochangia
theluthi moja ya uchumi wa Taifa.
Si
hivyo tu, katika bajeti ya mwaka 2016/17, Bunge liliidhinishia Wizara
hii fedha za miradi ya maendeleo katika kilimo kiasi cha bilioni 100.53.
Waziri amelieleza bunge hapa kuwa mpaka Mei 4, 2017 Wizara imepokea
shilingi bilioni 3.34, sawa 3.31% ya fedha zote za maendeleo ya kilimo.
Jambo hili linasikitisha mno, ni jambo linaonyesha kuwa hatuwajali
wanyonge wa Taifa hili.
Watanzania
wanyonge walikuwa na matumaini makubwa sana na Serikali hii, Rais
Magufuli alisema yeye ni rais wa wanyonge. Wanyonge nchi hii ni
wakulima. Matendo ya Serikali anayoiongoza yanaonyesha tofauti, Serikali
haiwajali wanyonge, inapuuza uchumi wa 65.5% ya wananchi wetu. Ni
vigumu kuondoa umasikini nchini ikiwa tutaendelea kuwadharau wakulima.
Kwetu
sisi ACT Wazalendo tunaofuata Ujamaa wa Kidemokrasia, Kilimo ndio sekta
ya msingi, ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, ni sekta nyeti ambayo
hatutaacha kuisemea. Hivyo pamoja na kuonyesha kasoro zote hizo za
serikali, tutatumia pia nafasi hii kutoa njia mbadala za kuondoa kasoro
hizo ili kuhakikisha uchumi wetu hauwaweki kando wananchi wetu wengi.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Bungeni Dodoma
Mei 20, 2017
SHARE
No comments:
Post a Comment