Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya utengenezaji wa jasi (gypsum) kutoka Ujerumani ya KNAUF, imedhamiria kuwekeza katika ukanda wa Afrika Mashariki huku ikipanga kuwekeza Sh. bilioni 30 nchini miaka michache ijayo.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa KNAUF Afrika Mashariki, Zacho na kubainisha kuwa hadi sasa wamewekeza Sh. bilioni 20 na ni matarajio yao kwamba watafikisha bilioni 30 muda mfupi ujao.
Aliongeza kampuni hiyo imeingia rasmi katika biashara ya jasi eneo la Afrika Mashariki na imechagua Tanzania kama makao yake makuu na ilianza rasmi shughuli zake nchini miaka mitatu iliyopita na tayari imeajiri wafanyakazi 150 na asilimia 99 kati yao ni Watanzania.
"KNAUF kwa sasa inafanya kazi katika nchi zaidi ya 200 hapa duniani lakini ofisi yake ya Tanzania ni ya kwanza miongoni mwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara. Tumefanya makao yetu makuu Tanzania kwa sababu imekaa katika eneo la kimkakati kijiografia na inaweza kuwa mlango wetu wa kuingia katika nchi zisizo na bahari zinazoizunguka na mbali zaidi.
"Sababu nyingine iliyotufanya tuichague Tanzania ni ukweli kuwa kuna hali ya amani na utulivu. Pia ina idadi kubwa ya watu ambao kwa mujibu wa takwimu zilizopo, inatarajiwa kuongezeka zaidi miaka ijayo," alisema.
Alisisitiza kuwa hiyo maana yake ni kwamba kutakuwa na soko la uhakika hivyo KNAUF imepanga kuendelea kubaki Tanzania kwa muda mrefu zaidi.
Mkurugenzi alisema kwa kawaida huwa wanatengeneza jasi kutokana na mahitaji ya wateja wao kwa wakati husika lakini kwa kuanzia, wameanza kutengeneza zenye ukubwa wa milimita tisa hadi 12 ambazo ni nzuri katika kukinga nyumba dhidi ya moto na unyevu unaosababishwa na maji ya mvua.
Kwa mujibu wa Georgios, KNAUF wameingiza nchini teknolojia mpya ya utengenezaji wa jasi ambapo wanaweza kuweka chuma mahali ambako zamani zilikuwa zinawekwa mbao.
Pia alisema teknolojia hiyo inatumika katika kiwanda chao kinachotumia teknolojia ya kisasa kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.
"Kwa kuzingatia hali ya uchumi ya Watanzania, pia tumetengeneza unga maalumu wa jasi ambao unaweza kutumika kwenye ujenzi hata wa nyumba za gharama nafuu," alisema.
Alisema kampuni hiyo ya kimataifa pia ina mradi maalumu wa kufundisha vijana kuhusu teknolojia mpya za ufungaji na utengenezaji wa jasi na lengo ni kutoa mchango wao kwa Tanzania.
"Mara wanapokuwa wamehitimu mafunzo yao, tunatoa vyeti vitakavyotambulika dunia nzima katika sekta ya ujenzi. Lengo letu hawa wanaofundishwa hapa waweze kuajiriwa popote duniani kwa sababu mafunzo yetu yana hadhi ya kimataifa," alisema Georgios.
Aliiomba serikali kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji. "Hatuombi upendeleo wowote kutoka serikalini isipokuwa mazingira wezeshi kwa ajili ya biashara zetu," alisema na kuongeza kwa sasa wanauza nje ya nchi asilimia nane ya bidhaa wanazozalisha huku lengoni kufikia asilimia 20 hadi 30.
Alieleza kuwa KNAUF Tanzania ni kampuni tanzu ya KNAUF yenye makao makuu Ujerumani, ikiwa na maeneo ya uzalishaji na ofisi za mauzo 150 katika nchi zaidi ya 60 ikiwa imeajiri wafanyakazi 26,000 duniani kote.
Mkurugenzi Mtendaji wa KNAUF Gypsum Afrika Mashariki, Zachopoulos Georgios akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi kuhusu shughuli za kampuni yake. Kushoto ni Saravanakkumar Thangavel ambaye ni Meneja Mauzo na Masoko wa kampuni hiyo kwa Afrika Mashariki.
SHARE
No comments:
Post a Comment